Ijumaa, 18 Julai 2014

VYOMBO VYA HABARI VIONGOZE MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA


Jaji Mstaafu Thomas Mihayo 


Makala hii ilitumika katika gazeti la Mtanzania Jumapili Oktoba 13, 2007

Na Elias Mhegera

Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa hamasa dhidi ya rushwa katika jamii. katika gazeti la Rai, toleo la Oktoba, 21-27, 2004  kulikuwa na makala mbili moja ya Jenerali Ulimwengu “Wanahitajika wapiga filimbi”, na ile ya Maggid Mjengwa “Ka kitandugaho na shamba la nguruwe!” zinatosheleza kueleza ninachotaka kukiongelea katika makala haya.         

Makala zile zinazungumzia athari za ufisadi, mwenendo wa viongozi wetu na umuhimu wa jamii kubadilika na kuichukia rushwa. Ukweli ni kwamba kama hatutajisahihisha na 
kubadilika tutajenga jamii ya wanyama-watu.                                                                                                

Jamii ambayo watu watajichukulia sheria mkononi kwa kadri wanavyopenda, kwa sababu wenye mamalaka wameshindwa kuwajibika, tutakuwa na jamii ambayo watu wanavaa kama binadamu anavyotakiwa kuvaa na wanatembea kwa miguu miwili lakini wanatenda mambo mengine sawa na wanyama (man-eat-man society).

Labda kwa sasa bado ni mapema kwa wasomaji wa makala hii kuamini kwamba ipo siku watanzania wanaweza kufikia huko, lakini ukweli ni kwamba hata wale waliofikia kiwango hicho walianza kumon’gonyoka kimaadili taratibu kama tunavyofanya sisi kwa sasa.   Lakini kwa kufanya hivyo tunaweza kutoa mwanya kwa walinzi wa maadili kujitokeza na tukajikuta wote tunaadhibiwa waliomo na wasiokuwemo.

Wakati wa kuanzisha mapambano yake dhidi ya ufisadi nchini Cuba rais wa sasa wa nchi hiyo Fidel Castro ambaye kwa sasa amekaimisha madaraka kwa mdogo wake Raul Castro kutokana na kuugua alisikitishwa na jinsi ambavyo wananchi wengi walishindwa kumuunga mkono wakati kulikuwa na kila dalili kwamba walikuwa wananyonywa na serikali ya fisadi Fulgencio Batista.

Hata hivyo alipofikishwa mahakamani baada ya jaribio lake la kwanza kushindwa alimtamkia jaji kwamba kwa sababu rais wa nchi yake alikuwa ameamua kuwa mwizi na fisadi watu wenye heshima zao nafasi yao ilikuwa ni gerezani au kaburini!

Ninapozungumzia walinzi wa maadili ni kwa sababu nina imani kwamba katika kila kizazi wapo waharibifu wa maadili na pia wapo walinzi wake isipokuwa jambo lisiloeleweka ni kwamba hao walinzi wa maadili watatumia mbinu gani. Ulinzi wa maadili (value clarification) hutokana na ujasiri wa kuchoshwa na mifumo isiyopenda haki.

Bado nina imani kwamba watanzania tuna vyombo kama mahakama ambavyo vinaweza kusimamia maadili yetu na mfano halisi ni jinsi ambavyo jopo la majaji watatu Jaji Natalia Kimaro, Jaji Salum Massati, na Jaji Thomas Mihayo walitoa hukumu ya haki dhidi ya takrima mwezi Aprili 2006.

Katika shauri lililokuwa mbele yao ambalo liliwasilishwa na asasi za wanasheria ambazo pia zinajihusisha na masuala ya haki za binadamu, yaani Legal and Human Rights Centre (LHRC), Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT), na National Organization for Legal Assistance (NOLA), jopo la mjaji hao lilizingatia mambo mengi  katika misingi ya kisheria na ile ya kijamii katika kufikia hukumu hiyo.

Miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu ambao ulikuwa umehalalishwa kupitia sheria ile ya takrima.  Kwa maneno mengine ni kwamba kitendo cha kuruhusu matumizi ya takrima katika chaguzi kilikuwa kinawapatia nafasi wenye uwezo wa kipesa mazingira mazuri ya kushinda dhidi ya wale wasiokuwa nacho.

Jambo hilo kwa mujibu wa majaji hao ni sawa na ugandamizaji, na ukiukwaji wa haki za binadamu. Pia jopo hilo lilizingatia athari za muda mrefu kama hali hiyo ingeruhusiwa iendelee Kwani ingesababisha matabaka katika jamii, na mwisho wa yote tungejikuta tunachagua viongozi kutokana na vigezo vya uwezo kipesa yaani uwezo wa kuhonga nyakati za uchaguzi badala ya kuangalia na kuzingatia vigezo vingine sahihi kama vile uadilifu na uwezo wa mtu kiutendaji na uwezo wa kuongoza pia.

Lakini pia jopo hilo lilizingatia mikanganyiko ambayo ingejitokeza kutokana na ukweli kwamba Tanzania imeridhia mikataba kadhaa ya kimataifa na tamko la Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu la mwaka 1948. Kwa hiyo takrima ilikuwa inakwenda kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa uhuru na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mtu yeyote bila ubaguzi.

Hivyo basi kwa kuzingatia yote hayo jopo hilo likaona kwamba  takrima ilikuwa na madhara katika jamii, ilikuwa ni sheria gandamizi kwa wasionacho na pia ilikuwa inakwenda kunyume na dhamira yetu njema ya kujenga taifa linaloheshimika, lenye uwazi, utawala bora, na linalozingatia misingi ya demokrasia.

Kwa kuzingati vipengele hivyo ndipo jopo hilo la majaji likaamua kutoa haki kwa walalamikaji kwa kuzingatia ukweli kwamba ombi lao mahakamani lilipelekwa kwa nia njema (bonafide), na kuzingatia maslahi ya jamii kwa ujumla. Ni katika mazingira hayo nimeshawishika kusema kwamba tunayo bahati kwamba mkondo wa sheria unaweza kutuunga mkono katika vita dhidi ya ufisadi.

Kwa hiyo kama dhamira ipo inabidi tujiulize maswali kwamba tuanzie wapi?. Ni lazima tukubaliane kwamba kabla ya kuanza vita vyenyewe kwanza tujifanyie tathmini sisi wenyewe kwa jinsi ambavyo tumechangia kuwepo kwa hali hii ambayo kwa sasa tunaiona kwamba inatukera.

Labda baada ya tathmini hiyo kila mmoja wetu anaweza kujikuta anahusika kwa njia moja au nyingine kwa mfano kumekuwepo na tabia ya kuwanyooshea vidole wanasiasa peke yao lakini tunasahau kwamba hao tuliwachagua sisi wenyewe na wala hawapo madarakani kwa kupindua nchi. Kwa hiyo kama tuliwachagua sisi wenyewe baada ya kupokea hongo zao basi dhamira zetu zitusute sisi wenyewe.

Hivyo basi hatuna budi kijisafisha sisi wenyewe kwanza kimaadili ndipo tuanze kupigania mfumo wa haki, bila kufanya hivyo hao tunaowasuta watakuwa na utetezi wa kutosha na kwa maana hiyo yeyote anayepingana na ufisadi ataonekana ni mnafiki tu.

Kumbe basi sasa ndiyo muda muafaka wa kubadilika na kuachana na ile dhana kwamba rushwa ni mfumo wa kawaida katika nchi za dunia ya tatu. Tupiganie uadilifu katika nyanja zote yaani siasa, biashara, taaluma na tuhakikishe kwamba mikataba yote tunayoingia ni kwa manufaa ya watu wote badala ya kuwanufaisha wajanja wachache.

Nimezungumzia mikataba kwa sababu hilo ni eneo mojawapo linalopigiwa kelele nchini mwetu, kwa mfano mikataba ya uchimbaji wa madini, ujenzi wa miundombinu, majengo ya mashirika ya umma na yale ya serikali kuu n.k. imedhihirika kwamba kumekuwepo na tabia ya kuchukua “kitu kidogo” na kusaini mikataba hiyo ambayo mara kadhaa imekuwa ikilitia hasara kubwa taifa letu.

Ili kubadilika katika hilo inabidi viongozi wetu na wote wenye dhamana kubwa wabadili dhamira zao ili kila anayepata nafasi ya kutuwakilisha katika kusaini mikataba afanye hivyo kwa nia njema.

Tutakuwa na imani kwamba mkataba wowote umesainiwa kwa dhaamira njema iwapo kutakuwepo na uwazi tokea mwanzo wa mawasiliano juu ya mkataba hadi kusainiwa kwa mkataba wenyewe. Pamoja na uwazi huo ni lazima mikataba hiyo iangalie mazingira ya kisiasa, kisheria, kiuchumi na faida katika jamii kwa ujumla (viability). Kwani hakuna manufaa ya kuwa na mikataba ambayo haiwanufaishi watanzania badala yake wawekezaji ndiyo wanakuwa wanufaikaji wakuu.

Pamoja na kuzingatiwa kwa mambo hayo muhimu lakini pia kuna umuhimu wa kuangalia uwezo wetu kisayansi na kiteknolojia la sivyo ndipo tunapewa visingizio mbalimbali kwamba Tanzania haina teknolojia fulani na hivyo inabidi madini yetu yasafirishwe katika mfumo wa mchanga? Kwa mtindo huo tutajikuta tunashindwa kuelewa hivi kinachosafirishwa ni mchanga wenye madini au ni madini halisi na ni ipi thamani yake halisi?

Njia nyingine muhimu ni ushirikishwaji wa wananchi, Kumekuwepo na malalamiko kwamba katika baadhi ya mikataba hata mamlaka husika zimekuwa hazihusishwi kwa mfano kamati husika za wabunge. Kwa maana hiyo inakuwa rahisi kwa wananchi kuwa na wasiwasi juu ya mwenendo wa wahusika katika kushughulikia mikataba hiyo kama kweli maslahi ya taifa yamewekwa mbele au kuna ajenda nyinginezo tofauti.

Kuongezeka kwa tuhuma za ufisadi nchini mwetu kunatoa taswira kwamba mambo yanayojitokeza sasa hayakuanza hivi karibuni bali ni hitimisho tu (culmination) la mambo ya aina hiyo kwa muda mrefu.Inatubidi sasa tubadilike badala ya kuthamini vitu tuanze kuthamini utu na watu na mambo kama haya hayatajitokeza tena.

Kile kinachoonekana kama ufisadi wa wanasiasa ni kielelezo tu cha mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima katika ujumla.wake isipokuwa wanasiasa wanaonekana kiurahisi zaidi kutokana na nafasi zao Kwani wao ni taswira ya jamii. Kesi za ufisadi zipo nyingi katika taasisi mbalimbali kwa mfano katika shule ambako walimu wanatuhumiwa kujihusisha katika vitendo vya ngono na wanafunzi wao, wakwe kuvunja ndoa za watoto wao watu kugombea zawadi za send-off na mirathi ni taswira tu ya tatizo kubwa la ufisadi na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Yote hiyo inaashiria kwamba jamii yetu imepoteza muelekeo wa kimaadili na ipo haja ya kurekebishana ili turudi katika mstari. Wapo wanaodai miongomi mwa sababau za kupoteza maadili yetu ni kutupa mila zetu na kukumbatia zile za kigeni (consumerist culture) ambazo tunaziona kupitia katika vyombo vya habari kama televisheni na katika mitandao ya intaneti  Kwa hiyo tumeiga mfumo wamaisha bandia ambao hauendani na jamii na mazingira yetu na athari zake ndizo hizo tunazoziona.

Kwa mtindo huo tutajikuta siku moja tumefikia mahali pa kuwaingiza binti zetu katika biashara ya ukahaba ili mradi sisi tumepata chetu kwa sababu tayari tumejiwekea mazingira ya kuthamini vitu bila kujali vimepatikana kwa njia zipi. Kwa msingi hiyo hata rushwa ya ngono inaweza kuhalalishwa kwa sababu vipaumbele vyetu vimebadilika kwa kisingizio kwamba tunakwenda na wakati au kwamba hiyo ndiyo “hali halisi”.

Katika vita dhidi ya ufisadi ni lazima tufahamu kwamba tunapambana na dhahama iliyojikita katika jamii yetu kwa muda mrefu. Kwa mfano tuwe na mitaala maalumu itakayowaelimisha vijana wetu athari za ufisadi. Ni kweli kwamba jambo hilo linafanyika mpaka sasa lakini bado halijapewa uzito unaostahili.

Njia nyingingine ya kuondokana na ufisadi ni kijufunza kutoka kwa watangulizi wetu. Kwa mfano mwanzilishi wa taifa letu Hayati Mwalimu Nyerere alikemea rushwa wakati akiwa madarakani na aliendelea kufanya hivyo hata pale alipostaafu.Wapo watendaji wengine pia waliofuata nyao zake kwa mfano Marehemu Jaji Francis Nyalali, Profesa Geoffrey Mmari  hawa ni baadhi ya viongozi ambao tunaweza kujifunza kutoka kwao kwa yale waliyoyasimamia katika jamii.Hiyo ndiyo njia ya kuendeleza maadili ya jamii (societal values)

Je ipo nafasi ya ushindi dhidi ya ufisadi? Ndiyo nafasi hiyo ipo iwapo tutajipanga upya, kwa mfano tupunguze urasimu na vikwazo mbalimbali katika taasisi zetu. Urasimu hushawishi watu wanaohitaji huduma watoe hongo ili waweze kupata huduma mara moja ili waweze kuendelea na mambo yao mengine.Njia nyingine inayoweza kusaidia katika kuondoa ufisadi ni kufanya mambo kwa uwazi zaidi na kutoa elimu kwa umma juu ya atahari za ufisadi.

Njia nyingine ni kutoa adhabu stahiki kwa wale wote watakaopatikana na hatia au ushahidi wa kutosha kwamba wamehusika na ufujaji wa mali ya umma adhabu hizo ni pamoja na kulipa fidia vifungo gerezani na mambo kama hayo.Ipo mifano mingi ya watu ambao wamefilisi mashirika ya umma lakini mpaka sasa bado wanakumbatiwa katika mifumo yetu ya utawala watu kama hao ni dhahiri wataendeleza ufisadi wao kila waendako.

Mwandishi Sahr Kpundeh katika chapisho lake Political Will in Fighting Corruption (1996) anasema katika kufanikisha vita dhidi ya ufisadi lazima kuwepo na utashi wa kisiasa nami namuunga mkono katika hilo kwani viongozi wetu ndiyo wanatakiwa kuonyesha ushawishi wa dhamira hiyo kwa umma.  Kwa hiyo wadau wote yaani asasi za kiraia, mamlaka husika kama vile TAKUKURU, waandishi wa habari na wafadhili wote tunatakiwa kushirikiana katika kudhibiti matumizi ya raslimali za umma.

Mwandishi huyo anaendelea kwa kusema viongozi lazima wawajibike katika kusimamia utawala bora, ukusanyaji wa kodi, udhibiti wa hongo katika huduma za umma, na uwezeshaji wa wananchi kupata taarifa muhimu zinazowahusu. Upo umuhimu wa watu kufahamishwa misingi ya utawala bora.

Kwa upande wa vyombo vya habari yapo mengi yameandikwa jinsi vinavyoweza kusaidia katika kukemea maovu mbalimbali katika jamii. Hapa nitapenda kunukuu japo kwa ufupi matazamo wa mwandishi Rick Stapenhurst katika chapiso lake The Medias’ Role in Curbing Corruption (2000).

Anasema uandishi wa habari za uchunguzi ni silaha muhimu dhidi ya ufisadi iwapo tu  uandishi huo utaungwa mkono na asasi nyingine. Kwa mfano lazima kuwepo na mazingira yanayoruhusu uhuru wa kujieleza, kuwepo na taasisi za kutoa elimu itakayowafundisha waandishi hao mbinu, maadili na utaalamu wa fani hiyo nyeti.

Mwandishi huyo anasema mambo mengine muhimu ni kuwepo na uhuru wa waandishi kutoa mchango wa mawazo yao bila kuingiliwa na dola au na wamiliki wa vyombo vya habari hata kama vinaandika habari za watu wanaowahusu wao wenyewe. Mwandishi huyo anasema iwapo kutakuwa na migongano ya kimaslahi kati ya maslahi ya wamiliki na utaalamu (professionalism) wa fani ya uandishi basi itafikia mahali vyombo vya habari vitashindwa kutimiza majukumu na wajibu wao katika jamii.

Kama hiyo haitoshi lakini pia lazima kuwepo na ulinzi wa kutosha kwa waandishi wa habari na watoa taarifa (whistleblowers).  Bila kuwepo kwa mazingira salama kwa waandishi basi watakumbana na vitisho au hata kudhuriwa na wale ambao habari zao zinafuatiliwa na waandishi hao. Katika baadhi ya nchi hapa Afrika imefikia mahali ambapo waandishi wamepoteza hata maisha yao kutokana na kukemea ufisadi.

Ni dhahiri vita dhidi ya ufisadi kama nilivyoeleza huko nyuma vinahitaji ushirikiano wa karibu sana na wadau wengine kwa mfano taasisis husika kama vile TAKUKURU, jeshi la polisi, mahakama, taasisi za elimu ya juu viongozi wa dini kwa hiyo vyombo vya habari ni chachu tu katika vita dhidi ya ufisadi lakini wadau ni wengi.Kwa hiyo vyombo vya habari hapa nchini tayari vimeonyesha njia sasa limebakia jukumu la viongozi wa nchi kuviunga mkono

Lakini kuandikwa tu magazetini kwa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadu hakutakuwa na maana kama lengo ni kuchafuliana majina au ni jambo linalotokana na mifarakano ndani ya kada ya viongozi, bali lazima kuwepo na ushahidi wa kutosha ili wahusika wasiishie kuandikwa magazetini tu bali wafikishwe katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua zinazostahili.. Kama kweli tuhuma zinazotolewa magazetini zitakuwa na ukweli basi hatua inayotegemewa ni wahusika kujiuzulu kutoka katika nyadhifa zao.

Kujiuzulu ni jambo la muhimu ili kutatoa nafasi nzuri zaidi ya tuhuma zinazowahusu kuchunguzwa lakini pia kutawapa nafasia watu wasafi wanaostahili kuendelea katika majukumu muhimu ya umma. Vinginevyo kama serikali itashindwa kuwachukulia hatua madhubuti wahusika wote basi itakuwa imejijengea mazingira magumu kwa wapiga kura kwani mpaka sasa watu wanasubiri kwa hamu taarifa sahihi zinazoweza kuwasafisha wote waliotuhumiwa kwamba wanajihusisha na vitendo vya ufisadi hapa nchini.

Kama nilivyoeleza hapo awali vita dhidi ya ufisadi vinahihitaji umakini mkubwa na utayari wa wahusika kubadilika kitabia. Lakini yapo mazingira ambayo pia yanachangia katika hali hiyo ya ufisadi, kwa hiyo ni muhimu pia kufikiria ni vipi mazingira hayo yanaweza kuboreshwa ili kuondoa ushawishi mbaya kwa watumishi wa umma na wahusika wengine ili waondokane na ufisadi.

Mazingira ninayoongelea hapa ni kama vile mishahara midogo na mazingira magumu ya kazi kwa mfano mtu aliyeajiriwa kama hakimu lakini asipewe usafiri wa uhakika kwa ajili ya kwenda kazini na kurudi nyumbani baada ya kazi, asipewe nyumba ya kuishi inayotosheleza mahitaji yake na familia yake anaweza kushawishika kuomba hongo ili kukidhi mahitaji yake hayo ambayo kimsingi ni mahitaji muhimu kwa binadamu yeyote yule.

Lakini kwa upande mwingine tuangalie kwa mtumishi wa umma kama vile mwalimu anayo nafasi gani kujipatia hongo? Ni dhari kwamba mazingira yake ya kazi ni magumu katika hali zote lakini vile vile hana hata huo upenyo wa kupata hiyo hongo.

Kwa maana nyingine mwalimu anapopata ukuu wa shule hapo ndipo na yeye ataanza rasimi kujijengea maisha yake ya baadaye na hapo ndipo utakuta mkuu huyo wa shule anajenga urafiki na mhakiki mali (stock verifier) na mkaguzi wa mahesabu (auditor) ili wamlinde katika taarifa zake hao nao watapata chao na kunyamaza kimya au kutoa ripoti nzuri.

Kwa maana hiyo ni kwamba mwalimu anaweza kujipatia kipato cha ziada kwa kufundisha vipindi vya ziada katika shule nyingine (part time) au kwa kutoa tuisheni lakini yote hayo tunajua fika ugumu wake na vikwazo vyake. Kwa mfano, miaka kadhaa nyuma serikali ilitoa agizo likiwazuia walimu wasifundishe tuisheni katika madarasa ya shule zao, lakini pia hilo la tuisheni linaweza kumfanya mwalimu afundishe darasani kwa kulipua na kutoa uzito kwenye darasa lake la tuisheni.

Kwa maana hiyo ukiwalinganisha watumishi hawa wawili tofauti wa umma utaona kwamba hakimu anayo nafasi ya kujihusisha na ufisadi kwa urahisi zaidi kuliko mwalimu.Kwa mfano hakimu anao uwezo wa kuamua apate chochote katika kutoa uamuzi katika kila shauri lililopo mbele yake na kwa maana hiyo haki itatolewa kwa aliyetoa “chochote” na kumnyima asiye nacho hata kama ndiye aliyestahili haki hiyo.

Ndiyo maana nimesema ufisadi ni dhana pana ambayo inatugusa wengi katika maisha yetu ya kila siku na wala tusiwanyooshee vidole wanasiasa tu bali tauangalie pia sisi wenyewe tumewahi kuhusika vipi au tunaendelea kujihusisha vipi na ufisadi.

Kwa hiyo mwandishi wa habari naye anaweza kuwa anahusika au anajihusisha katika ufisadi japo waandishi wa habari kwa sasa ndiyo wamekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi. Tusisahau kwamba ripoti ya Jaji Warioba ya mwaka 1996 inawataja waandishi wa habari pia kwamba hupokea hongo ili waandike habari katika mtindo ambao mtoa hongo anataka kwa mfano kumpamba au hata kumuandika vibaya adui au mpinzani wake.

Hoja ya msingi katika hili ni kwamba waandishi wa habari nao wazingatie maadili ya kazi yao kwanza ndipo zoezi zima la kupinga ufisadi litafanikiwa. Silaha nyingine kwa waandishi wa habari ni ujasiri katika kazi yao, kwa mfano sisi waandishi tusikubali kutishiwa maisha na kuacha kufuatilia uovu au uvundo ambao tayari tumefanikiwa kupata habari zake japo hata kama ni chembe ndogo kwani huo ndiyo mwanzo wa habari kubwa.

Visingizio vingine vinavyoweza kukwamisha kazi yetu ni ile hoja kwamba tunaingilia maisha ya mtu binafsi (privacy), au kwamba tunavujisha siri za serikali hakuna usiri wowote katika jambo ambalo linakwenda kinyume na maslahi ya umma. Uovu ni uovu tu bila kujali umetendwa na nani yapo madai mengine pia ya kipuuzi kwamba waandishi wa habari wanakosa uzalendo, ni uzalendo gani huo unaotakiwa wa kuficha maovu? wa kuwalinda mafisadi? Katika hayo hakuna uzalendo bali uzi uwe ni ule ule wa kukemea bila woga.

Kama tutafikia mahali ambapo serikali itawajibika kikamilifu na kuziba mianya yote ya rushwa basi haitatokea kamwe mtu adharau kazi ya mwingine kwa sababu kazi zote na hasa katika sekta ya umma zitakuwa na mapato yanayolingana tofauti na hali ilivyo kwa sasa ambapo baadhi ya sekta ambazo hazina hongo haziheshimiwi na wanajamii wengine kwa mfano kazi ya ualimu si kazi inayoheshimiwa lakini sote tunajua umuhimu wa elimu na kwa maana hiyo elimu haipo bila kuwepo na hao waalimu ambao tunawabeza

Kwa sasa inafikia mahali ambapo mtu anaweza kujiona ni mwenye bahati mbaya pale anapoomba kozi fulani kama vile uhasibu au sheria na akaambiwa kwamba pasi zake hazitoshelezi yeye kupata taaluma hiyo hivyo mtu huyo hulazimika kusomea kozi nyingine tena wakati mtu mwingine atakuambia nimechagua kozi ile kwa ajili ya kupata elimu tu lakini kamwe siwezi kanya kazi ile.

Dhana hiyo inatokana na ukweli kwamba tayari wanajamii wanajua ni kazi ipi inayolipa na ipi isiyolipa na kwa maana hiyo hayupo anayependa kuishi katika dhiki na njaa wakati upo uwezekano wa kuishi maisha ya raha kama wanajami wengine.

Kama tutaendekeza mtindo huu wa kuchagua kazi kwa sababu tunaweza kupata hongo au mapato haramu ya ziada tutajikuta tunakosa wataalamu muhimu katika jamii, kwa mfano madaktari, manesi au hata viongozi wa kiroho kama vile mapadri, wachungaji, masheikh maaskofu na wengine wa namna hiyo. Jambo la msingi kwetu ni kubadilika kimsimamo na kuziona kazi zote kwamba zina uzito unaostahili na vile vile tuone kwamba ufisadi ni dhambi ni jambo baya ambalo ni lazima tuondokane nalo sasa bila kusubiri, tukifanya hivyo tutakuwa tumejiwekea kinga ya kudumu ya kuwafanya watu fulani kujinyakulia madaraka kwa mabavu kwa kisingizio cha kulinda maadili.

Na tuanze na chaguzi zilizopo mbele yetu sasa kila atakayetoa hongo akemewe asutwe na hongo zake arudishiwe ili akale yeye na mkewe au na mumewe. Tukishinda katika hilo nina imani tutakuwa tumeshinda mtihani mkubwa kwa sababu kama tulivyoona hapo awali sisi wenyewe ndiyo waendelezaji wa ufisadi pale tunapokubali kupokea hongo za wanaogombea uongozi halafu baadaye tunajigeuza kuwa wakemeaji je huo sio unafiki? na tuanze sasa bado hatujachelewa


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 826 272 na kwa barua pepe: mhegeraelias@yahoo,.com







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni