Jumapili, 6 Julai 2014

MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI NI AIBU KWA TAIFA



 

Pichani: Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na wanakijiji wa  Mtanzania Januari 16, 2013 wakati alipokwenda kuwapa pole  kufuatia uvamizi waliofanyiwa  na watu wanaosadikiwa kuwa wafugaji ambao waliua watu watatu  na kuchoma nyumba . Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo.
Na Elias Mhegera
Asasi za kiraia na wadau wa ardhi wameendelea kuonyesha wasi wasi wao kutokana na kushindwa kwa serikali kukabiliana na migogoro ya ardhi ambayo tayari imesababisha madhara makubwa ikiwamo kupotea kwa maisha ya watu kadhaa.
Wasi wasi huo ulijidhirisha katika mjadala uliondaliwa na asasi ya uchambuzi wa sera na mipango ya Policy Forum ukiwa ni mdahalo wa kumaliza mwezi Januari.
Mdahalo huo uliofanyika katika ukumbi wa British Council tarehe 31 Januari, ambapo ilidhihirika kwamba migogoro ya ardhi imeporomosha uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa. 
Mdahalo wenye kichwa cha habari “Migogoro ya Ardhi na Misitu ni Suala la Kiutawala? Ulilenga katika kuchambua vyanzo vya migogoro ya ardhi, athari zake kwa taifa na kushauri juu ya ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Mada ya ufunguzi ilizungumzia uhusiano uliopo kati ya uwekezaji katika kilimo na migogoro ya ardhi, na mtoa mada Bw Alais Morindat ambaye ni mshauri mwelekezi wa masuala ya ardhi na mazingira akiwakilisha taasisi ya Institute for Environment and Development (IIDE).

Mtaalamu huyo alisema kwamba migogoro mingi imekwama kwa sababu ya kukosekana kwa utashi wa kuisuluhisha kutoka serikalini. “Huwezi kupata ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kwa kuanza na fikra kwamba tabaka moja halitikiwi kuwapo” alisema Morindat.
Alikuwa akiirejea kauli ambayo mara kadhaa imekuwa ikitolewa na viongozi mbali mbali akiwamo Rais Kikwete kwamba ufungaji wa makundi makubwa ya ng’ombe umepitwa na wakati.
Kwa bahati mbaya kauli hiyo imekuwa pia ikitolewa na wanamazingira wengi licha ya wanasiasa. Hata hivyo mtaalamu huyu ambaye anaweka bayana kwamba anatoka katika jamii ya wafugaji wa Kimasai anapingana na dhana hiyo.
Anasema ufugaji wa kienyeji ni suala la kimila na kiutamadani licha ya kwamba pia ufugaji umekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Anautetea ufugaji kwamba hauna madhara makubwa katika ardhi na kinyume chake kinyesi cha mifugo husaidia kuongeza rutuba na hata kwa kutengeneza gesi na hivyo kuokoa miti na mazingira kwa ujumla.
Anatetea kwamba wafugaji wamekuwa wakifanya mambo makubwa kiuchumi kwa sababu wanafanya shughuli mbili kwa pamoja, kilimo na ufugaji kwa wakati mmoja.
Hivyo basi anaulaani mtazamo hasi dhidi ya wafugaji hususani wale wa kimasai ambao huonekana kwamba ni watu walioachwa nyuma, wakorofi na wasiopenda kubadilika “huu ni mfumo mbaya na unawadhalilisha wafugaji,” anatetea.
Anayachambua mambo kadhaa anayodai kwamba ndiyo chimbuko la kuwatenga na kuwabagua wafugaji. Kwanza anasema ni mitazamo ya kiutandawazi inayolenga kukamata ardhi ya Afrika kwa kisingizio cha uwekezaji.
Pia anasema kwamba watunga sera wanatakiwa kuwa makini badala ya kukurupuka na kuanza kutimiza mambo kadhaa kisiri siri kabla ya kuwashirikisha wananchi, anasema jambo hili ni hatari kwa mustakabali wa usalama wa nchi.
Anashauri kwamba badala ya kutafuta namna ya kuondokana na ufugaji wa kimila serikali inatakiwa kupanga mikakati ya kushirikiana na sekta nyingine kwa lengo la kuwaendeleza wafugaji hao.
Na zaidi ya hayo adai kwamba serikali haiwezi kujivuna kwamba inazingatia haki za binadamu na utawala bora wakati ikishindwa kulilinda tabaka kubwa la wazalishaji linaloelekea kuangamia.
Katika kuachana na dhana ya utetezi wa kundi la wafugaji, muwasilishaji mwingine Bw Steven Mariki ambaye ni Mkurugenzi wa Taifa wa Mradi wa Uratibu wa Madhara ya Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (UNDP) anakuja na mtizamo tofauti.
Analiangalia tatizo la migogoro ya ardhi katika mtazamo mpana zaidi na kusema kinachotokea sasa ni hitimisho la matatizo yaliyojengeka kwa muda mrefu. Anasema kwamba matatizo ya sasa yanatokana na udhaifu uliosababishwa na mambo mengi.
“huwezi kuielezea migogoro ya ardhi kwa kutumia kiashiria kimoja, bali unatakiwa kufahamu kwamba kuna udhaifu katika sera zaardhi, katika sheria na hata katika mchakato wa kupanga vipaumbele vya taifa” anadokeza.
Akifafanua zaidi anasema kwamba mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani pia yamechangia sana katika migogoro ya ardhi inayoendelea nchini.
Kwa mfano; utolewaji wa fedha za wafadhili kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya kilimo umesababisha watu ambao hapo zamani hawakuwa na mawazo ya kujishirikisha katika kilimo kuhamia huko ghafla.
Pia anasema kujengeka kwa miundombinu ya barabara kumesababisha watu wengi kuyafikia kwa urahisi zaidi maeneo ambayo hapo zamani yalikuwa na changamoto kubwa.
Lakini pia anasema sera za uwekezaji katika kilimo, kwa malengo mbali mbali kama vile uzalishaji wa mazao kwa ajili ya uzalishaji wa nishati kama vile miwa na jatropha yamechangia katika kukithiri kwa migogoro ya ardhi.
Anakiri kwamba kwa bahati mbaya uwekezaji huo umeambatana na kuondolewa kwa nguvu kwa wakulima katika maeneo yao vijijini kwa lengo la kuikabidhi ardhi yao kwa “wawekezaji”.
Anasema yapo matatizo mengi ikiwamo udhaifu wa uendeshaji katika wizara ya ardhi ambao husababisha urasimu na wakati mwingine hata hutokea watu kadhaa wakagawiwa ardhi hiyo mara mbilimbili kama siyo tatu na mamlaka hiyo hiyo.
Bw Mariki anasema kwamba hata kabla ya kuingia kwa ukoloni watu wa makabila mbali mbali waliweza kujipangia matumizi ya ardhi na kubakia na amani lakini leo migogoro yote inaishia mahakamani ambako kuna ucheleweshaji mkubwa wa kupatikana kwa ufumbuzi.  
Kwa upande wa sera na mipango ya ardhi anasema kwamba lipo tatizo la kuachana na mipango ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi na kukimbilia katika mipango mipya isiyoeleweka vizuri.
“Inashangaza kuona kwamba ardhi iliyowekewa mipango ya muda mrefu kwa ajili ya uhifadhi wa vyanzo vya maji mara inageuzwa kuwa kwa ajili ya uwekezaji na hata ardhi kwa ajili ya vijiji inageuzwa kwa ajili ya mwekezaji, haya ni mabadiliko hasi yanayoleta mkanganyiko mkubwa, “ anaonya.
Anashauri kwamba kabla ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) kupokea maombi iwasiliane kikamilifu na taasisi nyingine ili kuepuka uwezekano wa migogoro ya ardhi. Anashauri kwamba kabla ya serikali kugawa ardhi iwashirikishe wadau wengine zikiwamo asasi za kiraia.
Katika michango ya mawazo kutoka kwa wadau mbali mbali wanaonesha hasira kwamba serikali imewatupa wanyonge tofauti ni ilivyokuwa enzi za Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania ambaye alitoa kipaumbele kwa maendeleo ya vijijini likiwamo suala la usalama.
Prof. Adolfo Mascarenhas anasema kumekuwapo na udanganyifu mwingi juu ya malengo mahsusi ya ardhi inayochukuliwa, “siamini kwamba ardhi yote inayochukuliwa ni kwa ajili ya uwekezaji, na wala siamini kwamba kila kampuni inayotajwa ni kampuni halisi, baadhi ya makampuni ni bandia kwa lengo la kupora ardhi tu” anaonya.
Hoja yake inaungwa mkono na afisa mipango ambaye pia ni mwanasheria kutoka HakiArdhi Bw Godfrey Massay anayesema kwamba kumekuwapo na kampeni kubwa katika vyombo vya habari kwamba kuna wawekezeji watakaotoa ajira lakini mwisho wa siku wakulima wanaoondolewa wala hawalipwi fidia.
Anadai jambo la kushangaza zaidi ni kwamba ardhi inabakia bila uzalishaji kwa muda mrefu hali inayooongeza umaskini hususani katika maeneo ya vijijini ambako ndipo kuna idadi kubwa ya Watanzania.
“Kuna maeneo mengi ambayo sasa hayazalishi kwa sababu eti wamekabidhiwa wawekezaji au kwa sababu yapo katika kesi mahakamani na hivyo shughuli za uzalishaji zinasimama,” anafafanua.
Naye Bi Ashura Kayupayupa anayejitambulisha kwamba ni mwanaharakati wa haki za vijana anasema kwamba umilikishwaji wa ardhi Tanzania unautata mkubwa kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaweza kutoa tamko la kuchukua sehemu kubwa ya ardhi kwa kile kinachoitwa manufaa ya umma lakini bila kuwafafanulia wananchi kwamba ni manufaa gani hayo.
Maneno hayo yanamnyanyua katika kiti Bw. Francis Uhadi kutoa Norwegian Church Aid anayesema kwamba akiwa mtumishi wa asasi ya mtandao wa masuala ya ardhi, Tanzania Land Alliance (TALA) alijifunza mengi juu ya dhulma zinazofanyika dhidi ya wanyonge.
“Kuna ulaghai mkubwa katika uporaji wa ardhi, wanyonge wanaambiwa watoe vyeti au nyaraka za kuthibitisha mikataba ya umiliki wakati inafahamika kwamba mambo hayo hayakuwahi kupewa kipaumbele kwa muda mrefu, kinachosumbua si udhaifu wa sheria bali ni tamaa za wanasiasa na matajiri wengine, ambao hawataki kuzingatia sheria,” anasema kwa sauti ya ukali.
Anafafanua kwamba leo taasisi za umma kama vile TIC, inaweza kutumika kisiasa kiasi kwamba hao hao waliokuwa wanazungumzia uwekezaji katika miwa kwa ajili ya nishati sasa hivi wamehamishia masikio ya Watanzania kwenye gesi asilia huku tayari wakiwa wamejilimbikizia ardhi za wanyonge.
Naye Bw Geoffrey Mwanjelwa anasema kwamba anahofu juu ya kile kinachoitwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali “Public –Private Partnership” (PPP), anasema huo ni mfumo mwingine wa wanasiasa wetu kujinufaisha na mali za umma.
“huwezi kujua nani anamiliki hiyo sekta binafsi kwani unaweza kuwa ni mradi wa mwanasiasa na akatumia nafasi yake kuipatia kampuni yake iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine,” anafichua na kusababisha kicheko ukumbini.
Anasema kila siku kuna miradi na mipango mipya kama ilivyokuwa kwa Kilimo Kwanza na hata Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) ambao yeye anauona kwamba ni muendelezo wa mikakati hiyo hiyo ya kupora ardhi za wanyonge na kuwaacha katika lindi la umaskini.
Naye mtaalamu wa misitu Bw. Kahana Lukumbuzya anasema kwamba pamoja na kwamba watu wenye nafasi wamekuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali,  lakini pia kumekuwapo na ongezeko kubwa la Watanzania ambao kabla ya uhuru walikuwa chini ya milioni kumi lakini leo wanakaribia milioni 50.
Hata hivyo hoja hiyo ilimnyanyua tena Prof Mascarenhas akipinga vikali kwamba hoja si ongezeko la idadi ya watu bali ni ongezeko la ubinafsi na tamaa mchango huo unasabibisha vicheko vingi ukumbini.
“Tumepoteza tunu za umoja wa kitaifa” anasema kwa kujiamini mzee huyo ambaye amekwisha vuka umri wa zaidi ya miaka 70.
Naye Bi Maureen Kwilasa ambaye ni mtetezi wa masuala ya jinsia ambaye kwa sasa yupo katika mafunzo kazini katika shirika la Oxfam anasema kwamba wakati kunapokuwa na mijadala juu ya migogoro ya ardhi mara nyingi wataalamu husahau kuangalia athari za ziada kwa watoto na akina mama.
Anakumbusha kwamba migogoro ya siku hizi huendana na ukatili na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu ambayo huwaathiri zaidi wanawake na watoto ambao hawawezi kuchukua silaha na kukabiliana na wavamizi.
Bw Laurent Joshua kutoka Tume ya Haki za Binamu na Utawala Bora (CHRAGG) anasema kwamba kulingana na tafiti zilizofanywa na taasisi yake migogoro mingi ya ardhi husababishwa na rushwa.
Hoja hiyo inaungwa mkono na mwansheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bw. Paul Mikongoti ambaye anasema kituo chake pia kimepata taarifa za kuwepo na matumizi ya rushwa katika upatikanaji wa ardhi hali ambayo mwishowe husababisha migogoro mikubwa.
Anakumbusha hali yenye utata ya bonde la Kapunga ambayo ilimfanya Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka kushindwa kutoa msimamo unaoeleweka hali inayoonyesha kwamba kuna utata katika baadhi ya maamuzi ya serikali.
Maeneo yanayotajwa kuwa na migogoro hatarishi kwa sasa ambayo hupoa na kuibuka tena ni pamoja na maeneo mengi mkoani Morogoro, Bonde la Ihefu, Kilombero, Ulanga, Basuto, Bonde la Mto Rufiji, Mvomero, Kiteto, Simanjiro, Loliondo, Babati na Mpanda.
Mwaka 2010 ikiwa ni siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu Mbunge wa Maswa Mashariki? Bw. John Shibuda alisema kwamba kumekuwapo na ubaguzi wa namna masuala ya wafugaji yanavyoshughulikiwa akidai kwamba wafugaji wa Kisukuma hawana msaada kama ilivyokuwa kwa makabila mengine ya wafugaji.
Haileweki kauli yake hiyo ilikuwa na ukweli kwa kiwango gani au ililenga kupata manufaa ya kisiasa na ndiyo maana itatolewa kwa wanahabari. Lakini msimamo kama huo unaungwa mkono na mfugaji wa kisukuma aliyepo Mkoa wa Katavi Dom training ambaye anasema kwamba wafugaji wanahangaika na makundi yao ya mifugo baada ya kufukuzwa eneo moja kwenda jingine.
Hivi karibuni mwandishi wa habari hizi alishuhudia habari katika mojawapo ya vituo vya televisheni wananchi wa Babati ambao walikuwa na kilio kikubwa baada ya kuchomewa nyumba zao na watu waliodaiwa ni askari wa wanyama pori kutoka katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akijibu hoja za mwandishi wa habari za televisheni Mkurugenzi Mtendaji wa TANAPA Bw. Alan Kijazi alisema nyumba zilizochomwa ni za watu waliolipwa fidia miaka minane iliyopita lakini walikuwa wamekaidi agizo linalowataka wahame katika maeneo ya hifadhi.
Hoja ya Kijazi kwamba walioondolewa watapewa maeneo mengine ilipingwa vikali na wananchi hao huku mmoja wao akitamka “eti wanasema watatulipa fidia hatutaki fedha tunazo za kutosha, tunataka ardhi yetu” alimaka.
Kauli za wanavijiji hao zinawakilisha wananchi wengi ambao wanasema serikali imekuwa haiwashirikishi kikamilifu katika kuchukua ardhi bali inawaburuza kwa kutumia vitisho na Jeshi la Polisi, ikiwamo uchomaji wa nyumba za wakulima.    
Mkuu wa Wilaya ya Babati Bw. Khalidi Mandia naye anadai kwamba wananchi walikwisha lipwa fidia na anaonekana hana majibu ya uhakika kwa wananchi wenye hasira isipokuwa anaweza kutimiza tu “maagizo ya serikali” ya kuwaondoa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni ya hifadhi.
Asasi za kiraia zinashauri kuwepo na uwazi na uhakiki zaidi juu ya wamiliki halisi wa hayo yanayoitwa ni makampuni ya wawekezaji ambapo kumekuwapo na tabia ya viongozi wa juu serikalini kuanzisha makampuni bandia na kudai eti ni ya wawekezaji kwa lengo la kupora ardhi.

Tuwasiliane: mhegera@gmail.com simu: 0754-826272

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni