uhaba wa walimu huchangia katika mlundikano wa wanafunzi kama huu
Makala hii ilitumika katika
gazeti la Mtanzania Jumapili Oktoba 21, 2007
Na Elias Mhegera
Kutokana na uhaba mkubwa wa walimu wa shule za msingi na sekondari
hapa nchini serikali yetu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilibuni mpango wa mafunzo ya miezi mitatu kwa
wahitimu wa kidato cha nne na cha sita ili kukidhi mahitaji hayo.
Mpango huo umepongezwa na baadhi ya wadau wa sekta ya elimu lakini
pia wapo walioukosoa mpango huo, hoja hiyo ndiyo mjadala wa makala haya.
Licha ya kwamba kila mtu anafahamu kwamba lengo la serikali yetu
ni zuri katika mpango huo lakini wadau wengi wameonyesha wasiwasi wao juu ya
kiwango cha elimu na hivyo kumekuwepo na mijadala mingi juu ya suala hilo miongoni
mwa walioonyesha wasiwasi wao ni Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Lakini serikali tayari imejibu hoja zao kupitia kwenye vyombo vya
habari kwa tamko lililotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara husika Bwana
Oliver Mhaiki.
Nimeshawishika kutoa mchango wangu katika mjadala kama wafanyavyo watanzania
wengine na kwa kuzingatia kwamba nami pia ni mdau katika sekta ya elimu.
Kabla sijaingia katika undani wa mjadala wenyewe napenda
kutanabahisha kwamba hoja ya msingi inayotolewa na wale wanaopinga walimu wa
mafunzo ya muda mfupi ambao wamebatizwa mitaani kama walimu wa vodafasta.
Wamekuwa wakisimamia katika msingi wa maandalizi kwamba muda wa
miezi mitatu ni mfupi na hivyo hautoshi kumuandaa mwalimu na kuweza kutoa elimu
yenye kiwango kinachokidhi mahitaji ya kitaalamu.
Sipendi kuipinga hoja hiyo lakini napenda tuangalie upande wa pili
wa shilingi ambao ni kutoa elimu kwa watanzania wote kwa kuzingatia kwamba
elimu ni haki ya kimsingi ya binadamu.
Kwa mantiki hiyo naamini mjadala wowote wenye kufanyiwa utafiti wa
kina utalenga katika mambo yote hayo mawili ubora, na haki ya vijana wetu
kupata elimu.
Labda tukianza na hilo la ubora napenda niseme kwamba ubora wa
elimu huchangiwa na mambo mengi na wala si ubora wa walimu pekee.
Kwa mfano mazingira ambayo elimu hiyo hutolewa, vitendea kazi,
motisha kwa walimu, malezi ya watoto nyumbani na shuleni, na pia msukumo na
msaada wanaoupata watoto hao nyumbani katika dhamira ya kujiendeleza kielimu
Kuhusiana na hilo la mazingira ambapo elimu yetu inatolewa taasisi
ya HakiElimu imekuwa mstari wa mbele kulipigia kelele kupitia katika vyombo vya
habari japo wapo ambao wamekuwa wakidai kukerwa na matangazo hayo.
Katika hilo naomba tusiangalie mazingira katika mtazamo wa
madarasa na nyumba za walimu bali pia mishahara yao, usafiri wa kwenda na
kurudi kutoka ofisini, na marupurupu mengine yanayoweza kumvutia mwalimu ili
aipende kazi yake.
Tukiachana na hilo la ubora wa elimu tuangalie upande wa pili ambao
ni haki ya kila mtanzania kupata elimu katika mazingira tuliyonayo kijamii na
kiuchumi.
Naomba kuweka wazi ukweli kwamba serikali kwa muda mrefu imeshindwa
kutoa vivutio kwa walimu na hivyo wanajamii wengine wamekuwa na tabia ya
kuibeza taaluma hiyo bila kukumbuka kwamba kila msomi amepitia shuleni kwa
msaada wa walimu haohao tunaowabeza kutokana na vipato vyao duni.
Kwa maana hiyo si sahihi kusema kwamba Tanzania ina uhaba wa watu
wenye taaluma ya ualimu bali inao wataalamu wengi katika taaluma hiyo ambao
wameikimbia na kwenda kupata kazi katika maeneo mengine tofauti kama vile
benki, jeshi la polisi, uhamiaji, jeshi la wananchi, uandishi wa habari n.k.
Kuhama huko kwa wataalamu hao kumeacha pengo kubwa katika taaluma
hiyo na hivyo kuwafanya wachache waliojitolea ‘wenye wito’ kubeba mzigo
mkubwa na wakati mwingine kuonekana
kwamba ni watu wasio na upeo wa kuona mbali (vision).
Ni hao hao wanaoendelea kutupatia wataalamu huku wakiendelea
kupigania kuboreshwa kwa maslahi yao kwa kweli yataka moyo!
Kumbe hao walioamua kwenda kupata mafunzo ya muda mfupi wameonesha
dhamira nzuri ya kuwasaidia kaka na dada zao walioelemewa na mzigo kwa nini
basi tusiwaunge mkono badala yake tunawakatisha tamaa? Kwa hoja yangu hiyo
nadhani tayari nimeishaeleweka ninasimamia wapi, naomba tufanye kila jitihada
kuwaunga mkono hao walijitolea (volunteers) kwa kuwapatia kila aina ya msaada
ili nao wasije kimbia kama wale waliowatangulia.
Baada ya kuona kumekuwepo na vipangamizi vya hapa na pale katika
jamii niliamua nifuatilie mwenyewe ili nijue huko vyuoni walikoenda kwa miezi hiyo
mitatu wamefundishwa nini na kuangalia kama kile walichofundishwa kitasaidia
katika jamii kulingana na mahitaji tuliyonayo na lengo zima la kuwa na jamii yenye
elimu au uelewa hata kama si kwamba wote watafikia ngazi ya vyuo vikuu.
Bila kurefusha mjadala nimejifunza kwamba vijana wetu
wamefundishwa na kuelewa nini maana ya elimu yaani kwamba elimu ni mfumo
endelevu unaodhamiria kumuandaa mwanafunzi katika majukumu fulani katika jamii
yake.
Kwa maana hiyo elimu huanzia nyumbani na wala siyo shuleni kwani
katika mila zetu tuna mafunzo ambayo humuandaa kijana, humjenga kitabia,
humpatia nidhamu inayohitajika na pia kumfahamisha wajibu wake katika jamii yake,
kwa hiyo elimu haishii katika kusoma na kuandika pekee bali katika kujiandaa
kukabiliana na maisha ya baadaye.
Jukumu la mwalimu ni kuweza kuchanganua ni zipi tabia zinazofaa
ambazo mwanafunzi anastahili kufahamishwa na kwa maana hiyo mwalimu anaweza kutoa
ushawishi wa matendo mema, na anaweza pia kutumika kama nyenzo ya kuongeza
uwezo wa mwanafunzi katika kukabiliana na maisha yake ya baadaye.
Kwa malengo ya muda mrefu mwalimu humuandaa mwanafunzi kujipatia
utaalamu utakaomuwezesha kujiajiri mwenyewe au kuajiriwa katika taasisi
mbalimbali na serikali yenyewe.
Lengo mahsusi likiwa ni kujikimu katika maisha yake ya
baadaye. Kwa elimu wanayoipata wanafunzi
wa sekondari ni elimu tosha inayowawezesha kujiendeleza katika ujasiriliamali,
kilimo, uvuvi na mambo mengine ya kimaendeleo.
Elimu hiyo ni ufahamu tu utakaowawezesha kuyapokea vyema
maelekekezo watakayopewa na wataalamu mbalimbali kama vile wa kilimo, au tasisi
zinazojihusisha na wajasiriamali kama vile FINCA, PRIDE, CARE, WORLD VISION
n.k. kwa hali yoyote ile elimu ni muhimu sana katika jamii ya leo ili kuendana na
mazingira yaliyopo kwa sasa.
Mjadala wangu umelenga katika elimu ya sekondari kwani huko ndiko
wanakoelekezwa hao walimu wa maandalizi ya muda mfupi (crash programme), Bila
kujali kwamba wanafunzi wetu wametokana na walimu wa namna ile bado wanaweza
kujiendeleza na kufikia ngazi za vyuo vikuu kutegemeana na jitihada binafsi ya
kila mmoja wao.
Lakini hata kama itajitokeza kwamba wanafunzi wetu wasibahatike
kuipata elimu ya vyuo vikuu bado elimu wanayoipata katika sekondari inaweza
kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Kwa mfano somo la uraia yaani civics limesheheni elimu inayoweza
kumsaidia mhitimu uelewa wa kutosha katika jamii yake kama vile masuala ya demokrasia,
elimu juu ya UKIMWI. Maadili mema na njia mbalimbali za kuondokana na
umaskini.Ndani ya elimu ya uraia kuna mbinu za kilimo endelevu ambacho
hakitaathiri mazingira, kuna haki za binadamu n.k.
Silengi kuwaambia vijana wetu wakomee kidato cha nne kwa sababu
elimu hiyo imejitosheleza bali nataka kueleza kwamba kwa yule ambaye
hatabahatika kukanyaga chuo kikuu asijione kwamba ana mkosi bali elimu
ilivyoandaliwa kwa mtaala wa sasa imelenga katika kumuandaa katika maisha yake
ya baadaye hata kama hatafanikiwa kupata elimu ya juu. Ni lazima pia tukumbuke
kwamba bado tuna uhaba mkubwa wa vyuo vikuu na wahadhiri kwa hiyo safari bado ni
ndefu katika medani ya elimu nchini Tanzania.
Tukirudi katika hoja yetu ya msingi je hao walimu wa mfunzo ya
muda mfupi wanaweza kutoa elimu hiyo niliyoizungumzia hapo juu? Jibu ni ndiyo
kwa sababu kulingana na kile nilichokiona walichojifunza vijana wetu ni kwamba
japo mafunzo wanayopata ni ya muda mfupi lakini pia tukumbuke kwamba wao ni
wahitimu katika elimu ya sekondari kwa
hiyo wanachoongezewa huko vyuoni ni mbinu tu za ufundishaji.
Katika vyuo hivyo walimu hao hujifunza mambo kadhaa yanayoweza
kuathiri au kufanikisha uelewa wa
mwanafunzi (learning process)). Katika
mbinu hizo walimu hufundishwa tabia na mambo ambayo wanaweza kukabiliana nayo
darasani na jinsi ya kuyakabili.
Kwa maana hiyo walimu hao hupewa nyenzo zinazoweza kuwasaidia katika
kuwaelekeza wanafunzi wao kwa mambo
yaliyo muhumu katika maisha yao na kuachana na yale ambayo yanaweza kuathiri
maisha yao kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, ulevi na uovu mwingine.
Kwa kufanikisha hilo walimu huelekeza nguvu zao katika falsafa na
matarajio ya taifa letu kwamba kijana wa kitanzania anatakiwa awe wa aina gani
kwa hiyo vijana hupata maelekezo sahihi
kulingana na utamaduni wetu na kwa kutumia maelekezo sahihi ya wanafalsasa
wa elimu kama vile Mwalimu Nyerere na falsafa yake ya elimu ya kujitegemea.
Pia walimu hao huweza kung’amua ni jinsi gani ya kuwasaidia watoto
wetu au vijana wenye matatizo mbalimbali ambayo yanaweza kuathiri uelewa wa mwanafunzi kwa mfano ufukara uliokithiri nyumbani,
malezi mabaya, n.k.
Pia walimu hao huweza kung’amua ni jinsi gani ya kuwasaidia watoto
wetu au vijana wenye matatizo ambayo yanaweza kuathiri uwezekano wa wao kupata
elimu kwa kiwango sawa na wenzao wasio na matatizo ya kijamii.
Ina maana japo walimu hao wamepewa mafunzo ya muda mfupi lakini
pia wamefundishwa mbinu za ufundishaji na mazingira yanayoweza kuathiri au
kusaidia kueleweka kwa somo na wala siyo kwamba baada ya kutoka vyuoni basi
ndiyo ukomo wa wao kujifunza bali wanaweza kujiendeleza kwa njia
mbalilmbali kwa mfano kwa kuazima vitabu
katika maktaba, kwa kujiendeleza katika Chuo Kikuu Huria n.k.
Basi ni vyema tuelewe mbinu walizofundishwa kulingana na kile
nilichokipata mimi baada ya utafiti wangu binafsi.
Vijana hao wamefundishwa tabia na mienendo ya binadamu juu ya
uelewa kutokana na tafiti zilizofanywa na wataalamu kama vile Ivan Pavlov
ambaye alifanya utafiti wake akiwahusisha mbwa pale mbwa anaposikia mlio wa kengele
na kufahamu kwamba huo ni muda wake wa kupata chakula.
Kwa hiyo tafiti hizo zimeingizwa katika mbinu za ufundishaji kwa
walimu. Mambo mengine waliyojifunza ni umuhimu wa kurudia somo, ubaya wa adhabu,
na adhabu zinazostahili kwa wanafunzi na motisha mbalimbali ambazo zinaweza kuchagiza
katika wanafunzi kuongeza jitihada katika masomo yao (positive reinforcements).
Ninapotetea kuwepo walimu wa aina hiyo ni kwa sababu nimeridhika kwamba
japo kuna malalamiko kwamba wanaweza kushusha kiwango cha elimu lakini
wakosoaji wengi wameshindwa kupendekeza njia mbadala ya kuisadia serikali yetu
kukabiliana na upungufu wa walimu.
je wakosoaji hao wamejipa
nafasi ya kufuatilia nini walichofundishwa walimu wetu hao? Binafsi
ninapoangalia kile walichofundishwa na kwa kuzingatia kwamba elimu ni haki ya
kimsingi ya binadamu naona serikali imechukua uamuzi wa busara ili kuwapa uwezo
wale ambao walikuwa wamesahaulika.
Kwa mfano katika baadhi ya mambo ambayo wamefundishwa walimu wetu
hao tunaowabeza ni jinsi mihemuko (emotions) inavyoweza kuathiri tabia za
vijana katika rika fulani hivi elimu kama hiyo nayo lazima ukae miaka minne
chuoni ndipo uonekane kwamba umeiva?
Baada ya kuupitia mtaala wao nimejiridhisha kwamba mbinu walizopewa
japo ni kwa mafunzo ya muda mfupi lakini zinagusa maeneo mengi yanayomuwezesha
mwanafunzi kupata uelewa darasani (cognitive domains).
Kwa hiyo kinachofuata sasa ni jinsi ya kuyaweka katika utekelezaji
yale waliyofundishwa jambo hilo linategemeana na uwezo au kipaji cha kila
mmoja.
Mtaalamu wa saikolojia Robert Gagnèanasema suala la uelewa halitegemei
tu nini kimefundishwa darasani lakini pia uwezo wa mwanafunzi mmoja mmoja kutafsiri
kile alichojifunza. Katika hilo anasema wapo wenye uwezo wa kushika mara moja
kile walichojifunza, wapo wenye uwezo mdogo wa kuelewa na hivyo wanahitaji muda
mrefu wa ziada ili kuelewa kile walichojifunza
na lipo kundi la tatu ambalo ni kama la wasindikizaji kwani wao huchukua
muda mrefu zaidi kuelewa somo hilo hilo ambalo wenzao wamelielewa kwa muda
mfupi tu.
Ninaungana mkono dhana hiyo kwa sababu sote tunafahamu kwamba wapo
watoto wetu ambao bila tuisheni mambo hayaendi, wapo pia ambao kuwatafutia
walimu wa tuisheni ni sawa na kupoteza pesa zetu bure kwani huelewa somo mara
walipatapo darasani.
Katika msingi huo siyo sahihi kabisa kumlaumu mwalimu na kwa maana
hiyo tunapojadiliana uwezo wa wanafunzi kuelewa ama kutokuelewa tusikimbile
kuwatupia lawama walimu wa kitanzania bali tuangalie mazingira yote hayo na
jinsi ambavyo yanaweza kuathiri taaluma kwa ujumla.
Mtaalamu huyo Gagnèanasema njia sahihi ya kutatua tatizo hilo ni kuwatenganisha
wale wenye vipaji maalumu na wale wenye uwezo mdogo wa kuelewa (slow learners).
Maana yake ni kwamba kama wanafunzi hao wataendelea kukaa katika
darasa moja basi mwalimu atalazimika kurudia mara kadhaa kwa lengo la
kuwasaidia ‘slow learners’ hali hiyo inaweza
kuwakera ‘fast learners’. Naamini serikali yetu ilizangatia ushauri huo wa
kitaalamu na ndiyo maana kukawepo na shule zenye vijana wenye vipaji maalumu.
Lakini hii haimaanishi kwamba ‘slow learners’ watelekezwe kwani
hata wao mara baada ya kurudia mara kadhaa wanaweza kujikuta wamepata uelewa
sawa na wenzao lakini katika kundi la tatu huko ndiko ambako muda wa ziada
huhitajika na wala si kwamba hali hiyo hujitokeza katika shule za sekondari
pekee bali hata katika ngazi ya vyuo vikuu inaweza kujitokeza.
Nikilenga kuonyesha kwamba serikali inaweza kuwatumia vipi walimu
hao wa muda mfupi basi labda uwepo utaratibu ambao utawawezesha wahusika
kufanya kazi katika shule za kawaida badala ya kuwapeleka katika shule za
watoto wenye vipaji maalumu tukifanya hivyo tunaweza kuondosha tatizo la uhaba
wa walimu bila kushusha ubora wa elimu yetu hususani katika shule za sekondari na
zile za msingi.
Pamoja na kuzingatia ubora wa elimu bado ni muhimu tukumbuke pia
kwamba suala la elimu ni haki na hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba elimu ya
msingi imepitwa na wakati kulingana na
mazingira ya sasa kwa mantiki hiyo lengo liwe ni kuhakikisha kila mtanzania
anapata elimu ya kiwango cha chini isiyopungua kidato cha nne.
Tamko la haki za binadamu la mwaka 1948 linasema elimu ni mojawapo
katika haki za msingi za binadamu, kwa wakati ule elimu iliwekwa katika fungu
la tatu la haki za binadamu lakini kwa wakati tulionao elimu inatambuliwa
kwamba ni haki ya kimsingi na hivyo ni haki iliyo katika daraja la kwanza
(fundamental rights).
Katika hilo napenda kuwakumbusha wale wote wanaobeza jitihada za
serikali kutoa elimu ya sekondari kwanza kwa kudai kwamba serikali imefanya
papara kwa kujenga sekondari za kata, na pili kwa kuwaruhusu hao walimu wa muda
mfupi kufundisha kwamba wameonesha kukosa uzalendo na fadhila kwa serikali yao
kwa sababu hawajatoa suluhisho mbadala.
Kimsingi serikali isingeweza kuchukua uamuzi ule kwa lengo la
kuwadhuru wananchi wake, isipokuwa kuna ukweli kwamba katika dhamira njema hiyo
ya serikali yapo mambo kadhaa ambayo pia hayakuzingatiwa.
Katika hilo sina pingamizi, kwa mfano ubora wa baadhi ya majengo
ya sekondari za kata unatia mashaka, nimeshuhudia majengo mengi ya sekondari za
kata yakianguka hata kabla hayajaanza kutumika.
Katika hoja hiyo hiyo kuna tatizo la mazingira ambamo shule hizo
zimejengwa.Jambo hilo ni la kisera zaidi na pia linaendana na mwenendo mzima wa
siasa za nchi yetu kwa sasa yawezekana kuna utetezi kwamba hali ya uchumi ni
mbaya.
Kwa mfano tukifuatilia kwa makini tutaona kwamba ni kata chache
sana nchini zenye huduma muhimu kama vile maji na umeme hiyo ni pamoja na
miundo mbinu mingine kama vile barabara zinazopitika katika kipindi cha mwaka
mzima.
Mazingira ya aina hiyo yanaweza kuondosha ari za walimu kufanya
kazi katika sekondari hizo ambazo zimechipuka kama uyoga nchini pote.
Sanjari na hilo ni urasimu uliopo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi yawezekana urasimu huo unatokana na uendeshaji mbaya lakini pia inawezekana
kwamba wizara hiyo imeelemewa na mzigo kutokana na ukweli kwamba imeajiri watu
wengi kuliko wizara yoyote nchini.
Mwaka 1990 rais wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi aliunda
Wizara ya Sayansi Teknlojia na Elimu ya juu katika kupunguza mzigo uliokuwa
unaikabili wizara ya elimu kwa wakati ule. Pamoja na jitihada hizo bado matatizo
ya shule yanaelekezwa katika halmashauri za wilaya lakini bado inaonekana
jitahada zote hizo hazijapunguza kwa kiwango kikubwa matatizo yanayoikabili
wizara hiyo.
Pamoja na kuzidiwa na mzigo wa uendeshaji kutokana na wingi wa
shule bado kuna tatizo la mfumo usiozingatia haki ambapo watendaji wizarani
hupendelea kusikiliza upande mmoja yaani wa wakuu wa shule bila kuwasikiliza walimu
ambao ni wataalamu na taifa limewaelimisha kwa gharama kubwa kwa hiyo yote hayo
ni mazingira yanayostahili kuzingatiwa katika dhamira ya kuboresha viwango vya
elimu katika sekondari zetu.
Ukiondoa mapungufu hayo machache naamini wizara husika inajitahidi
kwa kiwango kikubwa katika jukumu lake la kutoa elimu kwa watanzania wote bila
ubaguzi wa dini, kanda, kabila, rangi na mambo kama hayo.
Yapo marekebisho machache yanayohitajika ili kuwavutia walimu
waendelee kuipenda taaluma yao
(retention scheme) kwa hiyo
wizara inatakiwa kubuni mbinu za kutoa motisha kwa walimu.
Kwa sababu wote tunaona umuhimu wa watoto wetu kupata elimu bora
ni muhimu pia tukatoa mchango wetu wa jinsi ya kuboresha elimu nchini badala ya
kuwa wakosoaji wazuri bila kutoa njia mbadala.
Naomba kutoa changamoto hiyo kwa wakosoaji wote na hasa
ikizingatiwa kwamba mwishoni mwa miaka ya sabini serikali ilianzisha mpango wa
elimu ya msingi kwa wote Universal Primary Education (UPE).
Mpango huo pia ulikutana na upinzani kama huu ulijitokeza sasa.
Wapo waliodiriki kuwakejeli walimu wale kwamba walikuwa walimu weupe kwa maana
ya kwamba hawakuwa na lolote vichwani mwao.
Basi na tuwape nafasi hawa walimu wetu badala ya kuwavunja moyo,
lakini si kwamba tuangalie upande huo wa kwamba watatoa elimu tu bali kwamba hiyo
ni njia mojawapo ya serikali kutoa ajira kwa vijana wake ambao vinginevyo
wanaweza kijiingiza katika vitendo viovu kutokana na kusahauliwa na serikali
yao.
Tukumbuke ambavyo serikali imekuwa ikiahidi kutoa ajira kwa vijana
mara kwa mara hatuoni kwamba kwa njia hii serikali imefanikiwa kwa kiwango fulani
kupunguza ukali wa maisha kwa vijana wetu ambao katika umri wao hutawaliwa na ndoto
nyingi labda kutokana na vyombo vya habari ambavyo vianaonesha mambo ambayo
wakati mwingine hayaendani na hali halisi?
Jambo la muhhimu ni kuwaongoza ili wakamilike katika dhamira yao
(professional guidance). Kwa mfano tukiangalia katika jeshi la wananchi
tutakuta wapo askari wengi ambao walianzia katika ngazi ya mgambo lakini
wamewezeshwa na kupanda ngazi mbalimbali hadi kufikia viwango vya juu jambo
hili linafanyika katika taaluma nyingi, jeshi la polisi, magereza.
Katika mahospitali wapo wahudumu ambao baadaye wamegeuka na kuwa
wauguzi wazuri au hata madaktari kwa nini isiwe katika ualimu?
Na wala si hivyo tu hata
tukienda katika vyuo vikuu tutawapata wahadhiri waliobobea ambao walianzia
katika ngazi ya ukutubi na wameweza kupanda hadi kufikia ngazi ya uprofesa
kamili katika fani ya uandishi wa habari wapo waandishi walioanzia katika
ukarani leo ni waandishi maarufu.
Naamini mifano hiyo
michache inatosheleza kuonesha kwamba si jambo jema kuwabeza walimu hao
waliobatizwa huku mitaani kwamba ni walimu wa vodafasta bali waungwe mkono kwa
kila hali na serikali, wadau na wananchi wote kwa ujumla.
Nategemea mjadala haujafungwa bado upo wazi kwa kila mtanzania
kuchangia ili mradi uchangiaji huo uwe una lengo la kufanikisha kwa maana ya
kujenga wala siyo kubomoa ni ukweli usiopingika kwamba vyama vya kitaalamu kama
CWT vinayo nafasi kubwa ya ushawishi katika masuala yanayohusiana na elimu
lakini pia tusisahau kwamba elimu ni haki ya kimsingi ni vyema tukawawezesha na
wenzetu wakaipata kama tulivyobahatika kuipata sisi.
Naamini mawazo yangu yatachukuliwa katika mtazamo chanya kwamba
yametolewa kwa kuzingatia haki za binadamu na wala si katika misingi ya kisiasa
Mwandishi wa mkala haya anapatikana kwa simu 0754 826 272
Na kwa barua pepe mhegeraelias@yahoo.com

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni