\
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Tanzania Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
Muft Mkuu Shekhe Shaban Simba
28/11/2013 | Elias Mhegera
KATIKATI ya Novemba mwaka huu viongozi wa
kiroho na wawakilishi kutoka taasisi za dini walikutana katikati ya Jiji la Dar
es Salaam katika Hoteli ya Accomondia kujadili mustakabali wa amani.
Viongozi hao kutoka Zanzibar na makao makuu
ya Baraza la Madhehebu ya Dini kwa Ajili ya Amani Tanzania (IRCPT)
walikutanishwa chini ya ushirikiano na asasi ya Konrad Adenaeur Stiftung (KAS)
kutoka nchini Ujerumani.
Mjadala juu ya vyanzo vya chokochoko za udini
kama ilivyotarajiwa tokea awali haukuwa mwepesi kutokana na kila upande kati ya
Waislamu na Wakristu kujitetea au kujisafisha kila ulipoguswa.
“Mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba
Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani kwa sababu waamini katika taasisi zenu
za dini wana imani kubwa na nyinyi,” anasema Stefan Reith, Mkurugenzi Mkazi wa
KAS.
Reith anasema taasisi yake imekuwa ikiandaa
mikutano mingine kama huo wa siku hiyo na yote imekuwa na mafanikio makubwa.
Alikuwa na mategemeo kwamba mkutano huo utakuwa na mafanikio kama ile
iliyotangulia.
Naye Jaji mstaafu, Raymond Mwaikasu,
aliwaomba washiriki katika warsha hiyo kuwa huru katika kutoa mawazo yao kwa
sababu kwa kufanya hivyo ndipo watapata kuyaondoa madukuduku yao ili yafanyiwe
kazi vizuri.
Naye Sheikh Haji Mussa kutoka Wakf and Trust,
Zanzibar anashukuru kwamba sasa walau kuna utulivu visiwani Zanzibar kwani kwa
miaka kadhaa kumekuwa na hali tete ya kiusalama inayosababishwa na mambo ya
udini.
Wahudhuriaji walipata mwanya wa kukumbushana
jinsi ambavyo wazo lao lilisababisha kuanzishwa kwa Benki za Wanavijiji
(Vicoba), lengo likiwa ni kuwasaidia watu wenye kipato cha chini hususan
wajasiriamali.
Kutoka katika Kituo cha Uhusiano Mwema wa
Imani Zanzibar alikuwapo Mratibu wake, Daniel Madsen, aliyesema kwamba uhusiano
mzuri wa watu wa imani tofauti ni jambo linalotakiwa kujengwa tokea watu
wanapokuwa katika umri mdogo.
Anasema kwamba kituo chake kimekuwa
kikitimiza azima hiyo kwa njia ya vitendo kwa kuendesha kampeni mbalimbali
ikiwamo michezo kwa watoto. Akizungumzia historia ya kituo chake anasema kilianzishwa
mwezi Aprili mwaka 2009 na kujiweka sawa zaidi kiutekelezaji mnamo mwaka 2010.
“Tunajivuna kwamba leo kituo chetu kimekuwa
ni kimbilio kwa wengi wanaotaka kupata taarifa mbalimbali kwa kusoma nyaraka,
kujifunza kompyuta, kujifunza lugha ya
Kiingereza na hata kwa ajili ya utafiti,” anasisitiza.
Padri wa Kanisa la Kianglikana, Emmanuel
Masoud, ambye pia ni katibu msaidizi katika Kamati ya Maridhiano ya Dini
Zanzibar anasema visiwa hivyo vilijijengea umaarufu mkubwa kutokana na ukarimu
wa watu wake na hata watalii wengi wakaja visiwani humo na wengine kwa ajili ya
mashindano ya uvuvi.
Anasema leo hali imebadilika kidogo na watu
hawana tena uhakika wa usalama wao moja kwa moja bali katika hali ya mashaka
mashaka. Anasema hali hiyo ndiyo imesababisha leo Zanzibar kuwa kituo kikuu cha
wauzaji wa dawa za kulevya na hata biashara ya pembe za ndovu ingawaje Zanzibar
hakuna hata tembo mmoja.
Anasema vitabu vyote vitakatifu kwa Wakristu
na Waislamu vina sisitiza juu ya amani lakini leo ni kinyume chake na ana
wasuta wanasiasa kwamba wamechangia katika uhasama wa kidini visiwani humo.
Anayataja matukio yaliyoleta sintofahamu
visiwani humo kuwa ni pamoja na mauaji ya Padri Evarist Mushi wa Kanisa
Katoliki pamoja na kushambuliwa viongozi wengine wakiwamo Sheikh Fadhili Soraga
aliyemwagiwa tindikali.
Anasema matukio yote haya pamoja na uchomaji
wa makanisa si utamaduni wa Wazanzibari bali wa watu wabaya wenye lengo la
kuondoa amani na kuchafua jina zuri la nchi hiyo.
Pia alitumia muda huo kuzishukuru taasisi
zote ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba kuna maridhiano
ya watu wa dini tofauti nchini Tanzania Visiwani hususan; KAS na taasisi ya
Norwegian Church Aid.
Naye Katibu Mtendaji wa IRCPT, Mch. Thomas
Godda, alisema maridhiano ya dhati kati ya watu wa imani tofauti yatapatikana
tu kwa viongozi wa taasisi husika kupitia BAKWATA, TEC, CCT, HINDU, BAAHAI na
PCT kukaa pamoja na kutafuta ufumbuzi
wa matatizo yaliyopo.
Naye Julian Laurent, mtumishi katika Tume ya
Haki za Binadamu (CHRAGG) na mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Kuzuia Mauaji ya
Kimbari (NCPG), alishauri kwamba njia nzuri ya kuzuia chokochoko za dini ni kwa
viongozi wa madhehebu mbalimbali kuhubiri amani kwa waamini wao.
“Kamati yetu inaamini kwamba viongozi wa
kiroho wana mchango mkubwa sana katika kuzuia majanga ya vita na wakimbizi,
tunaomba mshirikiane na vyombo vya habari katika kufanikisha hilo,” anashauri.
Naye George Bagomwa kutoka IRCPT alishangaa
kuona kwamba Jeshi la Polisi katika siku za hivi karibuni limeshindwa kuwanasa
wale wote wanaochoma makanisa na hata kuwamwagia watu tindikali kama ilivyotokea
Zanzibar.
Lakini Ditrick Rutashobya kutoka Kitengo cha
Vijana cha IRCPT anasema kwamba matukio ya kuharibiwa mali za Wakristu ikiwamo
kuchomwa kwa makanisa ni matokeo ya propaganda hasi za wanasiasa zilizotumika
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Madai kwamba Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alikuwa anagombea ili kuwakilisha masilahi ya
Kanisa Katoliki kwa sababu yeye alipata kuwa padri, dhidi ya Jakaya Kikwete wa
CCM ambaye ni Mwislamu zimeacha makovu yasiyotibika, kampeni za aina hiyo
hazifai na wala zisije zikarudiwa tena,” alionya.
Naye Mratibu wa Miradi wa Chama cha Waislamu
Wanataaluma (TAMPRO), Said Ngolola, anadai kwamba Waislamu wana dukuduku kwa
sababu serikali imekuwa ikizisaidia fedha taasisi za Wakristu na kuzibagua za
Kiislamu.
Alikwenda mbele zaidi na kudai kwamba sasa
hivi baadhi ya wanavyuo Waislamu wameamua kususia mikopo inayotolewa na Bodi ya
Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) kwa sababu imeambatana na malipo yenye riba, jambo ambalo halikubaliki
katika Uislamu.
Hoja hiyo ilionekana kumgusa Pd. Damas Mtoi
wa Kanisa Katoliki Zanzibar ambaye alisema watu wasiongozwe na hisia katika
kutoa michango yao kwa sababu serikali imekuwa ikizifadhili taasisi zinazotoa
huduma kwa umma zikiwamo hospitali na vyuo vikuu na wala si kwa sababu ni mali
za Wakristu.
Ngolola alipata faraja mara baada ya mjumbe
wa bodi ya IRCPT Mama Hindu Lila kudai kwamba serikali imekalia madai 19 ya
Waislamu ambayo wameyalalamikia katika
awamu zote za uongozi wa nchi.
Anasema kwamba mnamo mwaka 1999 Waislamu
walikutana na Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa na wakamfahamisha madai yao
lakini hayajafanyiwa kazi mpaka leo ingawaje kiongozi huyo wa nchi aliahidi
kufanya hivyo.
Naye Mama Shamim Khan, aliyepata kuwa mbunge
na naibu waziri alisema kwamba Waislamu na Wakristu wamekuwa na mahusiano ya
karibu kwa muda mrefu lakini ghafla tu umezuka uhasama, jambo ambalo
linaashiria kwamba kuna uchochezi umefanyika.
Hoja ya kwamba Wakristu wanapendelewa na
serikali ilionekana kuzua mjadala mkali kwa kiwango chake huku Wakristu wakidai
kwamba watu wasitawaliwe na hisia bali wachimbe ili kupata ukweli zaidi juu ya
jambo hilo. Ndipo Madsen kutoka Zanzibar akaonyesha uhusiano uliopo kati ya
dhana, hisia na tabia.
Huku akitumia mchoro wa pembe tatu,
alionyesha kwamba dhana ikijengeka na ikaungwa mkono na hisia inaweza
kusababisha matendo mabaya. Japo hakuwa muwazi sana lakini yaelekea alitaka
kuonyesha kwamba mashambulizi dhidi ya taasisi za Kikristu yametokana na mzingo
huo wa mawazo.
Mhariri mkongwe, Lawrence Kilimwiko,
hakumng’unya maneno aliposema kwamba baadhi ya wanasiasa hutafuta kuungwa mkono
na wafuasi wa dini zao pale wanapokuwa wameshindwa kukidhi matarajio fulani.
Naye mhariri mwingine mkongwe, Mboneko
Munyanga, alionya kwamba wale wanaodhania kwamba wanaweza kuondoa amani ya
Tanzania kwa kupenyeza udini wamechelewa, kwa sababu kuna miingiliano mingi ya
kifamilia kati ya Waislamu na Wakristu.
Paul Shemshanga kutoka (PCT) alionya juu ya
kuwapo lindi kubwa la wahubiri ambao japo hawajapata mafunzo yoyote darasani
lakini wanaushawishi mkubwa kwa sababu wamezaliwa na nguvu fulani za kiroho.
Dk. William Kopwe kutoka CCT anashauri kwamba
kuwepo na uratibu mzuri wa watu wote wanaoendesha shughuli za kiimani ikiwamo
mihadhara ili kuzuia baadhi ya watu wenye nia ovu kufanikisha mambo yao.
Naye Mwendesha Mkutano huo, Salim Zagar,
akisoma majumuisho ya michango alisema kwamba wazo la viongozi wa kiroho
kukutana na Rais Kikwete limeonekana ni la muhimu sana.
Pia alisoma maoni kwamba mali za umma
zisitumike kwa manufaa ya dini yoyote kwa njia za kibaguzi. Na kwamba wajumbe
waliona kuna umuhimu wa masuala ya amani kwa watu wa dini tofauti yawe katika
mitaala ya elimu ya sekondari.
Wajumbe walikemea vikali tabia za uchochezi
wa kidini kutoka kwa wanasiasa, na propaganda zote zenye kuchochea udini
ikiwamo hata katika nyumba za ibada.
Kulikuwa na pendekezo kwamba serikali
iitambue rasmi IRCPT kama chombo halali cha kushughulikia maridhiano ya dini
kwa watu wa imani tofauti.
Kulitolewa ushauri kwa serikali kuangalia
upya suala la elimu na kuondoa umaskini kwa sababu mambo haya yanachangia kwa
kiwango kikubwa watu kushawishiwa kwa kudanganywa au hata kwa kupewa fedha
kidogo.
Viongozi wa kiroho walionyesha nia ya
kuitisha mkutano wa hadhara kwa watu wa
madhehebu yote kwa lengo la kuzungumzia amani. Hasa kwa kuzingatia kwamba
Tanzania inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014, na Uchaguzi Mkuu
2015.
Imeshauriwa kwamba wadau wengine kama vile
asasi za kiraia, wasomi, na vyombo vya habari vitoe mchango katika kuzungumzia
masuala ya amani na kupinga uchochezi wa kiimani.
Kuanzia sasa iwe ni marufuku kwa mtu yeyote
kuhubiri dini yake huku akiwa ameshikilia kitabu cha imani tofauti. Kanda za
redio na video zenye kuchochea udini zipigwe vita mahali pote ikiwamo katika
nyumba za ibada.
Naye kiongozi mwandamizi kutoka KAS, Richard Shaba anasema ili Tanznaia iendelee
kuwa na amani watu wabadilike na kuanza kuifikiria amani bila kujali tofauti za
dini, hisia na hata ufuasi wa dini zao.
Tuwasiliane: mhegera@gmail.com Simu-0754-826227


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni