Jumamosi, 19 Julai 2014

WAHISANI WASIBEZWE TUONDOE UFISADI!


Mtanzania Jumapili Novemba 18, 2007 
Na Elias Mhegera
Rais Barack Obama wa Marekani, taifa moja miongoni mwa wafadhili wakubwa Tanzania 


Hivi karibuni serikali kupitia kwa waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe iliwakumbusha (onya?) mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kwamba hawatakiwi kuingilia mambo ya ndani ya nchi kama inavyotakiwa katika makubaliano ya kidiplomasia ya Vienna (Vienna Covention).

Msingi wa hoja hiyo ulitokana na shinimkizo la mabalozi kuitaka serikali itoe tamko kuhusiana na tuhuma za ufisadi zinaoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wake. Makala haya yanatathmini uhalali wa mabablozi kutoa tamko lao.

Sote tunafahamu kwamba mabalozi wawapo katika nchi wanakowakilisha (receiving countries), hujitahidi kujifunza tamaduni, taratibu na kanuni za uendeshaji wa nchi hizo. Lengo la kufanya hivyo ni kuzuia uwezekano wa kugongana kidiplomasia na nchi wenyeji wao na hivyo hujaribu kulinda uhusiano uliopo badala ya kuudhofisha kwa namna yoyote ile.

Hata hivyo si kila wakati wana diplomasia wamekuwa wakimya wanapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo katika nchi wenyeji wao, na ndipo hulazimika kutoa tamko lao kuonyesha kutoridhishwa na mwenendo au mienendo ya nchi iliyowapokea. Kelele za kudai mabalozi na wahisani wasiingilie mambo ya ndani ya nchi hazijaanza leo. Mwaka 1994 nchi wahisani zilimshauri Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mzee Ali Hassani Mwinyi kumuwajibisha waziri wa fedha kwa wakati ule Hayati Profesa Kighoma Malima.

Mara Mzee Mwinyi na waziri wa mambo ya nje kwa wakati ule Hayati Hassan Diria hawakuchelewa kuwakumbusha wahisani kwamba walikuwa wanaingilia mambo ya ndani ya nchi. Wahisani hawakuchoka na kelele zao na ndipo hatimaye Profesa Malima alijiuzulu.
Rais wetu wa sasa Jakaya kikwete atakuwa na kumbukumbu nzuri sana ya dhahama hiyo kwani yeye ndiye alimrithi Malima katika nafasi ya waziri wa fedha. Kwa hiyo kelele za sasa za wahisani ni ishara kubwa kwake kwamba mambo si shwari tena lazima afanye njia ya kuisafisha serikali yake.

Tayari wawakilishi watatu wamekwisha iomba serikali kutoa tamko kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Kwa upande wake pia serikali imetoa ahadi ya kufuatilia tuhuma hizo na kwamba kama itathibitika kwamba tuhuma hizo zina ukweli basi hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote.

Tayari msemaji wa umoja wa nchi za Jumuia ya Ulaya (EU) ameiomba serikali kutoa tamko, mwingine aliyetoa tamko la namna ile ni balozi wa Marekani nchini Mark Green pia mwakilishi wa wahisani David Stanton wote hao wameishauri serikali kujitakasa mbele ya umma.

Ukiachana na hao bado kuna kelele za vyombo vya habari, na viongozi wengine wa kijamii kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku na viongozi wa dini kama vile kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Tanzania Askofu Alex Malasusa naye ameiomba serikali kufuatilia na kutoa taarifa za uhakika kulingana na tuhuma zinazoelekezwa kwa baadhi ya viongozi wake.

Pamoja na tamko la Waziri Membe bado nchi wahisani zitaendelea kuwa na dukuduku juu ya tuhuma hususani hizi zilizotolewa hivi karibuni na Dkt. Wilbroad Slaa Mbunge wa Karatu, tuhuma zinazohusu ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu, na tuhuma kadhaaa kuhusiana na mikataba tata ukiwamo ule wa Buzwagi ambao ulishupaliwa sana na mbunge Zitto Kabwe kutoka chama cha upinzani (CHADEMA).

Ni imani yangu kwamba wapo wengi watakao niunga mkono kwamba wahisani au hata kwa jina lolote tutakaloamua kuwaita yaani wafadhili au washirika katika maendeleo wana haki ya kufuatilia matumizi ya misaada yao ambayo hutokana na walipa kodi wao katika nchi husika. Ni dhahiri kwamba wahisani hufarijika pale wanapoona misaada yao imetumiwa vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na wala si vinginevyo.

Kwa mfano tarehe 15 Januari mwaka huu serikali ya Uingereza ilitangaza azma yake ya kuipatia Tanzania Pauni za Uingereza milioni 105 (sawa na shilingi bilioni 262) ikiwa ni mchango wake kwa bajeti ya serikali ya Tanzania mwaka wa fedha 2007/8.

Kwa maana hiyo baada ya kuwa wametimiza ahadi hiyo hatua inayofuata ni kuangalia kama kweli pesa hizo zimetumika kwa mambo yenye tija kwa wananchi wote badala ya kuwanufaisha wajanja wachache.

Wahisani ni watu ambao wanatakiwa wasikilizwe pale wanapotoa ushauri ili waweze kuendelea kutuunga mkono na hasa katika maeneo ambayo yanaelekea kusahaulika kama vile kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu.Kama tungeendelea kuwatumia vizuri wahisani leo tungekuwa tunafikiria masuala ya kupata matrekta kwa ajili ya kuyapeleka vijijin na pembejeo nyingine ili kuendeleza kilimo.

Kinyume chake serikali yetu imejiingiza katika mfumo wa kuagiza vitu vya kifahari kama magari aina ya mashangingi na kutokana na kushindwa kuinua kilimo ndiyo maana tunaona vijana wote sasa wanakimbilia mijini kwa sababu huko vijijini hakuna mvuto kumesahaulika kabisa.Vijana wanayo haki ya kukikimbia kilimo kilichopitwa na wakati kwa sababu kilimo cha jembe la mkono hakijajengewa mazingira mazuri na hicho ndicho chanzo kingine cha kuongezeka kwa uovu katika jamii kama vile biashara haramu ya ukahaba na unyan’ganyi.

Ni sera mbovu au sera ambazo zinabakia katika nadharia bila utekelezaji ambazo zinasababaisha vijana kuyakatia tamaa maisha ya vijijini na kuamua kukimbilia mijini ambako hata hivyo pia hawakubaliki. Na pia wanakutana na mazingira magumu zaidi.

Kama serikali imeshindwa kuviendeleza vijiji basi inastahili kuzitumia pesa za wafadhili katika kutoa mikopo kwa vijana waliopo mijini ili wawe wajasiriamali na kuhalalisha maisha yao badala ya kubakia wakifukuzana na askari mgambo mjini wakiwazuia kufanya biashara zao za umachinga.

Ni dhahiri serikali inapoomba misaada nje hutaja maeneo mbalimbali ikiwemo kuwasaidia akina mama, vijana na, makundi mengine katika jamii lakini inapofika katika utekelezaji hapo ndipo penye tatizo.Kwa mfano hali ingekuwaje kama vijana wote waliomaliza kidato cha nne au hata darasa la saba wangepatiwa elimu ya ufundi stadi na baadaye wakawezeshwa kujiajiri? Ni dhahiri tatizo la wamachinga lingekuwa limepata ufumbuzi wa kudumu.

Nashangazwa na kauli kali ya serikali kama vile ombi la wahisani dhidi ya serikali ni sawa na ujasusi (espionage) kumbe viongozi wetu wanapenda kusifiwa tu na kupambwa lakini hawataki kabisa kukosolewa au hata kuambiwa ukweli?Tatizo letu ni kule kujisahau kwamba tuna uchumi tegemezi kwa hiyo wahisani wanahaki ya kufuatilia misaada yao ili kuhakikisha kwamba imetumiwa kikamilifu kama ilivyokusudiwa.

Lakini kwa upande mwingine tusisahau pia kwamba wahisani haohao wanazo taarifa nyingi zinazotuhusu kwa sababu katika dunia ya utandawazi tuliyonayo mataifa ya dunia ya tatu kama Tanzania ndiyo yanaathirika zaidi kwamba hayana tena uwezo wa kudhibiti taarifa zao hata zile amabazo yanaziona kwamba ni nyeti.

Ninachomaanisha hapa ni kwamba tusije tukadhani kwamba nchi wahisani wamezipata taarifa za ufisadi kutoka magazetini tu bali magazeti yetu yamekuwa nikichocheo tu cha wao kutamka kwamba wanaona ni jambao jema serikali ikajitakasa ili kurudisha imani ya wananchi na wadau wengine.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu Ibara ya 18 inawapa ruhusa Watanzania kutoa maoni yao na kujieleza bila ya vipingamizi ili mradi hawavunji sheria. Pamoja na hayo sheria ya magazeti ya mwaka 1976 inaziruhusu mamlaka husika ikiwa ni pamoja na rais wa nchi kuzuia uchapishaji wa magazeti au machapisho ambayo yanakwenda kinyume na maslahi ya taifa.

