Ijumaa, 18 Julai 2014

RUSHWA KATIKA CHAGUZI ZA TANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) 


JE NI MFUPA ULIOMSHINDA FISI? (SERIKALI) 

Septemba 22, 2007 Mtanzania Jumapili

Na Elias Mhegera

Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi CCM, kiliendesha zoezi la chaguzi mbalimbali za ndani, katika zoezi ambalo baadhi ya viongozi na wagombea walituhumiwa kwa kutoa hongo na hivyo kuvunja imani za wanachama waadilifu.

Makala hii inachambua tatizo la rushwa katika ujumla wake kama tatizo la kijamii na ambavyo linagusa nyanja nyingi za maisha, na athari zake za muda mrefu.

Miaka kadhaa nyuma na hasa katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere siasa za Tanzania hazikuwavutia sana matajiri wakubwa, kwa kusema hivyo sina maana kwamba ni kosa kwa tajiri kuwa mwanasiasa.

Ninachokusudia kusema ni kwamba siasa za leo zimetawaliwa sana na mambo ya pesa na hivyo zinawakwaza watu wasiokuwa na uwezo mkubwa kipesa.

Tatizo ni kwamba kutokana na baadhi ya watu wasio waadilifu kupenda kujiingiza katika siasa sasa baadhi ya wanajamii wameamua kujinufaisha kwa kudai hongo nyakati za chaguzi bila kujali athari za muda mrefu za mtindo huu.

Kimsingi ni kwamba tunapokuwa na wanasiasa wengi waliotumia rushwa katika uchaguzi tunajenga mazingira magumu ya kuondokana na rushwa katika utawala wa wanasiasa hao.

Rushwa ikitawala katika jamii madhara yake ni kwamba itaibuka jamii isiyo na usawa, ufisadi unaweza kuchochea hata vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyokuwa kwa nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.

Mara nyingi matatizo ya aina hiyo hupikwa kwa muda mrefu kabla hayajalipuka na kusababaisha madhara makubwa.

Uadilifu katika uongozi unapopotea ndipo watu mbalimbali hujaribu kuitumia siasa kama kitega uchumi lengo likiwa ni kupata madaraka ili kujichumia mali ya umma.

Kwa maana hiyo maadili yote yahusuyo uongozi huwekwa kando, lengo la viongozi hubadilika kutoka kwenye kuwatumikia watu na kuwa kujinufaisha kwanza mtu binafsi na ndipo uongozi unapogombaniwa kwa mbinu zote ikiwamo rushwa.

Hali inakuwa mbaya zaidi kwenye nchi zenye demokrasia changa kama Tanzania kwani siasa za ushindani wa vyama zinatazamwa katika misingi ya uadui badala ya watu kuona kwamba ushindani ni sehemu ya mchezo wa siasa.

Mwaka 1992 serikali ya Tanzania iliruhusu rasmi kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi na kwa mara ya kwanza uchaguzi uliofuatia wa mwaka 1995, ukavihusisha vyama vingi.

Kwa bahati mbaya tokea wakati huo vyama vya upinzani vinazidi kudorora na hivyo chama tawala kimekosa mkosoaji wa dhati.

Hali hiyo pia imeendana na lindi la wapinzani maarufu kurejea katika chama tawala, CCM. Kwa mifano michache ni Dkt. Masumbuko Lamwai aliyekuwa tishio kipindi alipokuwa katika chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi, leo hasikiki tena wengine ni Richard Hiza Tambwe, Dkt Festus Limbu, Dkt Walid Kaborou, n.k.

Wote hao wamerejea katika CCM ambako wanaendelea kupwaya wakati huo huo wakiiacha kambi ya upinzani ikiwa hoi bin taabani.

Uamuzi wa mtu kurejea katika chama tawala ni wa mtu binafsi bila kujali kama ameshawishiwa na mtu kufanya hivyo lakini jambo lenye manufaa zaidi ni kuangalia nini hatma ya siasa za Tanzania kama kila mwenye nguvu atamezwa ndani ya CCM (co-optation).

Ni kwamba kwa hali yoyote ile chama tawala kinahitaji mkosoaji ili kiweze kufanya kazi zake kwa uwazi na umakini zaidi. Kazi hiyo inatakiwa ifanywe na vyama vya upinzani, asasi za kiraia, vyombo vya habari, taasisi za elimu ya juu, madhehebu mbalimbali ya dini, na wachambuzi wa masula ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani na nje ya nchi.

Ndiyo maana kabla ya kuangalia rushwa katika jamii inabidi tuangalie kwanza rushwa inavyotumika katika uchaguzi kwani hapo inawagusa watunga sheria za nchi kama vile wabunge na wawakilishi wengine.

Makundi ya wawakilishi ndiyo yanawagusa watanzania wote katika ujumla wao na ndipo inabidi tujiulize maswali kama tutakuwa na viongozi watoaji au wapokeaji wa rushwa watawezaje kutetea maslahi ya wengi katika nchi?

Siku moja nilibahatika kutoa mada kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, mada yenyewe ilihusiana na maendeleo ya kisiasa tokea kupatikana kwa uhuru hadi awamu ya tatu ya Rais Mstaafu Benjamini Mkapa.

Nilizungumza mengi katika mada ile lakini sikuona kama inapokelewa kwa msisimko niliotarajia. Hata hivyo baada ya mada yangu kulikuwa na mapumziko mafupi na ndipo nilipoona wasikilizaji wangu wakinifuata mmoja baada ya mwingine kwa hakika kila mmoja alitaka kuondoa dukuduku lake kuhusiana na kile nilichokisema ukumbini.

Kwa hakika wengi walikubaliana na maudhui ya mada yangu lakini walishindwa kuchangia kutokana na migongano ya kimaslahi.

Japo mimi niliamini kwamba mwanachuo wa chuo kikuu chochote nchini anaweza kuwa mchambuzi makini wa masuala yanayoihusu jamii yake lakini kwa upande wa chuo hicho jambo hilo linakuwa gumu kwani takribani watu wote wanakuwa katika ajira za serikali au wanakuwa ni wafanyabiashara binafsi.

Mambo yote hayo yanawatia woga wasomi hao kuchangia hoja yoyote ya kitaaluma au hata kuwa na hofu ya kuhatarisha ajira zao serikalini.
Ni imani yangu kwamba hali kama hiyo haiwezi kujitokeza katika vyuo vyenye wanafunzi wanaotokea shuleni moja kwa moja (direct entrants), kwa hiyo woga wa wasomi huo una jambo la msingi ndani yake.

Lakini ukweli ni kwamba wahusika walinifuata nje ya ukumbi na kila moja akaunga mkono mada yangu ni jambo lililonipa faraja kwamba ujumbe wangu uliwafikia walengwa.

 Kwa maana hiyo tunaweza kusema wapo watanzania wengi wanaoichukia rushwa katika sura zake zote lakini bado hawajajengewa mazingira mazuri ya kuikemea hadharani

Kwa hiyo jambo lililodhahiri ni kwamba tunakosa ujasiri japo tunaichukia rushwa mahali popote inapotumika kwani inatunyima haki zetu za kimsingi iwe ni mahakamani au katika jeshi la polisi. Kwa hiyo makala hii italenga katika kutoa ushawishi wa kujenga ujasiri wa kuikemea rushwa mahali popote ilipo.

Ni lazima tukubaliane kwamba siku zote maisha yetu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili: ushujaa (heroism) na uovu (villainy). Kwa hakika ni lazima wawepo mashujaa wanaokemea uovu ili jamii iweze kwenda katika mstari ulionyooka na katika dira inayostahili.

Kwa bahati mbaya ushujaa ninaouzungumzia hapa huwagharimu sana wale wanaojaribu kukemea, Kwani wote hao huonekana kana kwamba ni wanafiki, mabaradhuri na hivyo hutengwa na jamii zao mara moja.

Lakini kwa upande mwingine ni dhahiri kwamba yeyote yule aliyeamua kupingana na uovu basi ni lazima ajiandae kwa adhabu inayotokana na azma yake hiyo.

Siku zote watu ambao wanajaribu kuirudisha jamii katika dira sahihi huonekana kwamba wemekanganyikiwa (social rejects).Hii inatokana na ukweli kwamba watu wa namna hii huonekana kwa wenzao kama kero kutokana na azma yao ya kuwaondolea raha waliyoizoea.

Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza kwamba katika azma ya kuondoa ufisadi na uovu mwingineo katika jamii inabidi viongozi wa dini wahusike kikamilifu Kwani imani ya dini inaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa madhara yatokanayo na ufisadi kama si kuyaondoa kabisa.

Kwa mfano katika imani za kikristu tunaamini kwamba Bwana Yesu Kristu aliibadilisha alama ya msalaba kutoka kwenye alama ya kuulia wahalifu na kuigeuza kuwa alama ya ushindi ndiyo maana wakristu hupendela kuvaa misalaba kuashiria ushindi huo.

Leo watu wengi wanavaa ishara hiyo ya ushindi ya msalaba wakiwa wamesahau kwamba ushindi huo uliambatana na kumwagika kwa damu ya Bwana Yesu Kristu. Hivyo basi ni muhimu kufahamu kwamba ushindi wa muda mrefu wa jambo lolote uanahitaji kujitoa mhanga.

Kwa hiyo wale wote wanaopigania kuondoa ufisadi katika jamii na kuyatetea maadili mema katika jamii kwa ujumla wawe tayari kusutwa, kuzongwa zongwa.misukosuko ya kila aina na wakati mwingine hata kuuawa lakini mara yanapojitokeza hayo iwe ni faraja kwamba ujumbe wetu umewafikia walengwa.

Kwa mfano mbunge aliyeshinda kwa kutoa hongo anakuwa amejijengea mazingira mazuri ya yeye mwenyewe kupokea hongo kwani tayari anakuwa amekiuka maadili na kujijengea mazingira mabaya kiroho. Mbunge huyo anaweza akapewa hongo ili aipitishe bajeti fisadi kwa asilimia mia moja.

Ukweli wa jambo hilo ni kwamba ni lazima mtu yeyote ajuilize ni kwa nini amuhonge mtu anayetaka kumtumikia vinginevyo huyo mgombea ndiye anastahili kupewa zawadi na wanajamii kwa kuamua kuwatumikia.

Labda wapo wanaoweza kujiuliza maswali mengi kwamba bajeti fisadi ni ipi hiyo? Katika kujibu hilo mwandishi Jorge Martinez-Vazguez katika chapicho lake Corruption, Fiscal Policy, and Fiscal Management anasema miaka kadhaa nyuma wataalamu mbalimbali walikwepa kuizungumzia rushwa na ufisadi kwa sababu waliona ni mfumo wa kawaida (inherent) uliomo katika mifumo yote ya kisiasa.

Lakini siku hizi hali imebadilika kwa sababu wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wamegundua kwamba rushwa ndiyo kikwazo cha maendeleo popote ulimwenguni na ndiyo maana wanapigania kwa nguvu zote kuwa na utawala bora ambao utaondokana na ufisadi kwanza ndipo mambo mengine yafuate.

Maelezo wanayotoa ni kwamba kunapokuwa na ufisadi utendaji unakuwa legelege kwa mfano waziri atajihusisha na mikataba hewa, wabunge watashindwa kumkosoa, polisi watashindwa kumkamata, na hata wakimkamata atatoa hongo na kushinda mahakamani kwa hiyo mzunguko huo wa uovu ndiyo chanzo cha ulegelege wa serikali.

Athari za muda mrefu za mzunguko huo wa uovu ni kuwavunja moyo wafadhili kwa sababu hawaoni manufaa ya kuendelea kuzifadhili serikali zetu baada ya kujua kwamba misaada haiwafikii walengwa (walalahoi) bali wajanja wachache.
  
Na kwa bahati mbaya hali inapofikia hapo kila chombo kinakuwa kimeathirika vikiwemo vyombo vya habari, asasi za kiraia na hata wasomi ambao humezwa katika mfumo huo fisadi. Kwa hiyo katika mazingira ya aina hii, si jambo la ajabu kuona kwamba Bunge linapitisha bajeti fisadi.

Ni kwamba viongozi wakuu wa nchi wakianza kujihusisha na ufisadi basi hata taakwimu mbalimbali zinaweza kupikwa ili kukidhi matakwa yao. Katika mazingira ya aina hiyo maadili katika jamii hushuka kwa kiwangio kikubwa watu huanza kuhama ovyo kutafuta namna ya kujikimu.

Katika uhamaji huo usioratibiwa uhalifu wa kila aina unaweza kujitokeza kwa mfano: ugaidi, matumizi ya madawa ya kulevya na hata ongozeko la ugonjwa hatari wa UKIMWI.

Katika mantiki hiyo ni lazima tufahamu kwamba kabla ya kuanzisha vita dhidi ya ufisadi ni lazima kwanza tuwaelimishe watu wetu kwamba tunastahili kuichukia rushwa badala ya kuikumbatia, tuwaelimishe wafanyakazi kwamba mishahara yao ni midogo kwa sababu watu wanakwepa kulipa kodi zinazostahili.

Ni lazima tuwafahamishe watu kwamba rushwa ndiyo inakwamisha maendeleo yao, kwamba kila mmoja anatakiwa atoe mchango wake katika kupambana na rushwa. Kwamba jukumu la serikali ni kusimamia au kuratibu zoezi la kupambana na rushwa lakini ni jukumu la kila mwananchi kuisadia serikali katika mapambano hayo.

Vita dhidi ya rushwa ni vita vitakatifu kwa hiyo kila mmoja anastahili kuchangia kwa uwezo wake wote kwa sababu ufumbuzi ukipatikana utawanufaisha wote pia.

Kwa hiyo ndiyo maana wananchi wanatakiwa kuitaja mianya yote ya rushwa kwa sababu wanaifahamu, wao ndiyo wanaotakiwa kupigania nidhamu ya matumizi ya pesa za halmashauri zao na raslimali zingine za umma.

Kama kila mwananchi atatoa mchango wake katika hilo basi tutakuwa tumeirahisiha kazi ya Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Kwa ujumla jukumu lao ni uendeshaji (co-ordination) wa shughuli zote zinazoelekezwa katika kupambana na rushwa, lakini wao pekee hawana uwezo wa kuiangamiza rushwa.

Mambo yote hayo yanawezekana iwapo tutajiaminisha kwamba maana ya utumishi wa umma ni kuhudumia watu bila ya kuwabagua, wala kutegemea vipato haramu.Watumishi hao ni lazima wafahamishwe kwamba wao ni watoa huduma na wala si wafanya biashara.

Mkakati mzima wa kuondoa rushwa ni lazima uziainishe kwanza aina zote za rushwa yaani kubwa na ndogo. Kwa mfano mawaziri na wakurugenzi wa makampuni makubwa ya umma wanajinufaisha kutokana na mikataba minono inayosainiwa na serikali au makampuni yao hata kama hawapati malipo ya pesa moja kwa moja.

Hali hiyo ikiachwa ikaendelea kushamiri huleta matabaka makubwa katika jamii ambapo wale wasionufaika na uchumi au mikataba inayosainiwa hukata tamaa na kuanza kuhujumu uchumi katika azma ya kujikimu.

Kwa mfano askari polisi trafiki anajenga nyumba kubwa, anaendesha gari zuri, anaishi kifahari lakini mwalimu na daktari hawawezi kujenga wala kujikimu katika maisha yao ya kila siku ndipo hujitokeza walimu wakafelisha wanafunzi kwa sababu muda mwingi huutumia kutafuta vipindi vya ziada nje ya ofisi zao.

Tukichukulia mifano halisi katika nchi za Kenya na Tanzania tunaona kwamba rushwa imekuwa ikiathiri utendaji wa serikali hizo katika maeneo mengi.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi iitwayo The African Centre for Economic Growth ikihusianisha rushwa na umaskini nchini Kenya kwa mwaka 2000, inaonyesha kwamba rushwa imekuwa kero kubwa nchini humo kwa sababu inawahusisha wanasiasa wakubwa na hasa mawaziri.

Kwa upande mwingine rushwa imeiathiri kwa kiwango kikubwa serikali ya Kenya kwa sababu watendaji wengi wamekuwa wakijichukulia “kidogo dogo” kila mtu kwa wakati wake na nafasi yake.

Jambo hilo limekuwa na athari mbaya kwa sababu ndilo limechangia kuwepo na mfumuko wa bei na kuanguka kwa taasisi za pesa kama vile benki na mamlaka za ukusanyaji kodi.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo rushwa mbaya zaidi nchini Kenya ni ile ambayo inahusu tenda hewa, miradi inayofadhiliwa na serikali, mashirika na wafadhili wengine ambapo pesa hizo huishia mifukoni kwa wajanja wachache.

Kundi jingine linalotajwa na ripoti hiyo linawahusu wasomi ambao kutokana na taaluma zao na ukaribu wao na viongozi mbalimbali serikalini wameweza kujipatia mikataba minono kama vile utoaji wa elimu mbalimbali katika maeneo ya sheria, teknolojia, mazingira, n.k.

Watu hawa hutafuna mamilioni ya pesa na kuwaacha walengwa bila chochote chenye manufaa kwao. Kwa upande wa Tanzania ripoti ya Afrobarometer iliyotolewa an REPOA April 2006, inasema rushwa imejikita katika maeneo mbalimbali na imeathiri kwa kiwango kikubwa maeneo muhimu ya kiuchumi.

Ripoti hiyo inasema rushwa imeendelea kuwepo nchini Tanzania kwa sababu bado watu hawajaelimishwa vya kutosha juu ya athari za rushwa na kwa upande mwingine nchi haijajiweka tayari kwa ajili ya kuondokana na rushwa hiyo.

Kukosekana kwa uwazi, uwajibikaji na utawala bora vimechangia kwa kiwango kikubwa katika kuenea kwa rushwa nchini Tanzania. Kwa maana hiyo rushwa imekuwepo katika maeneo mabalimbali kama vile serikali za mitaa jeshi la polisi, mamlaka ya kodi, mahakamani, n.k.

NINI BASI KIFANYIKE?

Rushwa inaweza kusambaratishwa kama itapewa kipaumbele kwa mfano na makundi yote makuu husika katika jamii kama vile jeshi la polisi, mamlaka ya mapato (TRA), mahakama,na afya. Pia vyombo vya habari vinawajibika kutoa elimu kwa umma mzima kwa njia mbalimbali, kama vile magazeti, redio, televisheni vipeperushi, nyimbo, n.k.

Njia nyingine ni kujenga utawala bora wenye uwazi na uwajibikaji, kuunga mkono tasisi husika kwa watu kutoa taarifa, kujituma kwa wafanyakazi bila kujali kupata hongo na kwa upande mwingine serikali ifuatilie vilio vya wafanyakazi hususani madai yao ya kimsingi.

Kwa kushirikiana kwa taasisi mbalimbali jamii nzima inaweza kujikuta imeichukia rushwa na kuona ni jambo lisilofaa. Kwa maana hiyo jamii nzima itawaunga mkono mashujaa wa mapambano (heroes) na kuwakataa waovu (villains) baada ya hapo sote tutakunywa mvinyo wa kifikra tukishangilia ushindi dhidi ya RUSHWA.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754-826272 au barua pepe: mhegeraelias@yahoo.com



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni