Na Elias
Mhegera
Hivi karibuni nilichangia hoja katika mada iliyokuwa
ikiendelea kati ya mwanasiasa kijana na mwandishi wa mmoja wa kike. Katika
hitimisho langu juu ya mzozo huo nilisema kwamba mwandishi huyo alikuwa
amedandia farasi wa huruma kwa kusema kwamba mpinzani wake mwanasiasa kijana
anadharau waandishi wanawake.
Ni pia nikasema kwamba
mwanasiasa huyo hakumkosoa mwandishi wa kike kwa sababu ni mwanamke bali kwa
kuangalia udhaifu wa hoja zake. Baadaye hoja hiyo ilimfurahisha mhariri mmoja
wa gazeti la Mawio kuipenda hoja
yangu.
Mhariri huyo akaniomba niingalie hoja yangu katika muktadha
wa mvutano kati ya CCM na UKAWA ni nani alikuwa anadandia farasi wa huruma
katika kupata katiba mpya?
Kama tunavyofahamu wabunge wa vyama vilivyounda Umoja wa
Katiba ya Wanachi (UKAWA) waliamua kuondoka bungeni baada ya CCM kuanza
kuyagandamiza mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya iliyokuwa chini
ya jaji Joseph Warioba ambaye pia ni
waziri mkuu mstaafu.
Kwa kweli swali hilo lilikuwa ni la mtego kidogo ingawaje
jibu lake lipo wazi kabisa. Nami nikaaanza kwa kujibu kwamba mtu wa kwanza
kujibu hilo siyo mimi bali Mzee Jenerali Ulimwengu na tena katika miaka ya mwanzo
kabisa ya 90.
Mzee Ulimwengu alipata kuandika makala katika miaka ile akisema
kwamba baadhi ya wanasiasa wa CCM wa leo ni wanafiki na akaitetea hoja yake
akitoa ushahidi wa “makasri” kama alivyoyaita yeye akimaanisha majengo makubwa
makubwa ambayo ndiyo kwanza yalikuwa yameanza kuchipuka kama uyoga huko
Mikocheni na Masaki.
Ulimwengu alisema kwamba wanasiasa hao wa CCM walikuwa
wameficha mamilioni ya pesa ambayo baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu sasa
walianza kuyatumia kwa kuporomosha maghorofa kibao na hata dhana yenyewe ya
uwekezaji wa ndani ilianzia hapo hapo kukawa na miradi iliyofumuka kila siku na
kukabidhiwa kwa watu ambao siku chache zilizotangulia walikuwa ni mafukara wa
kutupwa.
Lakini baada ya “Mzee Ruksa” kusema watu kufungua “vijimiradi
vya kuku wa mayai”siyo mbaya wao wakaanza kukabidhi biashara zao kwa ndugu zao
na hapo yakaanza kununuliwa mabasi ya kisasa na kulihujumu shirika la reli ili
lisiharibu biashara za mabasi yao.
Hali ikaendelea hivyo mpaka baadaye mawaziri wakaanza
kumiliki mashirika ya ndege wengine wakipitia migongoni mwa watu binafsi na
wengine wakiyamiliki mashirika ya ndege moja kwa moja na hapo ndipo Air
Tanzania ikaingiwa na virusi vilivyoanza kufifisha afya yake.
Cha ajabu ni kwamba hao wana CCM mamilionea eti nao bado
wanadai wanafuata nyayo za “Baba wa Taifa” na kuwaambia Watanzania wakiacha
kuipigia CCM maana yake ni kwamba wanamsaliti Mwalimu Nyerere na waasisi
wenzake wa TANU akina Marehemu Rashid Kawawa na baadaye Mzee Abeid Amani Karume
katika muungano wake na ASP na kuunda CCM (chini ya Mzee Aboud Jumbe).
Kwa hiyo kwa falsafa hiyo mtu yeyote akihama kutoka CCM na
kujiunga na chama chochote cha upinzani basi huyo ni msaliti wa waasisi wa
taifa hili. Na kinyume chake mtu yeyote
akifanya ufisadi na bado akabakia ndani ya CCM basi huyo anamuenzi Mwalimu na
waasisi wenzake.
Hapo ndipo pananitatiza juu ya kumuenzi Mwl. Nyerere.
Nakumbuka Mwl katika kujiandaa kustaafu alimuweka katika nafasi ya uwaziri mkuu
mtu mahiri kabisa Marehemu Edward Moringe Sokoine ili apambane na ufisadi
lakini mtu huyo akafa kifo chenye maswali mengi kuliko majibu mwaka 1984 ikiwa
ni mwaka mmoja tu kabla ya kustaafu kwa Mwalimu Nyerere.
Kuhusu hatua alizochukua Sokoine kupambana na ufisadi watu wengi
wenye rika kama langu la miaka 50 na zaidi wanayo kumbukumbu nzuri.
Mimi mwenyewe nikiwa mwanafunzi Seminari ndogo ya Nyegezi
nilikuwa mmoja wa watu waliokwenda kuokota biskuti na madebe ya sukari
yaliyotupwa na wafanyabiashara wengi wakiwa ni wenye asili ya kiasia waliotupa
vitu vyao maeneo ya Nyegezi fisheries wakiogopa kukamatwa katika ile saka saka
hatari ya wahujumu uchumi.
Mimi mwenyewe pia niliingia kwa kujipenyeza katika mkutano
pale Liberty Cinema Mwanza mwaka 1984 wakati wananchi wa Mwanza walipokuwa “wakimcha
chana live” mkuu wa mkoa Marehemu Abdulnoor Suleiman na Mkurugenzi wa Mkoa Bw. Issaya Kasera
Gungu.
wakitaka wavuliwe madaraka kwa sababu wanaendesha biashara ya
magendo ndani ya Ziwa Victoria. Baada ya kurejea Dar Mwalimu hakusubiri cha
Tume ya Bunge wala cha TAKUKURU iwavyo kwa jina lolote lile, bali aliwafutilia
mbali watu hao.
Je tunakumbuka ya mwaka 1982 chini ya uongozi wa Mwl Nyerere yalivyowakumba
waziri Augustine Mwingira na Meneja Mkuu wa ATC Bw. Lawrence Mmasi chini ya
kashfa na hao walitimuliwa mara moja (kwa sasa wote hao ni marehemu).
Watendaji
hao walikodi ndege mbili chakavu zilizokuwa zikifanya safari kati ya Ulaya na
India zikimilikiwa na raia wa Lebanon Bw. George Hallack leo tunaambiwa CAG,
TAKUKURU, Kamati ya Bunge, Mahakama n.k. na wakati mwingine taasisi zote hizo
zinakosa ushahidi wa kuwatia hatiani mafisadi hao.
Kwa hiyo kwa muktadha wa mjadala huu aliyedandia farasi wa
huruma ni CCM na tena amefanya hivyo kwa miaka mingi. Vikundi vya walafi
wanaofikiria kujitajirisha leo wanasema eti wanamuenzi Mwalimu Nyerere je
wanafanya hivyo kivipi? kwa kupora mashamba na ardhi ya wanyonge?
Je ni kwa kuendesha biashara kubwa ya mahoteli? kwa kumiliki
malori na vituo vya mafuta? kwa mikataba mibovu katika madini? huko ndiko kumuenzi Mwalimu? je yeye
aliacha malori mangapi? aliacha mahoteli mangapi? baada ya kuwa amekaa
madarakani kwa zaidi ya miaka 20? nadhani nimeeleweka vyema.
UKAWA ni mojawapo ya jitihada kutoka kwa wale wasioridhishwa
na hali ya kisiasa nchini, jitihada hizo zimekuwa nyingi na pia katika majina
tofauti tofauti kuanzia lile kundi la wabunge 55 yaani G-55 lililokuwa likiongozwa
na Mzee Njelu Kasaka, Philp Marmo, Jeneral Ulimwengu na wenzao.
Baadaye alikuja mama ambaye sauti yake imezimika ghafla
hatujui kulikoni? (Anne Kilango) Lumambo Seleli, James Lembeli n.k. labda
tofauti ya hii UKAWA ya sasa imetokana na vyama vya upinzani.
Kwa hiyo UKAWA ni zaidi ya katiba mpya, bali ni njozi ya
matumaini iliyorejea baada ya wapinzani kuanza kupata busara baada ya kuwa
wakisutana wao kwa wao miaka nenda rudi.
Miaka iliyotangulia ilionekana Tanganyika ikirejea kutakuwa
na muamko wa kisiasa lakini leo hoja ya kukataa serikali tatu kwa CCM ni hofu
ya kushindwa, kwani Muungano kwa jinsi ulivyo sasa unawapatia wao manufaa ya
kuendelea kubakia madarakani.
Elias Mhegera-Tel:
0754-826272

wamemshambulia vikali kwamba ni msaliti kisha wakampatia tuzo ya uzalendo, wapi na wapi?
JibuFuta