Mpaka sasa hakuna yeyote kati ya waliotuhumiwa kwa ufisadi ambaye ameishachukua hatua za kisheria kama vile kuwashitaki waliomtuhumu au hata magazeti yanayochapisha tuhuma hizo. Hali hiyo inaashiria kwamba tuhuma zilizotolewa dhidi ya wahusika inawezekana zikawa na ukweli na ndiyo maana wanasita kuchukua hatua dhidi ya waliowatuhumu.kwani wanahofu ya kuumbuliwa mahakamani.

Ukiachana na suala la vyombo vya habari ni vyema tufahamu pia kwamba wahisani wanafahamu fika matatizo ya nchi za dunia ya tatu kama Tanzania kwani wengine tayari huwa wameyasomea katika vyuo nchini mwao kabla ya kuja kufanya kazi barani Afrika.

Wakati mwingine wanao uzoefu kutoka katika nchi nyingine kwani si kwamba Tanzania ndiyo nchi ya kwanza kuitumikia barani Afrika bali mara nyingi wengi huwa wameishazunguka katika nchi kadhaa barani humu hivyo wanao uzoefu wa kutosha juu ya uendeshaji wa mambo katika nchi zetu.

Kwa hakika wahisani hawawezi kupiga kelele kama wanaona serikali inajitahidi kujenga miundo mbinu bora kama ilvyokusudiwa wakati wa kuomba misaada yetu.hawawezi kupiga kelele kama wanaona nchi yetu inajenga hospitali shule na inawajibika katika kuendeleza taasisi za kimaendeleo.

Lakini wahisani wanakerwa wanapoona misururu mikubwa ya viongozi wetu katika ziara zao, au wanapoona tuna matumizi makubwa kuliko uwezo wetu kiuchumi kwa mfano ununuzi wa magari ya kifahari ya serikali, au pale wanaposhuhudia viongozi wetu wanashiriki katika kugombea raslimali za taifa kama vile ununuzi wa nyumba za serikali umiliki wa migodi na ardhi kubwa bila kuangalia uhalisia wa mambo nchini.

Wahisani wanafahamu fika kwamba viongozi wetu wamewekeza mitaji yao kwa wafanya biashara wakubwa, pia wanafahamu kwamba baadhi ya miradi inayoanzishwa na serikali haina tija kwa watu wa kawaida isipokuwa inaanzishwa kwa malengo ya kuwanufaisha wajanja wachache wenye nafasi kubwa kiuchumi.

Wahisani wanafahamu kwamba kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini kumechangia katika kuleta matabaka, kwani uchumi wa soko huria umewapa uhalali wenye nacho kuumilik uchumi, na kupandisha bei za bidhaa mbalimbali bila kuwakumbuka wanyonge.

Ni ukweli usiopingika kwamba mabadiliko ya kiuchumi ambayo yametoa mwanya kwa wawekezaji kutoka nje kuwekeza vitega uchumi vyao nchini Tanzania na hivyo kuweza kuingia ubia na wawekezaji kutoka nje katika biashara mbalimbali kama vile sekta ya utalii, mahoteli, makampuni ya simu za mikononi n.k.yametoa uhalali kwa wachache walionacho na kuwabagua wanyonge.

Ni jambo la kusikitisha kwamba viongozi wetu hujenga mazingira mazuri ya kuwalinda wawekekezaji na miradi yao kwa sababu wao pia ni wabia katika makampuni hayo ambayo kimsingi baadhi ya makampuni hayo hayatoi mchango wa maana nchini mwetu bali yanachangia katika kuhamisha raslimali fedha (cash outflow).

Ni nadharia hii inayowavuta baadhi ya matajiri katika siasa za Tanzania kwa sababu hali haikuwa hivyo enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere. Kwa lugha nyingine kwa sasa kwa tajiri kuwa mwanasiasa ni njia mojawapo ya kulinda mali zake. Haishangazi kwamba baadhi ya makampuni yanayohusishwa na wanasiasa wetu huanguka ghafla pale wanapostaafu au kupoteza nyadhifa zao serikalini.

Leo mashindano makubwa yapo katika kujipenyeza katika himaya ya kisiasa (hegemony), kwani mara baada ya kupata nafasi hiyo, inakuwa rahisi zaidi kufanikisha upatiakanaji wa leseni za biashara, mikataba yenye utatata na ujumbe katika bodi za mashirika mbalimbali na taasisi za umma.

Ujanja unaotumika ni uhalalishaji wa utawala kwa njia ya kuwashirikisha baadhi ya wananchi wa kawaida, kwa mfano wafanyakazi, wakulima n.k. ili kulinda maslahi yao yaliyofichika, kwa mfano baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu leo wanagombea ujumbe wa halmashauri kuu ya chama tawala lakini watu hao hao wamo katika bodi nyingi na tume mbalimbali.

Siasa za leo siyo sawa na zile za zamani zilizotokana na dhamira ya dhati ya utumishi bali siasa za leo zimekuwa ni biashara, ni mtaji, ni njia nyepesi ya kujitajirisha kwa wachache na kuwabagua walio wengi na hasa wale wanaojaribu kuipinga mifumo tawala.hali siyo tofauti hapa Tanzania

Katika mchanganuo wa tathmini ya maendeleo wa USAID nchini Tanzania, mwaka 2005-2014 (2004), taarifa inasema mabadiliko yaliyoanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, yameleta mabadiliko madogo kimuundo ambayo hata vile yamejenga mazingira ya kisiasa na kisheria kwa manufaa ya chama kilichopo madarakani hususani katika kuendeleza umiliki wa uchumi.

Hali ya sasa imeigeuza siasa kuwa biashara sawa na biashara nyinginezo. Wanasiasa ni watu wenye nguvu, utajiri, na wanao uwezo wa kujipatia mahitaji ya lazima kwa njia nyepesi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote yule.Taarifa ya UNDP kuhusiana na maendeleo mwaka 2005 zinaonyesha kwamba Tanzania bado haijachukua hatua madhubuti dhidi ya ufisadi licha ya kutoa taarifa mbalimbali kwamba imo mbioni kufanya hivyo.

Taarifa hiyo inasema Tanzania imebahatika kuwa na amani na utulivu ambao ni kivutio kikubwa kwa wawekezaji lakini kikwazo kikubwa ni rushwa ambayo imechangia kuteremka kwa thamani ya pesa yetu mara kwa mara na hivyo wawekezaji wanahofu ya kupata hasara iwapo watawekeza katika mazingira yasiyo na uhakika wa faida kwa miradi yao

Kwa upande mwingine taarifa hiyo inaonyesha udhaifu mkubwa wa vyombo vya dola katika kutimiza wajibu wao, hofu hiyo inatokana na uwezo mdogo wa wataalamu au uhaba wao, japo wanao uwezo na taaluma za kuosha. Ni katika mazingira hayo ndipo watafiti wanahisi kwamba rushwa inatumika katika kuzima utendaji wa baadhi ya vyombo vya dola.

Kwa mfano mahakama zetu zinonyesha kwamba zimezidiwa na mzigo wa kesi zisizosikilizwa na wakati mwingine rushwa inachangia katika utendaji duni wa mahakama zetu. Kwa upande mwingine taarifa hiyo inaonyesha kwamba hadi mwezi Juni 2004, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ilikuwa imepokea taarifa10,319 za tuhuma mbali mbali za rushwa lakini ni kesi 357 tu ndizo zilikuwa zimesikilizwa na zote hizo zilizosikilizwa zilikuwa zinawahusu watu wa kada ya chini katika utumishi wa umma.

Inakuwaje kila siku kuna tuhuma zinazowahusu viongozi wakubwa wa kisiasa lakini hawachukuliwi hatua? Jibu ni dhahiri kwamba siasa imekuwa kitega uchumi wanasiasa ni matajiri wasioguswa. Hata katika harakati za kugombea uongozi si kwamba wananchi ndiyo wanowatuma wanasiasa wawakilishe, bali wanasiasa wanatumia pesa zao kuwashawishi wananchi wawapigie kura, ili wawahalalishe katika madaraka, uwezo huo wanaupata kwa sababu ya pesa zao na lugha tamu wanazotumia wakati wa kutafuta uongozi.

Ni mazingira hayo ambayo yametujengea siasa za upambe, baadhi ya wajanja ambao wamefanikiwa kujipenyeza ndani ya mfumo wanajifanya wanakipenda chama tawala lakini ukweli wa mambo ni kwamba tukiwachunguza kwa undani baadhi yao hawana hata chembe ya itikadi ya chama alichokiasisi Mwalimu Nyerere bali wana itikadi ya kujitafutia chao tena mahali popote penye urahisi wa kufanya hivyo. Kwa hiyo kwa sasa wamo ndani ya CCM kwa sababu hiyo tu (opportunists).

Katika kitabu chao ‘Africa Works’ (1999), waandishi Patrick Chabal na Jean- Paschal Daloz wanajenga hoja kwamba siasa za utajirisho ndizo zimechangia katika kuwapo kwa madikteta barani Afrika kama vile Hayati Bokassa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye aliugeuza uteuzi wa uongozi kuwa mradi wa kuwanufaisha ndugu na rafiki zake wa karibu na hivyo ndiyo maana alikaa madarakani kwa muda mrefu kwa sababu wanufaika walimlinda.

Waandishi hao pia wanazungumzia tabia ya baadhi ya wanasiasa kuzigeuza taasisi za umma kama vile ni mali zao binfisi. Katika hilo wanamzungumzia Frederick Chiluba ambaye wakati wa utawala wake alimfukuza kazi mkurugenzi wa wa televisheni ya taifa baada ya mkurugenzi huyo kulalamika kwamba televishenu hiyo ilikuwa inatumia muda mrefu kwa kutangaza vipindi vya ‘walokole’ madhehebu ambayo Chiluba ni mfuasi wake.

Nakubaliana kwa kiwango kikubwa kwamba uanzishaji wa asasi za kiraia wakati mwingine umekuwa hauwalengi watu wa kawaida bali wanufaika ni watu wa mijini  ambao asasi hizo ndiko zimejikita zaidi huku viongozi wake wakiwa na kila aina ya ukwasi, magari mazuri, malipo kutoka kwa wahisani n.k.

Ujanja ujanja ndiyo imekuwa uendeshaji wa mambo katika nchi zetu kwani hata viongozi wetu hawataki kuachia madaraka. Kuna ukweli usiopingika kwamba kipo kizazi kinaelekea kurukwa kutokana na baadhi ya viongozi kung’ang’ania madaraka matokeo yake ni kwamba wasomi wetu wameamua kutafuta mbinu nyingine za kufaidi ‘matunda ya uhuru’.

Upo utani kwamba kizazi hicho ng’ang’anizi (rigid), kimekula matunda, majani na sasa kinamalizia kula mizizi ya uhuru na hivyo kuna hatari ya vizazi vijavyo kukosa urithi kutokana na kila raslimali zetu kuhamishwa na wenye mamlaka kwa sasa.

Tusipozingatia angalisho au tahadhari tunazopewa na wataalamu wetu, wahisani, viongozi wa dini tunataka tumsikilize nani? Vinginevyo tunataka tuache matabaka yakomeae na baadaye tuingie katika machafuko kama yale ya Sierra Leone, Liberia, au DRC ambapo katika machafuko hayo baadhi wanasiasa wanajinufaisha kwa kuendeleza biashara haramu kama vile kuiba madini, kuuza silaha kwa njia za magendo, uvushaji wa madawa ya kulevya hali ambayo imewaathiri kwa kiwango kikubwa wanyonge wasio na hatia.

Bila kuwakemea viongozi wetu wanaweza kujisashau na kudhani kwamba wao ndio pekee wenye hatimiliki ya majimbo au himaya zao za kisiasa. Kwa lugha nyingine viongozi wetu wanaweza kujenga ukuta kati ya wananchi na wahisani ili wananchi wasifahamu serikali inapokea kiasi gani cha msaada kutoka nje lengo likiwa ni kujitafutia sifa kwamba wanatimiza wajibu wao wakati hali halisi ni tofauti.

Ni katika mazingira ya kujisahau ndipo viongozi kama vile Felix Houphet Boigny wa Ivory Coast aliweza kujenga kanisa mfano wa Basilica la mjini Rome nchini Italia. 

Kwa upande mwingine Mobutu Seseko yeye alijenga uwanja wa ndege ambao unaiwezesha ndege aina ya Concorde kutua kijijini kwake.Yote hayo ni matatizo ya kulewa madaraka kutokana na kukosa nguvu kubwa ya ukosoaji. Kwa hiyo ukemeaji, ukosoaji na mambo ya aina hiyo yanastahili kuangaliwa katika mtazamo chanya badala ya kuonekana kwamba viongozi waliopo wanaonewa wivu au wanabughudhiwa na watu wasiohusika.


Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 826 272, na barua pepe mhegeraelias@yahoo.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni