Jumamosi, 19 Julai 2014



Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu Said Mwema
JESHI LA POLISI WAZINGATIE MAADILI WARUDHISHE IMANI YA WANANCHI

Novemba 04, 2007 Mtanzania Jumapili

Na Elias Mhegera
Siku ya Jumamosi tarehe 20 Oktoba mwaka huu wananchi wa kijiji cha Ilongero mkoani Singida walijichukulia sheria mikononi, wakavunja kituo cha polisi kwa lengo la kumsulubu mtuhumiwa wa ubakaji na mauaji aitwaye Mile ambaye hatimaye wananchi hao walimuua.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema ametoa tamko kali kukemea kitendo hicho cha wananchi hao, nami nimeona ni muhimu kulizungumzia suala hilo.

Katika vipindi vingi vya matukio katika redio zetu na hata katika habari zitolewazo magazetini matukio ya ukatili yamekuwa yakijitokeza kwa kiwango kikubwa na cha kutisha.

Mara kadhaa kumekuwapo na ripoti zenye kuleta simanzi kwa sababu ya watu kufanyiana vitendo viovu vya ukatili, kuuana na mambo kadhaa yasiyopendeza ili mradi kila jambo baya la aina hiyo hutokana na utovu wa maaadili kwa namna moja au nyingine.

Nimeshawishika kuandika makala hii ili nitoe mchango wangu mdogo katika jamii katika kuimarisha amani na utulivu.

Kwa namna yoyote ile katika dunia ya waungwana tunayojitahidi kuijenga hatuwezi kuruhusu kitendo kama kile cha wananchi wa Ilongero.

Lakini kwa upande mwingine napenda kutanabahisha kwamba tukio la Ilongero linaonyesha kwamba kulikuwa na mazingira ya uzembe kwa mamlaka husika ambayo hatimaye yalisababisha wananchi wakaamua kujichukulia sheria mikononi mwao kwani mhusika alikuwa amewahi kufikishwa kituoni hapo mara kadhaa na kuachiliwa huru katika mazingira ambayo yaliwatatiza wananchi wa kijiji hicho.

Lakini tukio la Ilongero linaashiria kwamba kama mamlaka husika hazitachukua hatua madhubuti katika muda muafaka ipo hatari ya wananchi kuendelea kujichukulia sheria mikononi.

Ni mara kadhaa wananchi wamekuwa wakitoa malalamiko kwamba wapo baadhi ya wahalifu ambao mara wafikishwapo katika vyombo vya dola kama vile Jeshi la Polisi na mahakamani huachiliwa huru kwa madai kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuweza kuwaweka hatiani watuhumiwa hao.

Athari za muda mrefu ni kwamba watu hao hurudi mitaani wakaendeleza uovu wao na hata wakati mwingine huwatambia wananchi kwamba wao kamwe hawawezi kuguswa na dola.

Nashawishika kuamini kwamba upo ufa mkubwa katika utendaji wa vyombo vyetu vya dola ambao usipozibwa matukio kama hilo la Ilongero yataendelea kujitokeza mara kwa mara.

Sehemu kubwa ya matukio ya namna ile yamechangiwa na utovu wa maadili si kwa wanajamii pekee bali hata kwa watendaji katika vyombo vya dola ambao hukubali kupokea hongo na kuwaachia huru wahalifu.

Yapo masuala kadhaa yanayolalamikiwa mara kwa mara na wananchi kuhusiana na kukengeuka kwa maadili ya kitaaluma kwa baadhi ya askari katika Jeshi la Polisi kwa mfano tukio la hivi karibuni la askari polisi kumuibia mwenzake silaha akiwa lindoni, ama hata baadhi ya askari polisi kuwafichiua watoa habari (whistleblowers), haya ni mambo yanayolivunjia heshima jeshi hilo katika jamii.

Kwa hali yoyote ile iwapo Jeshi la Polisi au hata mahakama zetu hazitarekebisha baadhi ya mienendo na kukidhi matakwa na mahitaji basi tutaendelea kushuhudia vitendo vya uvunjaji wa sheria kwa wananchi kujichukulia sheria mikononi kama walivyofanya wananchi wa Ilongero hivi karibuni. Lakini tukio hilo ni muendelezo tu wa matukio ya aina hiyo ambapo mara kadhaa wananchi hujichukulia sheria mikononi na kuwachoma watu moto kwa kuwavalisha watu matairi na baadaye kuwachoma moto kwa kutumia petrol mafuta ya taa n.k. 

Ndiyo maana katika makala zangu kadhaa nimekuwea nikisisitiza kwamba iwapo mamlaka halali zitashindwa kutimiza wajibu wao basi walizi wa maadili watajitokeza na kuifanya kazi hiyo.

Walinzi hao wa maadili ninaowazungumzia hawaishi katika ombwe (vacuum) bali ni sisi wenyewe pale inapofikia kwamba tumechoshwa na uovu tukaamua kuirudisha jamii katika mstari unaostahili. Siku zote wanadamu wanapofikia hatua hiyo ni kwa sababu wanakuwa wamekatishwa tamaa na mifumo halali inayotakiwa kushughulikia masuala hayo.

Mtuhumiwa aliyeuawa aliyefahamika kwa jina la Mile alikuwa na uzoefu wa uhalifu. Kulingana na maelezo ya wananchi wa Ilongero waliyoyatoa kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu mtuhumiwa huyo aliwahi kufikishwha kituoni hapo mara tatu kwa tuhuma mbalimbali na mara ya mwisho alitoroka baada ya kuvunja dirisha kituoni hapo.

Wananchi hao walidai kwamba mtuhumiwa Mile amewahi kuhusika katika vitendo vya ubakaji kwa zaidi ya wanawake sita kijijini akiwemo mama yake mzazi! Kabla ya kuwabaka watoto wa familia moja hadi kuwaua. Inadaiwa pia mtuhumiwa huyo wa ubakaji pia alimbaka mwalimu wa wanafunzi hao katika shule ya msingi Mlama.

Ilidaiwa kwamba akina mama waliobakwa waliogopa kutoa taarifa kwa kuona kwamba jambo hilo lingewafedhehesha katika jamii yao. Ukimya wa akina mama hao ndio uliompa kiburi mtuhumiwa huyo wa ubakaji akashirikiana na mtuhumiwa mwenzake aitwaye Hamisi Juma na wakatenda tendo hilo la kinyama tarehe 14 ya mwezi Oktoba hadi kusababisha vifo vya mabinti hao.

Hasira na uchungu wa kupoteza watoto wao wapendwa viliwafanya wananchi hao wa Ilongero wapoteze subira na hatimaye wakaamua kuikamilisha kazi ambayo tayari waliona isingefanywa katika kiwango walichoona wao kinastahili kwa wauaji hao.

Kwa sasa baadhi wa wanakijiji hao akiwemo mwenyekiti wao Issa Swedy wameshikiliwa na dola kutokana na kujichukulia sheria mikononi mwao na kuwaua watuhumiwa wao.

Hata hivyo mbunge wao Nyalandu ameliomba Jeshi la Polisi pamoja na kuwakamata wanakijiji hao nalo kwa upande wake liwajibike kwa kutoa maelezo ya kina juu ya kutoroka na kuachiwa mara kwa mara kwa mtuhumiwa huyo. Ni dhahiri hapo kuna tatizo kubwa ambalo sisi kama wanajamii inatubidi tukune vichwa na kuangalia namna ya kuyazuia matukio ya namna ile yasije tokea tena katika jamii zetu.

Labda tunaweza kuanza kwa kujifanyia tathmini ya viwango vyetu vya maadili na kutafuta jinsi ya kurekebisha mapungufu tuliyonayo.

Maadili ni mfumo wa uhalalishaji wa matendo mema na kwa upande mwingine kuyakataa matendo yote mabaya. Kwa kifupi maadili ni dhana pana inayohusu uchanganuaji wa mema na mabaya.

Labda tatizo lililopo ni kudhania kwamba maadili ni yale tu yaliyoandikwa katika vitabu vya kigeni na kwamba sisi waafrika hatuna maadili yetu au labda hatujawahi kuwa nayo isipokuwa yale yaliyoletwa na wakoloni, wamisionari wafanyabiashara wa kiarabu walioleta uislamu Afrika na mambo kama hayo.

Ni muhimu tukafahamu kwamba nasi tuna maadili yetu ambayo yamejikita katika mila, desturi na tamaduni zetu. Kwa mfano kile kinachoitwa miiko ni msingi thabiti wa maadili ya muafrika, kwa maana hiyo kwa sababu miiko imekuwepo siku zote katika jamii zetu, basi kumbe inadhihirisha kwamba maadili yetu yamekuwepo pia tokea enzi za mababu zetu.

Matukio ya watu kuuana wakigombea mwanamke, au kufumaniana ugoni, kuchomeana ndani ya nyumba, kuwaadhibu wasiostahili, kwenda kinyume cha taratibu za jamii, visasi kuwekeana vikwazo, ubaguzi wa rangi, unyanyapaa, kuathiriana kisaikolojia, kughushi malipo, kuwaingiza wenzetu katika mikataba ya uongo, kutumia madaraka vibaya yote haya ni utovu wa maadili ambao huchangia katika matukio ya kudhuriana kila uchao.

Lakini matukio yote yaliyotajwa hapo juu yanaweza kuzuilika iwapo tutazingatia maadili ambayo tunarithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kabla hata ya kufikiria kwenda darasani kwa ajili ya somo la maadili.

Katika mila zetu za kiafrika maadili yalitokana na umoja wa kifamilia kwa sababu koo mbalimbali ziliishi katika eneo moja katika mfumo wa ukoo, koo kadhaa na hatimaye kijiji. Kwa maana hiyo kijiji kimoja au vijiji kadhaa vilitokana na koo zenye kushabihiana katika lugha (kabila), mila na desturi, na kwa maana hiyo maadili yao yalifanana.

Maadili yenyewe yalirithishwa kwa njia ya imani, sherehe za kimila, nyimbo hadithi na simulizi mbalimbali. Kwa ujumla maadili yaliyokuwepo yalitegemeana sana na tafsiri ya mazingira na matukio yaliyojitokeza katika jamii husika. Kwa mfano kuzaliwa kwa mtoto, maradhi, vifo, mazishi, n.k.

Kila jamii ililinda maadili yake kutegemeana na shughuli zilizoizunguka jamii hiyo kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, uhunzi n.k. Kwa maana hiyo hata miungu walioabudiwa walitokana na mazingira husika. Kwa maana hiyo kulikuwa na miungu wa mvua, mavuno, tiba, amani, n.k.

Maadili hayo ya kiafrika ndiyo yaliyowatuma waafrika wachague mlo wa aina fulani, makazi yao, mavazi, namna ya kufunga ndoa kuwapokea watoto wanaozaliwa, kuzikana na namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali katika jamii husika.

Kimsingi katika maadili ya kiafrika hakuna eneo lililokuwa limetelekezwa kwani kila jambo lilikuwa na majibu yake tayari tayari. Kwa maana hiyo watu walikuwa wamejiwekea tayari utaratibu wa kukabiliana na majanga yoyote ambayo yangejitokeza mbele yao.

Kulikuwepo na taratibu za kurekebisha ndoa, mahusiano ya kawaida katika jamii namna ya kukabiliana na misukosuko mbalimbali ya kimaisha, kuvumbua dawa, matumizi ya ardhi, matumizi ya alama na ishara mbalimbali, masuala ya posa na utoaji wa mahari n.k. Mambo yote hayo yalilenga katika utoaji wa maamuzi sahihi mara yanapojitokeza mapungufu fulani.

Lakini pia ni katika maadili hayo hayo ndipo ulipopatikana mgawanyo wa majukumu mbalimbali ya kijamii na kazi. Kulikuwepo na misemo mbalimbali na tungo zenye ujumbe murua katika kila tukio husika.

Kwa bahati mbaya imani za kishirikina pia zilitawala sana katika jamii zetu na ndiyo maana kila jamii ilikuwa na madawa kwa ajili ya kujilinda na maadui zao.

Kinachojitokeza katika matukio ya sasa ambayo yanaripotiwa na vyombo vya habari kila siku ni kupotea dira au muelekeo wa maadili yetu ambako kumechangiwa kwa kiwango fulani na kuhama hama kwa ajili ya kutafuta maslahi.

Kuja kwa ukoloni na dini za kigeni ambazo zote zimeyakandamiza maadili yetu kwamba ni ya kishenzi na kwa maana hiyo mvurugiko huo ndiyo unaochangia katika matukio mabaya yanayosababisha watu wachinjane kama kuku kila uchao.

Kwa hiyo ni lazima tufahamu kwamba kuna ombwe (vacuum) kati ya maadili yetu na yale ya kigeni au wakati mwingine ni kwa sababu watu wa makabila mbalimbali wanafunga ndoa au hata kuingiliana kijamii bila kufahamiana vizuri kwanza.

Kwa hiyo kuna umuhimu wa kuwianisha maadili yetu (dialogue) ili kuondoa migogoro isiyokwisha na pia ili tupate dira moja inayokidhi mahitaji yetu sote kwa pamoja.

Si lengo la makala hii kuzungumzia maadili katika kila taaluma au kuingia kwa undani sana juu ya dhana ya uadilifu, bali lengo ni kuyazungumzia maadili katika ujumla wake na kuangalia vyanzo vya matatizo katika jamii zetu na hatimaye kutoa ushauri wa nini kifanyike ili kurekebisha hali iliyopo kwa sasa, yaani kilio cha utovu wa maadili.

Ni vyema basi tukagusia maadili kama yanavyotazamwa na wenzetu wageni: wao wameyagawa katika sehemu kuu tatu; metaethics, normative ethics, na applied ethics. Makala hii imelenga katika kuyachanganua maadili haya kama yanavyotazamwa na wenzetu na kutoa tafsiri yake katika mazingira yetu.

Metaethics ni dhana ya kimaadili inayo chunguza vyanzo vya maadili, maana zake, dhana ya ukweli na utashi wa Mungu katika yale tuyatendayo. Normative ethics ni dhana inayozungumzia matendo zaidi na pia namna ya kurekebisha matendo hayo na kutoa mwelekeo mzuri zaidi.

Kwa upande mwingine applied ethics ni dhana inayozungumzia au kuangalia, kuchunguza, au kupima matendo yasiyo ya kawaida katika maisha ya jamii zetu. Kwa mfano utoaji wa mimba, ushoga, na usagaji, masuala ya mazingira kama vile ukataji wa miti ovyo, kuchoma misitu, adhabu ya kifo n.k.

Baada ya kujadili maadili ni nini, na kuwianisha maadili yetu ya kiafrika na yale ya kigeni, ni vyema sasa tukajadili ni kwa nini hutokea watu wakakiuka maadili japo wakati mwingine wanayafahamu, na pia wanazijua fika athari za kukiuka maadili hayo.

MAZINGIRA YA MAAMUZI

Japo hakuna dhambi inayohalalishwa kwa namna yoyote ile lakini hujitokeza kwamba binadamu akayumbishwa kisaikolojia na kujikuta katika mazingira yanayoweza kumfanya akiuke maadili. Tukio la mauaji la Ilongero linaweza kuhusishwa na suala la mazingira ya maamuzi yaani uchungu wa kupoteza watoto na hasira kali ya wananchi

Kwa mfano binti aliyemaliza darasa la saba akajikuta haendelezwi kwa njia yoyote ile, hapati taaluma, wala ajira rasmi ni rahisi sana kwake kuhalalisha kujiingiza katika biashara mbaya ya ukahaba. Japo binti huyo anaweza asifurahishwe sana na uamuzi wake huo lakini anaweza kuwa na kisingizio kwamba hakuwa na njia nyingine mbadala ya kujikimu katiaka maisha yake.

UBINAFSI
Wapo watu wengi katika jamii zetu waliotawaliwa na ubinafsi bila kufahamu kwamba kufanya hivyo ni kukiuka maadili. Hii ni kwa sababu mara nyingi watu wa aina hii hujitahidi kukwamisha mambo ya wenzao kila wanapoona kuna dalili za mafanikio fulani, watu wa aina hii hudhania kwamba ni wao pekee wanaostahili kupata. 
  
Kama hiyo haitoshi kundi la watu wa aina hii husumbuliwa sana na ghiliba na roho za kwa nini kwa wale wenye upeo mkubwa au wenye tabia ya kujihangaisha katika kutafuta maendeleo (aggressive). Watu wa aina hii hawakawii kuwadhuru wenzao pale wanapoona kuna dalili njema mbele yao.

Katika kundi la watu wenye tabia kama hizi ndiyo tunasikia vifo vya mara kwa mara kutokana na kutaka kuzibiana ridhiki. Yapo mambo kadhaa yanayoambatana na ubinafsi kama vile kuchongeana na hata kulishana sumu. Mambo ya aina hii hutokea sana kwa wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi katika taasisi mbalimbali wanaotaka kutukuzwa.

HASIRA NA PAPARA
Kuna nyakati ambapo watu hukiuka maadili kwa sababu ya kulipiza visasi, na maamuzi ya pupa. Kwa mfano wapo akina mama ambao huamua kuanzisha mahusiano na rafiki za waume zao pale wanapojiona kwamba hawakutendewa haki lakini mara nyingi maamuzi kama hayo huwashushia heshima zao mbele ya jamii badala ya kutatua tatizo linalowakabili.
Hali ya visasi vya namna hiyo inaweza pia kufanywa na mwanaume dhidi ya mke wake au hata kwa wachumba ambao bado hawajafunga ndoa. Wakati mwingine visasi vya namna hii huchangiwa sana na  wazazi, mawifi mashemeji na marafiki wa karibu wa wapenzi hao kwa kuanzisha chokochoko zisizokuwa na maana yoyote wala tija kwa wapendanao.

Wakati mwingine watu hujiingiza katika utovu wa maadili baada ya jamii kuwatolea hukumu isiyostahili kwa mfano binti aliye masomoni apatapo mimba husutwa na kuitwa majina mabaya ambayo yanaweza kumvunja moyo na kumfanya ajitumbukize katika vitendo viovu.

Hiyo utokea baada ya kuona kwamba jamii haikumtendea haki. Mambo kama haya pia huwakuta watu wenye ugumba ambao huhukumiwa na jamii katika namna inayowaumiza sana na kuwaelekeza katika vitendo viovu katika namna ya kujiliwaza.

ULAZIMISHAJI
Japo hali ya ulazimishaji wa ndoa imepungua kwa kiwango kikubwa lakini bado kuna watu ambao wana tabia za kuwalazimisha watoto wao wa kike na wakiume kuingia katika ndoa bila hiari zao na matokeo yake ni kusababisha misuguano isiyoisha, uzinzi, visasi kushambuliana n.k.

MALEZI DUNI NA KUTOWAJIBIKA
Malezi duni ndiyo chimbuko la maovu mengi tunayoyashuhudia katika jamii zetu, iwapo tunaajiri watu wenye malezi duni toka nyumbani tunajenga mazingira ya kuwa na watumishi waovu.

 Malezi duni huanzia katika familia moja moja lakini baadaye huathiri taasisi, mashirika na mwisho wa yote ni ubadhirifu wa mali ya umma ukatili, unyama, fitina na majungu. Labda hapo ndipo tunapoona umuhimu wa dini katika kujenga maadili mema kwa familia zetu.

Kuwajibika kwa mtu yeyote kunatokana na mambo kadhaa, kwa mfano nidhamu binafsi ya maisha, majukumu aliyokabidhiwa katika jamii kulingana na wakati husika lakini mara nyingi suala la kuwajibika linamhusu zaidi mtu mmoja mmoja yeye na nafsi yake.

Kwa mfano ni vipi mtu anawajibika kwa wazazi wake, kwa jamii yake, kwa taifa lake, kwa dini yake, kwa familia yake, au hata kwa nafsi yake mwenyewe. Kutowajibika ndicho chanzo kikubwa cha utovu wa maadili na katika hilo wahusika wanaweza kuwa wataalamu kama vile waalimu madaktari, waandishi wa habari, wachungaji, askari polisi n.k.

UDHALILISHAJI
Udhalilishaji upo wa aina nyingi kwa mfano kutowatambua watu wenye vipaji maalumu husababisha wakate tamaa na wakati mwingine wajiingize katika vitendo viovu kama njia ya kujiliwaza kama vile ulevi wa kupindukia, udhalilishaji ni pamoja na kuwanyima nafasi za kujiendeleza watumishi ambao wameonyesha dhamira hiyo na pia kukwamisha bahati zao fulani fulani.

Udhalilishaji ni pamoja na kuwabagua wenzetu katika misingi ya dini, rangi, kabila, kutotimiza ahadi zetu kwao, ikiwa ni pamoja na kuwanyima haki zao za kimsingi. Kwa mfano muajiri anayedai rushwa ya ngono kwa binti au mwanamke hiyo ni aina mojawapo ya udhalilishaji. Wakati mwingine hujitokeza watu wakakwamisha biashara za wenzao katika misingi hiyo hiyo ya chuki na udhalilishaji.

NINI BASI KIFANYIKE ILI KUREKEBISHA HALI HIYO?
Jambo la muhimu sana ni kuwa wakweli katika kila jambo tulitendalo, yaani kuwe na uwazi, bila kificho chochote. Tujue kutubu na kuwaomba radhi wenzetu mara tuwakoseapo.

Ni jambo jema hata kulipa fidia pale unapoona umemuathiri mwenzako kwa njia moja au nyingine. Kwa lugha nyingine haitoshi kwa (IGP), kuonyesha tu kwamba Jeshi la Polisi linao uwezo hata wa kuua pale linapokwamishwha katika kutimiza majukumu yake bali pia aonyeshe ni kwa jinsi gaini jeshi hilo litarudisha imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Tujenge utamaduni wa kuwa na shukrani na fadhila kwa wenzetu, kwa mfano mtu asiyetambua umuhimu wa kuwashukuru waliomsaidia katika jambo fulani huwavunja moyo watu hao na kusababisha wasitoe misaada kama hiyo kwa wengine.

Kwa upande mwingine tusitegemee kupewa shukrani kila tunapotenda wema kwani inaweza kujitokeza kwamba mara unapomtendea wema mtu utalipwa kwa njia nyingine na mtu tofauti kabisa na wakati mwingine mahali usipopategemea kabisa.

Mwisho kabisa tujenge tabia ya kuheshimu misingi iliyowekwa na jamii kama vile kushiriki katika misiba ya wenzetu, sherehe mbalimbali, kama vile arusi, kuwatembelea wagonjwa, tuheshimu sheria na taratibu za nchi tukiyazigatia yote haya matukio maovu ya watu kuuana na kudhuriana ya tatokomea mara moja.

Wakati tukiwa bado na kumbukumbu ya tukio la Ilongero ni muhimu pia tujiulize mtuhumiwa wa ubakaji alikuwa ni mtovu wa maadili wa kawaida au upo uwezekano alikuwa ameathirika pia kisaikolojia (psychopathy).

Vitendo vya mtuhumiwa huyo vinaashiria kwamba kuna uwezekana kwamba alikuwa na matatizo ya kisaikolojia labda kutokana na ukatili aliofanyiwa na wanadamu wenzake siku za nyuma ndipo naye akaamua kulipiza kisasi kwa njia hiyo aliyoitumia? Nakaribisha mawazo yenu

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0754 826 272
Na kwa barua pepe: mhegeraelias@yahoo.com


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni