Jumamosi, 19 Julai 2014

WASTAAFU WAJISAFISHE ILI WAHESHIMIWE!

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikaa Ikulu kwa zaidi ya miaka 20 na kuaondoka akiwa na mali za kawaida kabisa, leo Ikulu ni mahali pa watu kujitajirisha!

Oktoba 28, 2007 Mtanzania Jumapili

Na Elias Mhegera
Kila mfuatiliaji wa masuala ya kijamii katika vyombo vya habari nchini Tanzania atakubaliana nami kwamba miongoni mwa habari ambazo zimegonga vichwa vya habari vingi hususani katika magazeti katika siku za hivi karibuni ni tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwa rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa.

Nimeshawishika kuchangia mawili matatu katika mjadala huo muhimu kwa maslahi ya taifa letu.

Labda kabla hata sijaenda mbali katika mjadala huu naomba nieleweke wazi kwamba simo katika kundi la wale wanaotaka iundwe tume kuchunguza tuhuma hizo za ufisadi wake, sababu zangu ni kwamba ni dhahiri kufanya hivyo hakutatuletea tija yoyote na badala yake tutaliingiza taifa katika gharama kubwa na mwisho wa siku tutaambiwa hakuna ushahidi wowote kuhusiana na tuhuma hizo.

Lakini pia naomba kutanabahisha kwamba mnamo mwaka 1995 Mkapa alipotajwa kwamba ni mtu msafi ‘Mr. clean’ nilikuwa na wasiwasi mkubwa juu ya usafi huo. Hofu yangu ilitokana na imani yangu kwamba kama kweli Mkapa alikuwa msafi basi alikuwa ni mtu wa kipekee kwani mazingira ya wakati ule yalitoa mwanya mkubwa kwa viongozi wengi kujilimbikizia mali kwa kile kilichoitwa kupunguza ‘ukali wa maisha’

Hofu niliyokuwa nayo wakati ule ndiyo hiyo hiyo inayonitatiza juu ya uwezekano wa kuundwa kwa tume huru inayoweza kuja na majibu ya uhakika na yanayoweza kukidhi matarajio ya watanzania wengi juu ya tuhuma hizo ambazo zinafumuliwa kila uchao.

Kwa hiyo naona kuna uwezekano kwamba siasa za makundi zilizoibuka hivi karibuni katika nchi yetu ndizo zinazochangia kufumuliwa kwa tuhuma hizo na inawezekana wanaofanya hivyo hawana usafi wowote pia ni watu waliokuwa ndani ya mfumo huo huo.

Naomba nisieleweke kwamba namtetea Mkapa kwa namna yoyote ile isipokuwa nataka kutanabahisha kwamba matatizo ya Mkapa ni matatizo ya mifumo tawala yote isiyotaka kuachia madaraka (rigid systems) ambayo imesambaa takribani katika bara letu zima la Afrika.

Kwa lugha nyingine ni kwamba mfumo alioupokea na ule aliofanya nao kazi na baadaye kukabidhi madaraka katika mfumo mpya lakini wa chama kile kile ni mazingira yanayoweza kusababisha kwa mtu yeyote awaye kukengeuka kimaadili hata kama aliingia madarakani akiwa msafi.

Kutokana na kukaa madarakani kwa muda mrefu kwa chama kimoja lazima kuwepo na madhara ya aina fulani kisiasa kama tunavyoshuhudia sasa hapa nchini mwetu.

Lakini pia chama pekee si tatizo bali tatizo linakuja pale chama tawala kinapokosa vyombo mahususi vya ukosoaji kama vile asasi za kiraia, vyombo huru vya habari vyama vya dhati vya upinzani na mambo kadhaa yanayoweza kuweka mazingira ya utendaji halali wa serikali iliyopo madarakani (legitimacy).

Ile dhana kwamba huyu ni mwenzetu ambayo ilikuwa inatumiwa mara kadhaa na wanasiasa wa chama tawala ilikuwa na mwangwi mbaya kwa sababu ilionyesha kwamba chama kilikuwa tayari kulinda hata waovu kisa tu ni ‘wenzetu’siasa iligeuzwa kuwa ajira ya kudumu badala ya kuthaminiwa kwamba utumishi wa umma ni jambo la kujitolea tena kwa watu wasafi na wenye dhamira njema pekee na wala si kwa kila awaye 

Ni hofu hiyo ndiyo ilinishawihi niamini kwamba kama kuna dhana ya huyo ni mwenzetu maana yake kulikuwa na mazingira ya kuwalinda wale waliokuwa na hofu ya kukabiliwa na mashtaka ya ufisadi kwa hiyo labda walimuona Mkapa kwamba ni mtu ambaye asingediriki kuhatarisha maslahi ya watu wa aina hiyo.

Kwa lugha nyingine mfumo wa awamu ya pili ndiyo hasa ulikuwa chimbuko lililojenga mazingira ya ufisadi wa baadhi ya viongozi wetu, mazingira ambayo hayakuwepo katika awamu ya kwanza ya Hayati Mwalimu Nyerere.

Kwa kusema hivyo simaanishi kwamba ufisadi haukuwepo kabisa katika awamu ya kwanza isipokuwa ulijengewa mazingira magumu ya kushamiri. Wenye nacho walijengewa mazingira magumu ya kuonyesha ukwasi wao (extravagancy).

Hivyo basi yawezekana kabisa kwamba viongozi wetu walianza kujichumia mali taratibu, kimya kimya katika awamu ya kwanza lakini wakaonyesha kucha zao katika awamu iliyofuata kutokana na ukweli kwamba mazingira yaliwaruhusu kufanya hivyo.

Kwa maana hiyo kile kilichoitwa usafi wa Mkapa yawezekana kilitokana na ukweli kwamba yeye binafsi kamwe hakuwahi kujidhihirisha kwamba alikuwa muathirika wa ukwasi wa viongozi wa awamu ya pili jambo ambalo lilichangia kuanguka kwa umaarufu wa kisiasa wa Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Upo pia uwezekano kwamba Mkapa alikuwa mtu msafi hadi wakati ule lakini aliharibiwa na mfumo alioukuta kwa sababu hakuweza kufanya mabadiliko ya dhati kuwaondoa viongozi ambao usafi wao kimaadili ulikuwa unatia mashaka.

Historia inatuonyesha kwamba wapo viongozi ambao wamepata kuharibiwa na mifumo japokuwa walikuwa na dhamira safi kabla ya kutekwa nyara na mafisadi na watu wenye dhamira za kufanikisha mambo yao binafsi.La kushangaza ni kwamba historia inatueleza kwamba hata watu kama Adolf Hitler ambao baadaye wamekuja kingizwa katika safu ya madikteta wabaya kabisa waliopata kutokea hapa duniani nao walianza kama watu wenye dhamira njema hadi pale walipotekwa nyara na watu wenye maslahi binafsi.

Hadi pale alipotoa kitabu chake ‘Mein Kempf’ (1925) yaani mapambano yangu bado Hitler alikuwa bado ni mtu mwenye dhamira safi kabisa. Lakini dhamira hiyo safi ya kuwatumikia wanyonge aliyokuwa nayo Hitler iliotekwa nyara na mabepari waliohofia kutaifishwa mali zao iwapo utawala wa kikomunisti ungeingia madarakani kwa hiyo mabepari hao ndiyo waliomteka nyara Hitler wakamgeza kuwa chombo cha kulinda maslahi yao hususani mali na viwanda vyao.

Kuungwa mkono huko kwa Hitler hakukuja kama bahati mbaya bali kulitokana na fundisho walilopata kutoka kwa wenzao wa Urusi baada ya mapinduzi ya kikomunisti yaliyoendeshwa na V.I. Lenini Oktoba 1917.
Katika mazingira hiyo mabepari wa Ujerumani walikuwa na haki ya kulinda mali zao ili zisije taifishwa na kuwekwa mikononi mwa umma kama ilivyojitokeza huko Urusi. Hata hivyo Hitler huyo huyo baadaye aligeuaka na kuwa shubiri kwa kila mpenda amani duniani yaliyofuata baada ya hapo ni historia ambayo inafahamika na takribani na kila mmoja wetu.

Kwa mantiki hiyo ndiyo maana nasema upo uwezekano kwamba Mkapa alikuwa mtu msafi kabisa lakini alitekwa nyara katikati ya safari yake na kundi fulani la watu ambao walikuwa wametanguliza maslahi yao binafsi.
Ni kundi hilo ambalo limesababisha sasa aandamwe an tuhuma nyingi ambazo hata hivyo hajawahi kuzikanusha kwa ukamilifu bali amekuwa akizizungumzia kijuujuu tu.

Kwa hiyo kama tunajiaminisha kwamba mkapa alikuwa mtu msafi basi lazima tukubali kwamba lipo kundi la watanzania wenzetu ambalo lilimpaka mawaa likamvuta katika ufisadi, akajikuta ameangukia huko bila kutarajia.

Kwa upande mwingine naweza kusema kwamba hatuna uhakika kama kundi hilo bado limo ndani ya mfumo unaotawala sasa au la kwa sababu chama ni kile kile japo yamefanyika mabadiliko hapa na pale.

Lakini upo uwezekano pia kwamba kama kweli tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa zina ukweli basi labda msukumo ulitoka nje.  Kwa upande huo napenda niunge mkono hoja iliyotolewa na mwandishi mwandamizi Lawrence Kilimwiko katika makala yake: Afrika Bado Haijawa Huru, Mwananchi, toleo namba. 02634 jumatano Agosti 29, 2007.

Hoja ya Kilimwiko  katika makala yake ni kwamba viongozi wetu wanaangukia katika ufisadi kwa sababu ya kukubali kutumiwa kama maajenti wa maslahi ya nje.

Jambo hilo linafanyika  kwa lengo la kulinda mikataba inayolinyonya bara letu au hata kwa lengo la kuanzisha mikataba mipya ya aina hiyo. Kilimwiko anatahadharisha kwamba hicho ni chanzo kimojawapo cha kushidikana kwa wazo la kuwa na serikali moja ya bara la Afrika.

Kwa hiyo kama kuna ukweli juu ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa basi tuziangalie katika mtindo huo kwamba yawezekana amepotoshwa na kundi la mafisadi wa ndani, wa nje au hata kwa ujumuisho wa makundi yote haya mawili la ndani na lile la nje.

Hapo ndipo kuna swali muhimu kwetu kwamba tupo tayari kuikabili na kuitokomeza mifumo yote hiyo miwili ama tunataka tuishie kwa Mkapa peke yake?

Katika kitabu chao Governance and Politics in Africa (1992) waandishi Goran Hyden na Michael Bratton wansema tatizo lililopo Afrika ni ile hali ya kupokea na kuanzisha siasa za ushindani ambazo kwa kweli zimeonyesha kwamba bara letu lilikuwa bado halijaandaliwa vya kutosha kwa siasa za aina hiyo. Matokeo yake ni kwamba vyama tawala vimeamua kuwabagua wapinzani hata katika mambo ambayo ni ya kimsingi kabisa na yanatija kwa watu wote bila kujali itikadi zao.

Mifumo tawala ndiyo inajipa ukiranja wa usimamizi na ugawaji wa raslimali za taifa hali ambayo imechangia kuwapo kwa mikanganyiko mingi na ufisadi.

Ni katika mazingira hayo sasa tunaweza kutoa hukumu ya haki kwa Mkapa, kwa kuzingatia suala la mifumo na misukukumo ya ndani na nje na wala siyo kwa kumunyooshea kidole yeye binafsi, kwa hiyo tuanze na mifumo ndipo tumalize na watu binafsi kama kweli tumedhamiria kupata ufanisi wa kudumu.

Ndiyo maana mimi binafsi kama mwandishi sina sababu ya kumtetea Mkapa lakini pia sioni sababu ya kundwa kwa tume ya kumchunguza kwa sababu kufanya hivyo ni kuliingiza taifa katika gharama kubwa na mwisho wa yote hakuna lolote la maana litakaloletwa na tume hiyo kama kweli itaundwa.

Sababu nyingine ni kwamba lazima tuangalie kwamba serikali iliyopo madarakani ni ile ile ya CCM. Kwa namna yoyote ile tuhuma zinazomhusu Mkapa (kama kweli zipo) lazima zitawagusa pia baadhi ya watendaji wakubwa wa serikali iliyopo madarakani kwa sasa jambo hilo linaweza kujenga mazingira ya kulindana.

Lakini la muhimu zaidi ni kwamba pamoja na mapungufu yake rais huyo mstaafu ameacha mambo kadhaa ya kimaendelo ambayo kwa sasa inaelekea yanasusua, hasa suala la ujenzi wa barabara ambao ulikwenda kwa kasi nzuri ya kuvutia katika kipindi cha uongozi wake.

Kwa hiyo ni lazima tufahamu kwamba pamoja na mapungufu yake zikiwemo tuhuma za kufanya biashara akiwa Ikulu, tuhuma nyingi si kwamba zinamgusa yeye pekee bali zinaugusa mfumo mzima uliokuwepo madarakani katika kipindi chake wakiwemo baadhi ya mawaziri ambao wamo katika awamu iliyopo madarakani kwa sasa.

Kama vile hiyo haitoshi tushukuru pia kwamba mfumo wa Mkapa ulikuwa na uwazi na uliruhusu kukosolewa jambo ambalo ni la muhimu katika ujenzi wa demokrasia na ndiyo maana waandishi wa habari walikuwa na uhuru wa kukosoa kila walipojisikia kufanya hivyo.
Kipindi cha utawala wake Mkapa hakuwa na kikundi cha waandishi wa kumtetea bali alijibu mapigo yeye binafsi kwa kadri alivyoona inafaa.

Ipo haja ya rais wa sasa kuchota yale machache anayoona kwamba yatamfaa katika uendeshaji wa serikali yake ya sasa. Kwa mfano ipo haja ya kupunguza ukubwa wa serikali nikiwa na maana ya kwamba baraza la mawaziri ni kubwa kuliko mahitaji halisi na uwezo wa nchi yetu kumudu gharama za mawaziri hao

Kinachojitokeza sasa kinanifanya nikumbuke dhana zilizojengwa na mwanafalsafa wa kiitaliano kwa jina Antonio Gramsci aliyeishi 1891-1937. Gramsci anayo machapisho mengi lakini yanayokumbukwa zaidi ni yale aliyoandika alipokuwa gerezani kati ya mwaka 1925-35.kutokana na kupinga ukandamizaji nchini mwake.

Mwanafalsafa huyo anazungumzia dhana nzima ya ukiritimba wa vyama kuhodhi madaraka kwa muda mrefu kwa kuhakikisha kwamba wapinzani wote wenye nguvu wanamezwa ndani ya vyama hivyo (co-optation), au vinginevyo wawe tayari kuangamizwa.

Anasema mfumo tawala uliokaa madarakani kwa muda mrefu hufikia mahali ukachoka na kushindwa kuleta mambo mapya lakini hubakia madarakani kwa kazi hiyo ya kujenga himaya ya kisiasa (hegemony). Kwa hiyo kubakia madarakani ni zoezi linalopewa kipaumbele kuliko mambo mengine yenye tija zaidi.

Mifumo tawala hulazimisha makundi yote yenye nguvu kuunga mkono mfumo tawala kwa njia mbali mbali ikiwemo kuunda tume na vyombo au itikadi zisizo na maana yoyote zaidi ya kuwapofusha watawaliwa.

Katika kutimiza hilo mfumo tawala hujenga mazingira ya kuungwa mkono kwa kila jambo, hata asasi za kiraia, wasomi, viongozi wa dini waandishi wa habari wote huvutwa ndani ya mfumo tawala kwa kutumia mbinu mbalimbali ili waunge mkono matakwa ya watawala.

Kwa bahati mbaya pale inapofikia kwamba makundi yote hayo yakagundua kwamba kuna hadaa nyingi kuliko utendaji ndipo mapambano ya dhati huanza na mwishowe ni kuzaa udikteta na ukandamizaji wa hali ya juu dhidi ya wote wanaotaka kujitoa katika “himaya” hiyo.

Yawezekana falsafa hiyo ya Gramsci ilitokana na kufungwa na utawala mbovu nchini mwake lakini mawazo yake yanatupatia fundisho kwamba si jambo jema kwa kiongozi kusifiwa sana au hata kumiliki madaraka makubwa kupita kiasi.Kama hatutaanza sasa kurekebisha mambo tusishangae kuona hali hiyo ikijitokeza hata hapa kwetu Tanzania.

Kinachonipa hofu hiyo ni ukweli kwamba tumejenga mazingira magumu sana kwa rais aliyepo madarakani kwa sasa kukosolewa. Takribani kila kundi kubwa limemezwa ndani ya ‘mtandao’ uliofanikisha zoezi la kumuingiza madarakani Rais Kikwete. Hali hiyo si ishara nzuri katika ujenzi wa demokrasia.

Tunaona kwamba makundi mbalimbali yameguswa katika teuzi mbalimbali baada ya uchaguzi mkuu uliopita. Viongozi wa taasisi, madaktari, waandishi wa habari, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasanii, n.k. wote wamemezwa ndani ya mfumo tawala.

Mazingira tuliyonayo ambapo kila inapojitokeza mwandishi mmoja akaukosoa mfumo tawala basi hushambuliwa vilivyo na kundi jingine  la waandishi ambao kwa haraka haraka huzima hoja yoyote ile isiyoufurahisha mfumo tawala. Hii si njia muafaka katika ujenzi wa demokrasia.

Waandishi hao wenye kuwashambulia wenzao wananifanya niamini kwamba Rais Mstaafu Mkapa alikuwa sahihi zaidi kwa kuruhusu kukosolewa na kujibu mapigo yeye mwenyewe pale alipoona inastahili kufanya hivyo.

Nadhani sasa ni muda muafaka kila amtakiaye rais wetu mema afanye hivyo kwa kuzingatia pande zote mbili yaani kupongeza pale inapostahili na pia kukosoa inapobidi kufanya hivyo.

Ni dhahiri kwamba kama tutaendeleza tabia ya kumpamba rais kila uchao badala ya kumsahihisha pale tunapohitajika kufanya hivyo kwa njia ya kumkosoa basi tutakuwa tunambomoa badala ya kumjenga.Vyombo vya habari ni viunganishi kati ya watawala na watawaliwa tuache vitimize jukumu hilo.

Naungana mkono hoja ya wale wanaosema Mkapa aachwe apumzike kwa sababu utamaduni wetu wa kisiasa hauonyeshi kama kweli kuna jambo lenye manufaa litakalopatikana baada ya kumchunguza zaidi ya kupoteza bure pesa za walipa kodi, na tumuache Mkapa apumzike aliyotutendea yanatosha aliyotukosea basi tumsamehe.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754 826 272




  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni