Makala hii ilitumika katika
gazeti la Mtanzania Jumapili mnamo tarehe 11 Novemba mwaka 2007
Na Elias Mhegera,
Baada ya Rais Mstaafu wa Msumbiji Joachim Alberto Chissano (68),
kutangazwa kwamba ndiye mshindi wa kwanza wa tuzo ya Mo Ibrahim ya uongozi bora
zimezuka hoja kadhaa miongoni mwa watanzania na labda hata nje ya nchi yetu.
Baadhi ya wale wanaohoji ni ambao hawaoni umuhimu wa tuzo yenyewe
na pia lipo kundi ambalo linashindwa kuelewa vigezo vilivyotumika kumpatia tuzo
hiyo kiongozi huyo mstaafu, hiyo ndiyo mada ya makala haya.
Chissano amejinyakulia kitita cha Dola milioni 5 za kimarekani
labda niwe wazi kwamba dhamira yangu si kujikita katika mjadala wa tuzo yenyewe
bali zaidi kuangalia umuhimu wa tuzo hiyo kama upo na kama kweli Chissano
alistahili au labda aliyestahili kupata tuzo hiyo ni Mkapa kama baadhi ya
watanzania walivyotarajia.
Kwanza nasema tuzo hiyo ni muafaka kwa lengo la kujenga
demokrasia, haki za binadamu na utawala bora kwa ujumla.
Vile vile napenda tujadili juu ya uhalali wa Chissano kupokea tuzo
hiyo na kwa nini Mkapa hakuipata, tuwaweke katika mizani na kuangalia kama
vigezo vilivyotumika ni sahihi bila kusahau nguvu ya ushawishi ya wale
waliokuwa katika jopo la uteuzi.
Kabla hatujawalinganisha viongozi hao wawili yaani Mkapa na
Chissano ni vyema tukajadili japo kwa uchache kuhusu hoja mbali mbali
zilizotolewa kuhusiana na tuzo yenyewe.
Alfajiri ya Alhamisi tarehe 25, Oktoba 2007 nilisikiliza mjadala
ulioendeshwa kati ya BBC na Dkt. Azaveri Lwaitama wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kuhusiana na tuzo hiyo.
Dkt. Lwaitama alitoa changamoto kwamba tuzo hiyo ilitakiwa
ibadilishwe mfumo wake ili wahusika watokane na viongozi wote waliopata
kuongoza Afrika kuanzia enzi ya akina Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Kenneth
Kaunda, hadi waliostaafu hivi karibuni kama Mzee Nelson Mandela.
Kwa mtazamo wake walengwa wa tuzo hiyo walikuwa hawakidhi viwango
na kwa maana hiyo Chissano alikuwa bora miongoni mwa hao ‘bora viongozi’ na
wala siyo viongozi bora.
Kama hiyo haitoshi Dkt. Lwaitama alisema lengo lisingekuwa
kuwapatia mamilioni ya pesa viongozi hao ambao tayari wanazo pesa nyingi na
badala yake pesa hizo zingeelekezwa kwenye taasisi zao ili kuwasaidia wenye
mahitaji kama vile ‘scholarship’, huduma za kijamii n.k.
Sipingani na mawazo hayo ya Dkt. Lwaitama lakini napenda
kumkumbusha kwamba waingereza wanayo methali isemayo ‘amlipaye mpiga zumari
ndiye huchagua wimbo’ –‘He who pays the piper, calls the tune’.
Kwa maana hiyo mtoaji wa tuzo hiyo ndiye alikuwa na kauli ya
mwisho kwamba tuzo hiyo iwalenge watu wa aina gani. Kwa hiyo kama huo ndio
ulikuwa utaratibu, na viongozi 13 wastaafu wa kiafrika wakaingizwa katika
kinyang’anyiro hicho basi ni muhimu tukawajadili hawa wawili kwa sababu
wanatuhusu zaidi.
Chissano ni kwa sababu tayari amefungua njia kwa kupokea tuzo
hiyo, na Mkapa ni kwa sababu alikuwa rais wetu watanzania.
Lakini pia ni muhimu tuwafahamu baadhi ya viongozi waliongizwa
katika kapu hilo la marais wastaafu 13 waAfrika: Ukiwaondoa Mkapa na Chissano
wengine ni pamoja na Kumba Yala wa Guinea Bissau, Maaouiya Ould Sid Ahmed Taya
wa Mauritania, na Mathew Karekou wa Benin.
Wengine ni Albert Rene wa Seychelles, Gnasingbe Eyadema wa Togo,
Bakili Muluzi wa Malawi miongoni mwao watano waliingia madarakani kwa njia ya
mapinduzi ya kijeshi. Eyadema amewahi kupindua serikali mara mbili na pia
inadaiwa kwamba alihusika katika mauaji ya Sylvanus Olyimpio rais wa kwanza wa
Togo.
Baada ya kuizungumzia tuzo yenyewe; ni vyema tuwazungumzie pia
wahusika katika jopo la uteuzi. Walengwa wangu katika hili ni Katibu Mkuu
Mstaafu wa Umoja wa Mataifa. Kofi Annan na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Nchi
za Afrika (OAU/AU), Dkt. Salim Ahmed Salim.
Wengine ni Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson, Rais Mstaafu wa
Finland Martti Ahtisaari, Waziri wa zamani wa Uchumi wa Nigeria Ngozi Okonjo
Iweala.
Kabla sijawazungumzia Chissano na Mkapa napenda tumchambue Kofi
Annan Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa. Kupatikana kwake katika nafasi
hiyo kulikuja baada ya shinikizo kubwa la Marekani la kumzuia Dkt. Boutros
Boutros Ghali asigombee ukatibu huo kwa mara ya pili.
Nchi kadhaa za kiafrika zilishinikiza kwamba arejee tena lakini
jitihada hizo ziligonga mwamba na ndipo akaenguliwa na nafasi hiyo ikachukuliwa
na Dkt. Kofi Annan mwaka 1996.
Shinikizo la kumuondoa Dkt. Boutros Ghali na kuingizwa kwa Kofi
Annan kwa mchunguzi yeyote makini kunaonekana kulipangwa na wamarekani labda
kwa kudhania kwamba muda wote Annan angeendelea kuwa mtiifu kwao japo katika
utendaji wake kuna nyakati hakusita kuwakemea wamarekani kwa kuugeuza umoja huo
kama mhuri tu wa kutimiza haja zao…
Kofi Annan alikuwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa wa muda mrefu
lakini hakuwa mwakilishi wa nchi yake, Ghana, bali alikuwa mwajiriwa wa kawaida
(civil servant) ndani ya umoja huo kwa kujitafutia ajira hiyo yeye mwenyewe
binafsi.
Uteuzi wake uliambatana na
minong’ono kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kiafrika kwamba walikuwa
wamesalitiwa kwani walimuona Annan alikuwa ‘mkimbizi’ aliyeliasi bara lake la
Afrika akaoa ugenini na kuyahamishia makao yake ya kudumu Amerika na akalisahau
bara lake la Afrika, walimuona ni mtu aliyekwisha hamishika kifikra (uprooted).
Tukiachana na Annan tumzungumzie Dkt. Salim Ahmed Salim huyo ni Mtanzania
kutoka Pemba mahali ambako ndiko kumeathirika zaidi na mtafaruku wa Zanzibar
ambao Mkapa rais wetu mstaafu alishindwa kuutatua.
Salimu pia anashikilia rekodi ya katibu mkuu wa OAU/AU aliyekaa
kwa muda mrefu zaidi katika utumishi wake. Katika nafasi hiyo Salim Ahmed Salim
alikaa katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka 12 akiwa anakaribiwa kwa karibu
kwa rekodi hiyo na katibu mkuu wa kwanza wa umoja huo marehemu Diallo Telli
raia wa Guinea aliyekaa katika kiti hicho kwa kipindi cha miaka kumi kati ya
1963 hadi 73.
Jarida la Mambo toleo la
Agosti 1994 katika uchambuzi wake wa nani alistahili kuwa rais katika uchaguzi
wa mwaka 1995, lilimwagia sifa nyingi Dkt. Salim hali ambayo imekuwa tofauti
kidogo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2005.
Nitanukuu maneno mchache ya gazeti hilo kuhusiana na Dkt. Salim.
‘Salim hana matatizo na watu wa bara. Mama yake ni Mnyamwezi na ukoo wake
haujatoweka Tabora. Alipokuwa waziri mkuu (1985) alitekeleza suala la kuruhusu
mitumba ambayo ilisaidia wananchi wa kawaida katika kipindi hicho kutokana na
hali ngumu ya maisha iliyokuwepo’.
Ikumbukwe kwamba kipindi hicho Mwalimu Nyerere alikuwa bado yungali
hai, na ndipo rais wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa anamalizia
kipindi chake Mwalimu Nyerere aliuchukia sana ubaguzi wa rangi, na Mzee Mwinyi
alikuwa akitokea Zanzibar, mazingira yote hayo yalikuwa na faida nyingi kwake
(Dkt Salim).Mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM), mwaka 2005 ulikuwa na mazingira magumu kwa Dkt. Salim.
Baadhi ya makombora yaliyoelekezwa kwake ni ‘Uarabu’ wake na
kwamba baadhi ya ndugu zake walikuwa na nafasi kubwa serikalini na jeshini
katika nchi za uarabuni.
Yote hayo yalifanyika wakati Mkapa akiwa na nyadhifa zote mbili, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia mwenyekiti wa chama tawala CCM.
Kwa kuyazungmzia hayo simaanishi kwamba Dkt. Salim ameitumia
nafasi yake katika jopo la uteuzi kwa lengo la kulipiza kisasi bali nataka
kuonyesha kwamba yeye akiwa ni muathirika wa ubaguzi wetu na akiwa binadamu
mwenye hisia kama sisi wengine tulivyo alikuwa ana haki pia ya kujiuliza mara
mbilimbili utoaji wa tuzo ya kiongozi bora kwa Mkapa.
Tukiachana na hao viongozi wawili mahiri waliohusika katika jopo
la uteuzi. Sasa tuwageukie viongozi wetu ambao wamezua mijadala mingi hapa
Tanzania yaani Joachim Chissano na Benjamin Mkapa. Wapo walioona tuzo hiyo
ilistahili kumwendea Mkapa badala ya Chissano wapo pia wanaoona Chissano
alistahili kuipata tuzo hiyo.
Mijadala hiyo ndiyo imenifanya niwaweke viongozi hao wawili
wastaafu katika mizani ili baadaye tufikie muafaka kwamba ni nani kati yao
alistahili kupata tuzo hiyo. Lakini ni muhimu kwanza tujiridhishe kwamba ni kwa
nini Chissano ameipata tuzo hiyo badala ya Mkapa.
Joachim Alberto Chissano alikuwa ni miongoni mwa vigogo wa juu
kabisa ndani ya chama cha FRELIMO baada ya kifo cha Samora Machel mwezi Oktoba
mwaka 1986. Awali ya hapo Samora alisaini mkataba wa maelewano na serikali ya
makaburu (Nkomati Accord) tarehe 16 Machi 1984.
Lakini hakuna msukumo wa nguvu unaonishawishi niamini kwamba ni
yeye pekee alistahili kumrithi Samora najua hilo linaweza kukutana na upinzani
lakini wafuatiliaji wa mambo yalivyokuwa Msumbiji kwa wakati ule watakubaliana
nami kwamba waliostahili kumrithi Samora ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa FRELIMO
Marcelino Dos Santos vinginevyo angekuwa mjane wa Samora Machel Graca Machel.
Marcelino Dos Santos msomi mwenye kiwango cha shahada ya udaktari,
mwenye uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali za kimataifa na pia mshairi mahiri
alirushiwa makombora kwamba ni chotara wa kireno!
Graca Machel alitupwa nje ya mfumo kwa muda na baadaye alirudishwa
lakini pia kukiwa na minon’gono kwamba yeye aliwahi kuwa katika timu ya watu
waliotaka kuendesha mapinduzi dhidi ya serikali ya Jochim Chisssano.
Wapo wanaodai kwamba kifo cha Samora kilikuwa ni muendelezo wa
mauaji ya wakomunisti kama ilivyojitokeza kwa Amilcar Cabral, Patrice Lumumba,
Ernesto ‘che’ Guavara, Walter Rodney na wengineo hasa katika nchi za Latini
Amerika.
Rejea habari za The New Nation Septemba 4, 1992, na madai ya
aliyekuwa rais wa Russia marehemu Boris Yeltsin. Yeye alidai mauaji ya Samora
yalikuwa mauaji dhidi ya ukomunisti na alikuwa tayari kugharimia uchunguzi huru
juu ya ajali iliyochukua uhai wa Samora.
Mojawapo ya sifa anazopewa Chissano kwamba zimechangia kupewa tuzo
hiyo ni kuibadilisha nchi hiyo kutoka katika ukomunisti kwa hiyo tuamini kwamba
yawezekana hiyo ni zawadi maalumu kwake kwa kufanikisha kuua ukomunisti barani
Afrika?
Hoja hiyo inawiana na madai kwamba wapo viongozi ndani ya FRELIMO
waliohusika na mauaji ya Samora kwa ajali ya kupangwa kama ilivyofanyika
Pakistan kwa Jenerali Zia Ul Hug ambaye alimpindua na baadaye kumuua Zulfikar
Ali Bhutto waziri mkuu aliyekuwa kipenzi cha ‘walalahoi’ wa Pakistan
Hoja hiyo inaweza kuwa na maelezo ya ziada ya kisayansi kwamba
licha ya ukomunisti hata ule uamuzi wake wa ghafla wa kugeuza mwelekeo bila
kuwashirikisha wenzake ilikuwa ni sababu tosha ya wenzake kumuangamiza.
Historia inayo mifano mingi inayowahusu wote waliopata kuchukua
maamuzi ya namna hiyo (U-turn decisions), katika kusaini mikataba bila kuwashirikisha
wenzao kikamilifu au hata kwa kuonekana wameisaliti misimamo yao ya awali.
Watetezi wa hoja hiyo wanadai kwamba viongozi wote waliopata
kufanya maamuzi ya namna hiyo baadaye waliuawa kwa kuhujumiwa na wenzao ndani
ya mfumo,mifano michache inayotolewa ni ule wa Camp David wa tarehe 17 Septemba
1978 kati ya waziri mkuu wa Israeli kwa wakati ule Menachem Begin na Rais Anwar
Al Sadat wa Misri.
Kitendo hicho kilihesabiwa na baadhi ya waarabu wenzake kwamba ni
cha kisaliti na hivyo Sadat aliuawa kwa kumiminiwa risasi tarehe 6 Oktoba 1981.
Jambo kama hili liliwarudia waisraeli pale waziri mkuu wao Yitzhak
Rabin aliposaini mkataba wa maelewano na kiongozi wa mamlaka ya wapalestina
Yasser Arafat kwanza kwa maelewano na wapalestina ya tarehe 20 Agosti 1993
(Oslo Accords) na baadaye tarehe 13 Septemba 1993 katika kile kilichoitwa
‘Declaration of Principles’ au kwa jina jingine Gaza-Jericho Washington Peace
Agreement.
Kwa baadhi ya waisraeli Rabin alionekana ni msaliti kwani
maelewano hayo yalihusu kuachia baadhi ya maeneo yanayokaliwa na waisraeli kwa
wapalestina hivyo naye aliuawa tarehe 4 Novemba 1995 kwa kupigwa risasi.
Tukirudi kwa suala la Msumbiji ni vipi basi makaburu waliendelea
kumuunga mkono Alfonso Dhlakama wakati tayari kulikuwa na maelewano ya Nkomati?
Maelezo ya hilo ni kwamba kuingia kwa Chissano si kwamba kuliondoa
tu ukomunisti Msumbiji lakini pia hakukutekeleza maelewano ya Nkomati ndiyo
maana makaburu waliendelea kukifadhiri kikundi cha RENAMO hadi muafaka
ulipofikiwa mwaka 1992 na kikundi hicho kikatambuliwa kama chama cha siasa.
Lakini pia suala la kumalizika kwa vita kati ya FRELIMO na RENAMO
linafaa liangaliwe katika mtazamo wa kihistoria kwamba kusambaratika kwa Soviet
Union ya zamani ndiko kulichangia kuwapo kwa mabadiliko kadhaa duniani.
Kwa mfano kuachiliwa kwa Mzee Nelson Mandela, ambako kulihitimisha
utawala wa makaburu kisiasa lakini kumewanufaisha zaidi kiuchumi “Makaburu” kwani
sasa wanamtandao mkubwa wa uwekezaji wakizidi kupanda kaskazini mwa bara la
Afrika.
Maelezo yangu marefu ambayo kwa msomaji mwingine anaweza kuona
kwamba hayawiani na uteuzi wa Chissano ni katika kujenga hoja kwamba
inawezekana kwamba japo wenye ushawishi mkubwa zaidi katika uteuzi wa Chissano
ni waafrika wenzetu lakini pia upo uwezekano kwamba kulikuwa na ushawishi wa
nje katika uteuzi huo.
Maana yangu ni kwamba kumalizika kwa mgogoro wa FRELIMO na RENAMO
hakukutokana tu na busara za Chissano lakini pia ni kwa sababu yeye pia
aliusambaratisha ukomunisti nchini mwake.
Sababu nyingine ni ukweli pia kwamba Chissano hajawahi kutuhumiwa
kwa udikteta nchini mwake na vyombo vya habari vya ndani na nje ya Msumbiji
tofauti na viongozi wengine wa kiafrika kama ilivyokuwa kwa Mugabe au hata kwa
ukiukwaji wa haki za binadamu kama ilivyokuwa kwa Mkapa kama nitakavyoeleza
hapo baadaye.
Licha ya hayo ni jinsi ambavyo Chissano amefanikisha zoezi la
mpito kutoka kwenye serikali yake hadi kwa serikali iliyopo sasa ya ‘Comrade’
Armando Emilio Guebuza kwa njia ya amani, na katika uchaguzi ambao haukuleta
malalamiko makubwa kama ilivyo katika chaguzi za nchi nyingine.
Tusisahau pia kwamba wakati Rais Mugabe alipoamua kunyakua
mashamba ya walowezi waliopo nchini mwake na kuyakabidhi kwa wazalendo,
Chissano aliwakaribisha walowezi hao nchini mwake ambapo wamenunua ardhi bikira
(virgin land) ambayo inarutuba na haijawahi kulimwa kabisa.
Kilichofanyika ni kuyategua
mabomu yaliyokuwa kwenye ardhi hiyo ambayo yalitegwa wakati wa vita ya wenyewe
kwa wenyewe ya muda mrefu.
Lakini siyo kwamba Chissano hakupata upinzani wa hapa na pale
kutoka kwa wanajopo waliohitimisha kwa kumpatia tuzo hiyo.Kwa mfano baadhi ya
wanajopo walidai yeye hajawahi kukemea vitendo vinavyofanywa na jirani yake
Mugabe.
Pia tuhuma zinazomhusu mtoto wake kwamba alihusika na mauaji ya
mwandishi wa habari Carlos Cardoso tayari Chissano amewahi kutoa ruhusa kwa
mamlaka husika kama vile polisi na mahakama kuchukua hatua bila kujali kwamba
mhusika ni mwanae kwani tayari huyo ni mtu mzima.
Doa kubwa la Mkapa ni suala la mgogoro wa Zanzibar ambalo alionekana
kulifumbia macho, au kushindwa kuchukua hatua madhubuti ambazo zingeweza kuleta
ufumbuzi wa kudumu. Sasa kwa sababu mojawapo ya sifa kuu iliyompatia tuzo
Chissano ni uwezo wake wa kutatua mgogoro wa chama chake na RENAMO.
Hata kama ulikuwa
umechochewa kutoka nje lakini kushindwa kwa Mkapa kutatua mgogogoro wa Zanzibar
kati ya CCM na CUF mahali ambapo mmoja wa wanajopo anatoka yaani Dkt. Salim ni
sababau tosha ya kumnyima sifa ya kupata tuzo hiyo.
Lakini kwa upande mwingine doa jingine kubwa kwa utawala wa Mkapa
ni mauaji yaliyotokea Zanzibar Januari 26 na 27 mwaka 2001. Ambapo zaidi ya
wafuasi 20 wa chama cha upinzani CUF waliuawa na polisi.
Hilo lilikuwa ni doa kwake kwa sababu Zanzibar ni sehemu ya
Tanzania kufuatia Muungano wa mwaka 1964. Pia Mkapa anatuhumiwa kwa
kuvigandamiza vyama vya upinzani pamoja na uchanga wa vyama hivyo. Kwa mfano
matumizi ya rasilimali kubwa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Sengerema mwaka
1998.
Matukio mengine ni kushindwa kwake kuwalinda raia wake kama vile
kupigwa kwa makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha UDP, Dkt Fortunatus
Masha mwezi Oktoba, 2000.
Matukio mengine ni pamoja na kukamatwa kwa mwenyekiti wa chama cha
TLP, Augustine Mrema na Rais wa Chama cha Wanasheria za Mazingira (LEAT) Nshala
Rugemeleza baada ya kutoa madai kwamba wachimbaji wadogo walifukiwa na kufa
huko Bulyanhulu mwaka 1996.
Pamoja na hayo ni hizi tuhuma za ufisadi ambazo bado zinaendelea
kufumuliwa dhidi ya serikali ya Mkapa. Kwa hiyo ukiwaweka katika mizani Chissano
na Mkapa kwa kuzingatia vithibitisho hivyo vichache tulivyonavyo ni dhahiri tuzo
hiyo inastahili kwenda kwa Chissano na wala siyo kwa Mkapa.
Lakini kukosa tuzo hiyo pekee hakuondoi mazuri ambayo Mkapa kama
kiongozi amewaachia Watanzania kama vile mfumo mzuri wa miundo mbinu, sekondari
za kata, majengo mapya ya serikali, uwanja wa kisasa wa mpira, pia
ameshughulikia kwa kiwango kikubwa matatizo ya wakimbizi kutoka katika nchi za
jirani zilizokumbwa na machafuko.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 826 272

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni