Jumamosi, 9 Agosti 2014

AZIMIO LA ARUSHA LITAREJESHA MAADILI NCHINI TANZANIA


 Dk. Camillus Kassala mtoa mada

Na Elias Mhegera
Imetabiriwa kwamba mara ifikapo mwaka 2017 Tanzania itarejea katika kulitambua rasmi Azimio la Arusha bila kujali rais atatoka katika  chama tawala Chama  Cha Mapinduzi (CCM) au upinzani.
Utabiri huo ulifanywa na mwanazuoni maarufu katika masuala ya uchumi, siasa na falsafa Dk. Camillus Kassala  alipokuwa akitoa mada kuhusu uchumi wa soko unaozingatia mahitaji ya jamii.
Alikuwa akitoa mada kwa wanafunzi wa chuo cha Mwalimu Nyerere Kivukoni waliokuwa katika maandalizi ya ziara ya mafunzo nchini Ujerumani. Siku ya Ijumaa tarehe moja, Agosti, 2014.
Wanafunzi kutoka chuo hicho na wale wa Ujerumani wamekuwa katika ushirikiano wa kutembeleana wakitumia kauli mbiu ya Pamoja. Miongoni mwa mambo wanayojifunza katika ziara hizo ni uongozi na maadili yake.
Katika semina hiyo ya maandalizi iliyoandaliwa na Pamoja kwa ushirikiano na shirika la - The Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS). Miongoni mwa masuala yaliyozungumziwa ni undeshaji wa uchumi katika muktadha wa soko huria lenye kujali ustawi wa jamii.  
Akiongea kwa kujiamini Dk. Kassala alisema kwamba uchumi wa soko huria usiozingatia jamii ndiyo umeifikisha Tanzania hapa ilipo kwa sasa ambapo kuna tofauti kubwa ya kipato kati ya watu wachache walionacho na wananchi walio wengi wasionacho.
Mada tajwa ililenga katika kuangalia wajibu wa serikali katika kuhakikisha usalama kwa rika la vijana, na kulinda utamaduni wao bila kuathiriwa na mfumo wa utandawazi.




























                                                   Bi Debora Maleyek akiuliza swali 

Katika mijadala iliyoendeshwa katika mdahalo huo ilijidhihirisha kwamba vijana wengi 

wanakutana na changamoto kubwa mara wanapohitimu masomo yao kwa sababu ni wachache wanaopata nafasi za kuendelea na masomo ya juu huku wengi wao wakiwa hawana ujuzi wowote wa kujiajiri au kukabiliana na changamoto za maisha.
Dk. Kassala anasema kwanza tatizo la Tanzania siyo uwepo wa sera bali ni sera zilizopo na zimekosa watekelezaji wake. Anasema kitendo cha vijana wengi kuyakimbia maeneo yao ya asili na kujitafutia ujira wao katika miji mikubwa ni kiashiria cha kukata tamaa kwa tabaka hilo muhimu katika jamii.
Anasema vijana ambao bado damu zao zinachemka huwa wakorofi pale wanapoburuzwa bila kuambiwa ni wapi wanakopelekwa. Na hasa inapotokea kwamba hawahusishwi katika maaamuzi ya namna ya kuendeshja uchumi.
Dk Kassala anakumbusha kwamba vijana hawajawahi kuhusishwa katika mjadala wa namna ya kujitafutia mitaji, wala ubinafsishaji, mizunguko ya pesa katika uchumi na namna mtu mmoja mmoja anavyoweza kushiriki katika uchumi wa taifa.
Anasema Tanzania imejiwekea malengo kwamba itakuwa na uchumi wa daraja la kati mara ifikapo mwaka 2025 lakini haoni dalili zozote zinazoashiria maono hayo. Kwa mfano, ni njia gani zitatumika, katika ngazi gani? na wahusika wakuu ni akina nani.
Mwanazuoni huyo anasema kwamba maono hayo yanatakiwa kuwamo katika bajeti ya taifa ya sasa, namna ya kuanzisha ajira, namna ya kukuza sekta binafsi, namna ya kukuza kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili, na namna ya uendeshaji wa taasisi za umma.
Mtaalamu huyu anasema kwa kawaida jamii imekuwa na tabia ya kutupa lawama kwa vijana bila kuangalia kwamba kabla ya kukengeuka kwao walikuwa wamejengewa mfumo gani wa kimaadili ambao hautoi uhakika wa usalama kwao na kutoa uhakika wa maisha yao ya baadaye.
Dk. Kassala anasema vijana wengi huwa na matumaini ya kupata mafanikio kwa haraka na hilo likishindikina ndipo vijana hujiingiza katika mambo maovu. Kimsingi anasema vijana wanatakiwa kuoneshwa kwamba wanakumbukwa na watawala.
Alisema njia nyingine kwa viongozi ni kujenga mazingira ya kukubalika ni kuzingatia maadili, uhuru, na kujiamini kunakoweza kuwafanya wajitegemee hata pale wanapokosa ajira.
Anasema Mwl. Nyerere alipotangaza Azimio la Arusha alilenga kuleta amani, kulinda mali binafsi lakini pia kuweka uwazi na uwajibikaji katika kusimamia ugavi wa raslimali za umma. Anasema kimsingi serikali inatakiwa kujenga mifumo ya kuwalinda wananchi wake ambao ndiyo wazilishaji kiasi kwamba hata wakipata hasara basi waweze kufidiwa.
“Wananchi ni lazima walindwe pale wanapopata hasara, inabidi tuthamini utu kabla ya faida,” anasema kukosa utu kwa tabaka la chini ndiko kumesababisha chuki kutokana na watawala kuwajali wawekezaji badala ya Watanzania.
Mtaalamu huyo anainisha mambo kadhaa ambayo ya naweza kuisadia Tanzania. Kwanza ni utu, kuheshimu maadili, na tamaduni za Kiafrika. Anasema serikali inatakiwa kuondokana na dhana ya kuthamini pesa kuliko utu.                                            

             Bw Deus Fidelis akichangia katika mada hiyo 
Vile vile anashauri kwamba jamii iepukane na tabia ya kuthamini amali za kimagharibi na kuwasahau Watanzania na tamaduni zao. Anashauri kwamba teknolojia mpya kama ipad na mambo mengine yanayohusisha mitandao ya intaneti yalenge kwenye mambo ya kujenga na wala siyo kuupotosha umma.
Nao vijana walipata nafasi ya kutoa michango ya mawazo na kuuliza maswali na hali ilikuwa kama ifutavyo: Bi Deborah Maleyek alitaka kujua Azimio la Arusha ni nini kwa nini lilishindwa kufanya kazi endelevu.
Akijibu hoja hiyo Dk. Kassala anasema kwamba azimio hilo lilikuja kama jibu muafaka katika kipindi cha mwanzo wa uhuru wa nchi hii baada ya kutokea  misigano ya kifikra ya namna ya kuendesha utawala wa nchi hii.
 Anasema wapo waliotaka kupata mafao kama waliyopata watawala wa kikoloni kabla ya uhuru huku wengine wakiona kwamba kufanya hivyo ni kuwadhulumu wanyonge.
“Nyerere aliona kwamba wenzake wanatamaa ya kuvaa viatu vya wazungu na akatafuta uhalali wa kufanya hivyo na azimio hilo likawa ndiyo msingi wa kuondokana na wale wasiotaka kujinyima kwa ajili ya walio wengi” anasema.  
Kassala anasema kwamba Mwl. Nyerere alihakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu ya bure katika ngazi zote na ndiyo maana kulikuwapo na elimu ya watu wazima. Msingi wa kufanya hivyo ulitokana na imani kwamba uelewa utasaidia katika maendeleo ya kiuchumi.
Lakini anawaeleimisha vijana kwamba miongoni mwa mambo muhimu aliyoyafanya Mwl. Nyerere ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata ardhi ambayo inasimamiwa na rais wa nchi.
Akijibu sehemu ya pili ya swali hilo msomi huyo anasema kwamba siyo kwamba Azimio la Arusha lilishindwa bali mapokeo ya siasa za kiliberali yalipongia nchini na katika hali ya kurekebisha uchumi baadhi ya watu wenye ushawishi waliweweseka, na kupotoka kiasi cha kushindwa kuona mazuri ya azimio hilo.
Naye mwanachuo Kamala Dickson aliomba kufahamu iwapo kufufuliwa kwa Azimio la Arusha ni jambo linalowezekana katika hali ambapo uchumi wa soko ndiyo unaotawala.
Akajibu swali hilo Dk Kassala anasema hilo ni jambo linalowezekana kwa sababu Tanzania inaendeshwa katika mfumo wa uchumi mchanganyiko uanaozingatia mahitaji ya kibinadamu.


Kwa upande wake Semainda Fredrick alitaka kujua matokea hasi ya mfumo wa soko ambayo labda Mwl Nyerere aliyahofia katika enzi za utawala wake. Akijibu swali hilo  Dk Kassala anasema kwamba hakuna mfumo usiokuwa na hitlafu zake lakini kilichokosena ni udhibiti wa serikali baada ya Mwl. Nyerere kustaafu.
Kwa maana hiyo anasema kwamba uchumi wa kijamaa bado unakubalika sehemu nyingi mpaka sasa isipokuwa udhibiti wa serikali hupishana sehemu moja hadi nyingine.
“Nimetembea hadi Venezuela nikashangaa kuona kwamba chini ya utawaka wa marehemu Hugo Chavez Azimio la Arusha lilitafsiriwa kwa Kireno ili kila mmoja alifahamu vilivyo kwa hiyo udhaifu haukuwa kwa nadharia yenyewe bali katika utekelezaji wake.
Lewis Mmbando anauliza iwapo kiwango cha maendeleo ya sayansi na teknolojia kinaruhusu mfumo wa soko huru kufanya kazi vizuri. Anasema jambo la msingi ni kukubalika kwa dhana zenyewe kwa Watanzania. 
                                                                                                                                      Bi. Agnes Kessy akiuliza swali

4.     
Naye Cacilie Radert –akiwakilisha taasisi ya KAS anasema kwamba historia ya Wajerumani iliwasidia sana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa sababu waliona wana wajibu wa kulinda hadhi ya taifa lao katika misingi ya uzalendo.
Anasema kitendo cha Ujerumani kutengwa baada ya vita ya pili ya dunia kiliwafanya wananchi wa taifa hilo kujiuliza wao wanaweza kuifanyia nini nchi yao. Hata hivyo anasema kwamba changamoto kubwa iliyokuwapo  ni kwamba kulikuwa na uhaba wa fedha za kuyasaidia makundi yasiyozalisha likiwamo kundi la wazee.
Vile vile Ujerumani ilipata kazi kubwa ya kupambana na wapinzani wake wa nje lakini pia namna ya kurejesha nguvu ya taifa katika uzalishaji.
1
3.  

Maoni 1 :

  1. Bado nasubiri kwa kina kuona iwapo kweli hapo mwakani 2017 Azimio la Arusha litarejewa

    JibuFuta