Jumapili, 6 Julai 2014

WAKULIMA WANAPODHULUMIWA ARDHI YAO JE WAKALIME WAPI?



Mkulima wa kijiji cha Makaani Gama, Kata ya Magomeni, Wilaya ya Bagamoyo akililia ardhi yake ambayo imeporwa kwa njia za kifisadi na kukabidhiwa kwa "investor?" 

Na Elias Mhegera/Januari 20/2014  
Iwapo kuna jambo linaweza kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Tanzania kwa hali inayojionyesha sasa basi vita hiyo itasababishwa na migogoro ya ardhi kama ilivyodhihirika Bagamoyo hivi karibuni.
Mgogoro wa kugombea ardhi Bagamoyo katika kijiji cha Makaani Gama ni wa muda mrefu na wenye mtiririko wa mambo mengi ya ajabu. Siku ya Jumapili tarehe 19, Januari (juzi) Kamishina wa ardhi Bw Gapser Luanda alilazimika kuambatana na timu ya watendaji wake kwenda kijijini hapo ili kusikiliza malalamiko ya wakulima.
Mgogoro huo ambao mpaka sasa umefunguliwa kesi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Kesi Na: 162/2012 umekuwa ukichukua sura tofauti tofauti kulingana na maslahi yanayokinzana ndani yake.
Awali serikali ilitoa ardhi ya Ranchi ya Zanzibar iliyotolewa na Mwalimu Julius Nyerere kwa serikali ya Zanzibar chini ya utawala wa Mzee Abdu Jumbe mwaka 1984. Hata hivyo baada kugawiwa ardhi mwekezaji amejitanua katika vijiji vya jirani kama vile Makaani Gama, Fukayosi na Matipwiri na hivyo kusababisha migogoro ya kugombea ardhi.
Moto uliowashwa hivi karibuni umetokana na jaribio la mwekezaji kupitia kampuni ya Eco-Energy kujaribu kuandaa taratibu za kuwalipa fidia wakazi wa maeneo hayo ili wapishe na kuachia eneo hilo kabla hata kesi ya msingi iliyopo mahakamani ikiwa haijakamilika.
Uchunguzi wa mfafanuzi.blogspot.com umebaini kwamba kulikuwa na mbinu ya mwekezaji au ya kigogo anayetuhumiwa kujificha nyuma ya mwekezaji kutaka kuwagawa wamiliki wa mashamba hayo yanayogombewa.
Mchezo uliotumika ulikuwa na wa kuwaahidi nyumba wanavijiji waliomo katika mashamba kwa sasa ambapo inadaiwa mtoto wa kigogo aliwaahidi wanavijiji kwamba watajengewa nyumba za kisasa na kisha kukabidhiwa funguo za nyumba zilizokamilika.
Mbinu hiyo ilionekena kuleta mafanikio kwa kiwango chake kwa upande wa “mwekezaji” kwani baadhi ya wanavijiji walikuwa tayari kupisha katika eneo hilo kwa ahadi ya kujengewa nyumba hizo.
Hata hivyo mpango huo ulikutana na pingamizi kubwa kutoka kwa wamiliki wa mashamba ambao wanaishi jijini Dar es Salaam na baadhi ya wale wa kijiji Makaani Gama.  Kwa upande wao wanadai wapo tayari kushirikiana na mwekezaji wa Eco-Energy katika kilimo cha miwa kwa ajili ya sukari lakini bila kuachilia ardhi yao. 
Kwa upande mwingine jitihada za serikali kupitia kwa watendaji kadhaa wa wizara ya ardhi Wilayani Bagamoyo na hata makao makuu ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi akiwamo Waziri Prof. Anna Tibaijuka na  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi zimekuwa ni kuwashinikiza wanavijiji na wamiliki  wa mashamba kuondoka na kumpisha “mwekezaji” ili aendelee na kazi yake.
Katika mkutano wa Jumapili ilidhihirika kwamba mpango wa tahmini ya thamani halisi ya ardhi husika tayari kwa kuwalipa fidia walengwa ili waupishe mradi huo wa miwa haukabaliki na walio wengi.
Hata alipopewa nafasi ya kusoma kilichoandikwa katika Fomu Na: 69 Mthamini Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi Evelyn Mugasha, alisononeshwa pale aliposikia sauti ya wengi ikiitikia kwa kishindo kwa kusema “hatutaki fidia, hatutaki fomu zenu!”
Fomu hiyo ambayo humtambua mmiliki halali tayari kwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya thamani ya ardhi husika na kisha kuwalipa fidia walengwa imeonekana sawa kabisa na sumu kwa wamiliki hao wa mashamba.
Awali kabla ya kufikiwa kwa hatua hiyo kulikuwapo na hamasa kubwa kutoka kwa viongozi wa wamiliki hao. Mwenyekiti wao Bw Ally Mbawe alisikika akiwahamasisha wenzake na kusema “mnataka nishambuliwe na kudhuriwa kama ilivyokuwa kwa Dkt Stephen Ulimboka na Mhariri Absalom Kibanda? Kwa nini wengine mnabaki nyuma katika harakati zetu? Alilalama.
Alidai kwamba kamwe haitawezekana wao waiachie ardhi yao ambayo wameitumikia kwa muda mrefu huku wakiwa wamewekeza pesa nyingi kwa ajili ya kuendeleza mashamba yao. “Hatuchoki mpaka…alianzisha ghani hiyo na kuitikiwa na umati wa watu wasiopungua 800 tena kwa kishindo… “kieleweke!”.
Baada ya hapo mwenyekiti huyo alimuachia kipaza sauti katibu wake Bw Bessa William ambaye alisema bila kutafuna neno kwamba haya ni mapambano kati ya wanyonge na mafisadi, “usitegemee kuletewa haki yako nyumbani kwako ni lazima iufuate ilipo” alimaka mkulima huyo kijana.
Jitihada za Afisa Ardhi Maliasili na Mazingira Bw. Clement Mkusa kuwatuliza hasira wananchi hao hazikuzaa matunda ingawaje alidhihirisha kwamba anaufahamu vizuri mgogoro huo na ana uwezo mkubwa wa ushawishi kwa wananchi hao.
“Jamani mimi nimekuwa nanyi siku zote  nikitaka mpate haki yenu iweje leo mnayakataa maelekezo ya viongozi wangu kutoka wizarani? Hamuoni kwamba mnapingana na sheria za nchi? Naomba tafadharini sana mteue watu kumi ili wawakilishe kundi lenu na tuanze mazungumzo na serikali yenu je mnaonaje wazo hilo?” aliuliza.
Baada ya mashuriano ya kina wamiliki wa mashamba walisema watateua wawakilishi 10 kutoka katika makundi yote yaliyoguswa na mgogoro huo. Wawakilishi hao watatoka katika makundi ya wakulima wakazi wa makaani, makundi ya asasi za haki za binadamu na Shirika la HakiArdhi ambalo limekuwa likipigania haki za wanyonge katika migogoro yote ya ardhi.
Katibu Bessa alitamba kwamba wao ni kundi lililojotosheleza na kwamba miongoni mwa watu wanaopigania ardhi hiyo wakiwakilisha wanyonge wamo mawakili, madaktari, wahadhiri wa vyuo na wasomi wengine. “tuna hazina kubwa ya watu wenye uelewa hatutaichia ardhi yetu hivi hivi, tutapambana,” alitamba.
Wakulima hao walitoa onyo kwa kigogo yeyote anayetaka kuingilia mgogoro huo hata kabla hukumu katika kesi ya msingi haijatolewa ajiendae kupambana nao popote iwapo sheria hazitazingatiwa. “mahakama ndiyo mwisho, alisema kwa msistizo mkubwa”.
Historia inaonesha kwamba mabavu na ubabe vimekuwa vikitawala kwa sehemu kubwa dhidi ya wanyonge hao. Kwa mfano uvunjaji wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Tawi la Makaani Gama ulifanywa hata kabla hati ya umiliki wa ardhi haijatolewa na Kamishna wa Ardhi.
Mwandishi wa habari hizi alipomfuata Mkuu wa Wilaya Kipozi na kumhoji alipata wapi ujasiri wa kuivunja ofisi ya CCM kabla hukumu ya Mahakama Kuu haijatolewa wala hati ya umiliki alijibu kwa kujiamini akisema “mimi nawakilisha maslahi ya serikali wailayani hapa, tayari serikali imemkabidhi ardhi mwekezaji na hawa wanavijiji wanakwamisha mradi huo.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika ofisi za Uhamiaji Makao Makuu ili kujiridhisha iwapo taratibu za idara hiyo zilifuatwa katika kutoa kibali cha makazi ya kwa mwekezaji wa Daraja A. Majibu ya afisa mwandamizi mwenye cheo cha Kamishina yalidhihirishwa kwamba taratibu hazikufuatwa.
Kwa kawaida sheria za uhamiaji zinamtaka mwekezaji ahamie nchini baada ya kukamilisha taratibu zote ikiwamo zile za Kituo cha Uwekezaji (TIC). Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mwekezaji wa kampuni ya Eco-Energy, Bw. Anders Bergfors ameishi nchini Tanzania tokea mwaka 2007 bila kuwa na shughuli yoyote ya uzalishaji hali inayozua maswali mengi kuliko majibu.
Mahojiano kati ya mwandishi wa habari hizi na mwekezaji yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo Bw. Amani Sinare.
Baada ya Afisa Uhamiaji wa Vibali (Residence Permits) kubanwa na mwandishi ni kwa nini Uhamiaji walishindwa kuchukua hatua na kumshauri mwekezaji huyo arejee nchini kwao wakati wawekezaji wenzake katika mradi huo waliopo nchini wakitafuta muafaka, alijibu kwa kifupi, Bwana mwandishi serikali imesema tutoe kipaumbele kwa wawekezaji wakubwa katika kilimo wewe unawasiwasi gani?
Naye mwekezaji alipofuatwa na mwandishi wa habari hizi kuelewa imekuwaje anaishi Tanzania tokea mwaka 2007 mpaka leo bila kazi yoyote alijibu kwamba kampuni yao ni ya kimataifa na kwamba aliingia nchini kwa kampuni ya SEKAB ambayo baadaye aliachana nayo na ardhi hiyo kuchukuliwa na Eco-Energy.
“Bw Mwandishi fanya uchunguzi wako vizuri mimi nimeingia ubia na serikali wa kuzalisha miwa katika ardhi hiyo jukumu la kunitafutia vibali vya uhamiaji ni la serikali siyo langu,” alijibu kwa kujiamini “mwekezaji huyo”
Baada ya mwandishi kuwasiliana na Uhamiaji ili kufahamu iwapo taratibu zimebadilishwa na kwamba sasa serikali ndiyo inawatafutia vibali wawekezaji afisa mwandamizi wa Uhamiaji ilijibu kwa ukali kidogo, Bwana mwandishi taratibu hazijabadilika hata hivyo siyo lazima serikali ikupatie siri zake!
Alipaombiwa kwamba kuna usiri gani katika uwekezaji na kwamba mwandishi huyu naye alikuwa akifuatia maslahi ya umma afisa Uhamiaji huyo aliangua kicheko na kukata simu. Hali hii ya sintofahamu ndiyo inayozua maswali kwamba nyuma ya mwekezaji Eco-Energy kuna mtu mzito anayetumia idara za serikali kufaniksha mpango huo.
Huku kukiwa na lindi la kushambulia waandishi wa habari  na kutoa vitisho hali mikoani pote ni hiyo hiyo linapokuja suala la ardhi. Kwa mujibu wa taarifa ya mahitaji ya kiusalama ambayo inahusisha mikoa 16, miwili Tanzania Visiwani na 14 Tanzania Bara miongoni mwa watetezi wa haki za binadamu walio katika mazingira hatarishi ni wale wanaofuatilia masuala ya ardhi.
Tuwasiliane: 0754-826272 na 0715-076272 na

barua pepe:  mhegera@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni