Jumamosi, 19 Julai 2014



Kiongozi wa Kanisa Katoliki Tanzania Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo 
TUHESHIMU DINI ZETU LAKINI PIA TUSIBEZE UTAMADUNI WETU

Novemba 25, 2007 Mtanzania Jumapili

Na Elias Mhegera
Kutokana na vuguvugu la kutaka kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi hapa nchini tayari baadhi ya Watanzania wameanza kuwa na hofu kwamba  nchi yetu inaweza kuingia katika malumbano ambayo yanaweza kuondoa amani na utulivu mambo ambayo yamedumu kwa muda mrefu hapa nchini.

Lakini pia kuna hofu kwamba mivutano ya sasa inaweza kusababisha mambo ambayo yaliwahi kujitokeza huko nyuma kuhusiana na mivutano ya kidini makala haya yanajadili hofu hiyo.

Labda tuanze na kile kilichoandikwa na mwandishi mahiri nchini Joseph Mihangwa katika gazeti la Raia Mwema, toleo la Novemba 14-20, 2007.mada ya udini inajadiliwa katika Nasaha za Mihangwa na makala yake yenye kichwa cha habari ‘Nalilia utamaduni wangu, nimechoshwa na udini’

Kimsingi Mwandishi Joseph Mihangwa ametoa duku duku lake kulingana na hofu iliyoibuka kwamba mjadala wa Mahakama ya Kadhi unaweza kuleta mitafaruku nchini. Nami naungana mkono naye katika hilo japo napenda pia kuonyesha tofauti zangu kuhusiana na mustakabali wa hizi dini ambazo yeye ameziita ni za mapokeo.

Tofauti yangu na Mihangwa ni kwamba ni vigumu kwa sasa kusema tunaweza kuziondosha hizi dini ‘za kigeni’ yaani Uislamu na Ukristu kwa sababu tayari zimeishajikita ndani ya damu na roho zetu, lakini pia ni kwa vizazi na vizazi kwa hiyo zoezi la kuziondoa linaweza kuwa gumu.

Jambo la msingi ninaloona linaweza kutusaidia ni kutafuta maelewano ili kuheshimiana na kuweza kuishi bila migongano (dialogue).

Hata vile kwa sababu huo ulikuwa ni mtazamo wake binafsi Mihangwa anayo haki hiyo kwa sababu katika nchi yetu suala la imani ni suala binafsi na kila mtu amepewa uhuru wa kuchagua dini anayopenda ili mradi havunji sheria za nchi. Kwa mtazamo huo ni haki yake ya msingi kama ameamua kurudi katika dini yake ya mizimu.

Miaka kadhaa iliyopita nilisoma makala ya Mihangwa mmoja wa waandishi ninaowaheshimu sana kutokana na misimamo yao isiyoyumba. Makala hiyo ilikuwa inaiomba Tume ya  Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kumuunga mkono ‘Dkt’Matunge kutokana na uvumbuzi wake wa usafiri wa ungo.

Sielewi Mihangwa alimaanisha nini katika makala ile, au labda alilenga kutoa burudani tu kwa wasomaji wake. Ndiyo maana hata sasa ninakuwa na wasi wasi huo kwa sababu siamini kwamba anachokisema Mihangwa ni jambo linalowezekana katika mazingira ya sasa (feasible).

Hofu yangu hiyo inatokana na ukweli kwamba hata huo usafiri wa ungo sijawahi kuamini kwamba upo au ipo siku utakuwapo.

Lakini naomba nisieleweke kwamba mimi ni mmoja katika wale wanaomini kwamba mambo mengi hayawezekani, au yapo kwa malengo yasiyodhahiri (ploys), na kwa maana hiyo nisiwekwe katika kundi hilo la watu wenye hofu kila wakati (cynics).

Mataifa kadhaa yanao watu wasiofuata uislamu wala ukristu, kwa mfano Uchina, Japan na Korea kuna wafuasi wengi wa dhehebu la Confuscianism, Iran napo kuna wafuasi wa Baha’i madhehebu yote niliyoyataja hayafuati Uislam wala Ukristu. 

Hofu yangu ni kwamba iwapo tutakubaliana kimsingi kwamba tuziondoe hizo dini ‘za kigeni’ basi tusitarajie kwamba moja kwa moja tutakuwa tumetoa nafsi ya kukua kwa tamaduni zetu za kiasili maana hata dini zetu ambazo zilikandamizwa na ujio wa wageni. Sana sana matokeo yake kutakuwa na ombwe (vacuum) ambalo linaweza kuleta matatizo makubwa katika jamii.

Japo mimi banafsi nimelelewa katika malezi ya Kanisa Katoliki, lakini pia ninayo mengi ninayokubaliana na Mihangwa na wala sitaki nionekane kwamba ni muasi wa dini yangu isipokuwa kwamba naongozwa na mambo mawili makubwa kwamba kama tunavyofundishwa na historia.

Na pia taaluma ya uandishi wa habari naongozwa na misingi ya kitaaluma ambayo inatanguliza ukweli kwa sababu ukweli siku zote ndio unaotuweka huru.

Kwa mfano ni ukweli usiopingika kwamba wamisionari wa kwanza walichangia sana kuingia kwa ukoloni kwa sababu walipeleka nyumbani taarifa juu ya mambo mazuri waliyoyakuta Afrika (prelude) hali iliyowafanya mabepari wa kikoloni waje kuwekeza na kunyonya raslimali za bara letu.

Lakini ukiachana na hao wamisionari kuna upande wa pili wa shilingi ambapo Waarabu walifika na kuwakamata mababu zetu na kuwauza kwa wazungu tayari kwa kupelekwa utumwani.Huo ndiyo ukweli ambao hatuwezi kuufuta katika historia kuhusu kuingia kwa Ukristo na Uislamu katika bara la Afrika.

Pamoja na kwamba Waarabu walikaa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu wakitafuta pembe za tembo na watumwa lakini ni katika maeneo hayo hayo ambako Uislamu ulishamiri.

Anzia Ujiji Kigoma, uje Tabora ambako kulikuwa na kambi ya mapumziko ya watumwa nenda Bagamoyo, na Dar es Salaam tayari kuingizwa katika mashua tayari kwa kusafirishwa kwenda Amerika ambako mpaka leo tuna kizazi cha watu weusi (African Diaspora).

Ninachomaanisha hapa ni kwamba hoja ya Mihangwa inagusa mazingira hayo ya kuingia kwa dini hizo na sasa zinataka kugeuka kuwa vyanzo vya vurugu badala kujenga umoja ambao unatokana na utamaduni wetu wa Afrika.

Yawezekana wale wanaotaka kutumia dini kutugawanya hawana kumbukumbu hiyo au vinginevyo wameamua kusamehe yale yaliyofanywa na wamisionari na Waarabu wakati wa kuingia kwao  barani Afrika.

Hivi karibuni wakati akitawazwa kuwa kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alionya juu ya tabia ya viongozi wa dini kujaribu kuitumia dini kwa manufaa ya kisisa.

Japo hakutaja jina la mtu lakini imani yangu kubwa ni kwamba alimlenga Mchungaji Mtikila ambaye amekuwa katika mzozo na serikali akipinga hiyo mahakama ya kadhi. Wakati akiachiliwa kwa dhamana Mchungaji Mtikila alipokelewa na viongozi wengine wa dini wenye mtazamo kama wake.

Ni dhahiri kwamba jambo hilo linatoa taswira kwamba hoja hii ya Mahakama ya Kadhi inao wapinzani wengi na wala si Mtikila pekee.Kwa hiyo huo ni ujumbe tosha kwa serikali kwamba jambo lolote ambalo linakutana na upinzani katika baadhi ya makundi ya jamii yetu basi lipewe uzito unaostahili hata kama lengo la jambo hilo nia yake ni njema (bonafide).

Ukweli wa hilo unatokana na ukweli kwamba kwa miaka kadhaa serikali yetu imedhamiria kujenga jamii yenye usawa na isiyokuwa na ubaguzi wa namna yoyote ile, sasa kama leo tutaanza kuyumbishana ina maana tutakuwa tumeondoa ile dhana kwamba serikali yetu haina dini isipokuwa watu wake ndiyo wenye dini (secularism).

Kwa lengo la kuondoa manung’uniko yasiyo na tija kwa ujenzi wa jamii yetu jambo la Mahakama ya Kadhi linaweza kufanywa kwamba ni jambo la ndani la dini husika na wala lisifike mahali likaonyesha kwamba dini fulani ni nyeti (unique) kuliko dini nyingine hali hiyo ikiendekezwa inaweza kuleta athari za udini (bigotry), tukifikia hapo basi hiyo ndiyo safari kuelekea kwenye machafuko.

Ikumbukwe kwamba hata neno ruksa kwa mara ya kwanza Mzee Ali Hassan Mwinyi alilitumia alipokuwa akihalalisha watu kula aina yoyote ya chakula bila kuingiliwa katika maamuzi yao. Akasema anayetaka kula chura ruksa, anayetaka kula nyoka ruksa. Hiyo ilifuatia kikundi cha Waislamu wenye ‘itikadi kali’ kuvamia bucha ya nguruwe ‘kiti moto’na kuvunja bucha hiyoya Mbokomu maeneo ya mwembechai.

Tukiyafanyia mzaha mambo ya dini yanaweza kuwasha moto ambao baadaye tutashindwa kuuzima. Mwaka 1966 nchini Nigeria yalizuka machafuko makubwa kutokana na mivutano ya kidini kati ya waislamu na wakristu.Chanzo cha mgogoro huo ni tabia ya wa Ibo ambao wengi wao au takribani wote ni wakristu kujiamulia mambo yao kinyume na serikali kuu ambayo ilionekana kulalia upande wa uislamu.

Kwa mfano katika mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina wa Ibo walikuwa wanawaunga mkono Waisraeli wakati ambapo serikali kuu ilikuwa inawaunga mkono Wapalestina. Jambo hilo liliilazimisha serikali kuu kutunga sheria ambapo watu wote walilazimika kuzifuata nchini humo.

Kwa upande wao wa Ibo hawakuridhishwa na baadhi ya sheria zilizokuwa zimelalia katika misindi ya dini ya kiislamu (shariah)  na hapo ndipo wa Ibo wakiongozwa na Ezekiah Odumwegu Ojukwu wakatangaza kujitenga kwa Jimbo la Biafra kwa lengo la kuunda serikali yao kamili mpango ambao ulisababisha machafuko na vifo vya watu kadhaa.

Tatizo la Biafra lilichukua sura ya kimataifa ambapo Mwalimu Nyerere pia alimuunga mkono Ojukwu, na mataifa mengine yaliiunga mkono serikali kuu. Haishangazi Ojukwu alikuwa mmojawapo wa Wanaigeria walioambatana na Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegen Obasanjo katika Mazishi ya Mwalimu Nyerere mwezi Oktoba 1999.

Kwa hapa Tanzania ukiachana na suala la mabucha ya Mbokomu kumekuwapo na matatizo ya mara kwa mara katika msikiti wa Mwembechai . Vurugu hizo zimewahi kusababisha kuvunjwa vunjwa kwa vioo vya magari ya serikali na hata kuuawa kwa kuchomwa visu kwa askari polisi katika machafuko ya aina hiyo wafuasi wawili madhehebu ya Kiislamu wamewahi kuuawa.

Labda katika harakati za ‘kumtafuta mchawi’ chama cha upinzani CUF kilituhumiwa kwamba ndicho kilihusika na uchochezi wa vurugu hizo.Chama hicho kwa upande wake kilikanusha vikali tuhuma hizo. Vyovyote iwavyo lakini lazima tufahamu kwamba kuuzima moto unaotokana na uhasama wa kidini si jambo jepesi kwani hayo ni masuala yanayohusu imani za watu.

Kwa ujumla tunaweza kukubaliana kwamba kuna nyakati uchochezi wa udini unafanywa na watu wa nje na wala huwezi kusema kwamba hiyo ni chokochoko ya wakorofi wachache tu ndani ya nchi.

Matukio ya Bosnia, Serbia, na Poland kwa kiwango kikubwa yalichochewa kutoka nje.Hali kama hiyo imejitokeza hivi karibuni nchini Somalia ambapo kulikuwa na mapambano makali kati ya wanamgambo wa mahakama za kiislamu na majeshi ya Ethiopia.

Upo ushahidi kwamba makundi ya wanamgambo wa mahakanma za kiislamu walielekea kuizidia nguvu serikali ya Somalia kwa sababu walikuwa wanapewa msaada kutoka Irani, ndipo kwa upande mwingine Marekani ilipojitokeza na kutoa zana za kivita ambapo majeshi ya Ethiopia yaliweza kuwasambaratisha wanamgambo wa kiislamu.

Kwa upande wa Poland nchi ambayo Hayati Papa John Paul II alikuwa anatoka hakukubaliana na utawala wa kikomunisti wa serikali ya Jenerali Jaruzeski na hatimaye papa huyo alikiunga mkono chama cha wafanyakazi cha Solidarity kikiongozwa na Lech Walesa ambacho hatimaye kilifanikiwa kuungusha utawala wa kikomunisti nchini humo.

Yote haya yanatufundisha kwamba ushawishi wa dini ni mkubwa sana katika siasa kwa hiyo viongozi wa dini wanatakiwa kuwa makini katika uendeshaji wa mambo yao ili isifikie mahali wao ndiyo wakawa vyanzo vya machafuko kama ilivyokuwa kwa Sudani, Chechnya, Afghanstan n.k.

Miaka ya nyuma kiongozi wa Italia Benito Mussolini aliona umuhimu wa kufanya maelewano na viongozi wa Kanisa Katoliki na baadaye walisaini mkataba wa maelewano (The Lateran Treaty , 1929)ambao hatimaye uliitambua Vatican kama mamlaka kamili ndani ya Italia. Huo ni mfano tosha wa jinsi ambavyo serikali zinatakiwa kushughulikia masuala ya dini kulingana na mazingira halisi.

Mvutano uliopo sasa kimataifa ni kile kinachoitwa ubeberu wa kimarekani kupitia katika utandawazi. Haishangazi kwamba Waislamu wa Nigeria walipinga mashindano ya urembo yasifanyikie nchini mwao na badala yake yalihamishiwa Sanya nchini China.

Yote hiyo ni katika kuonyesha kwamba pande hizo mbili zimeshindwa kufikia muafaka (dialogue) kuhusuana na tofauti zilizopo ambazo zinaweza kupata ufumbuzi na kuondoa mivutano isiyo na tija.

Kwa upande wa nchi za magharibi nazo hazijachoka kutoa nafasi kwa wakosoaji wa Uislamu kama vile mwanamama Ayaan Hirsi Ali mkimbizi kutoka Somalia ambaye ameishi nchini Uholanzi kuanzia mwaka 1992 akipinga ndoa ya lazima aliyopangiwa nchini mwake.

Kwa sasa mwanamke huyo anaandika mengi ambayo anayaona ni ukandamizaji wa dhahiri wa mwanamke unaofanywa na dini ya kiislamu, mama huyo kwa sasa ni mbunge nchini Uholanzi. Wapo wengine wanaomuunga mkono kama vile Naghem Khadhim wa Iraq na Homa Arjomand wa Irani.

Kwa hapa Tanzania mvutano uliopo si kwamba ni wa Waislamu na Wakristu pekee lakini hata Wasabato ambao mara kadhaa wamekuwa wakilalalamika kwamba siku yao haiheshimiwi, labda tatizo lililo dhahiri hapo ni kwamba ipo siku hata Waislamu watadai kwamba Ijumaa iwe siku ya mapumziko kama ilivyo kwa Jumamaosi na Jumapili sijui mwisho wa yote hayo utakuwa ni upi.

Kwa hakika tunahitaji kukaa na kufanya maelewano ya kidini ili kupunguza mizozo isiyo na manufaa vinginevyo tutafikia mahali pa kuanzisha vikundi vya kuziondoa dini za kigeni (nihilistic movements), hapo ndipo tutakuwa tumefikia mwisho wa amani yetu. Chonde chonde Watanzania tusifikie huko!

Lakini kwa Mihangwa kama ameamua kurudi alikotoka na tumtakie safari njema, wasalimie Mlungu na Kubeh!

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 826 272, na Barua pepe: mhegeraelias@yahoo.com





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni