Mchungaji Christopher Mtikila ni mmoja wa watu walioipigania Tanganyika kwa muda mrefu na tumuunge mkono na wale wote wanaotaka serikali tatu au uwepo wa Tanganyika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Na Elias Mhegera
19/02/2014
VUTA nikuvute ya Katiba mpya
imefika pazuri ambapo ingekuwa ligi ya soka tungesema imefikia ‘patamu’. Hoja
hii inatokana na mivutano inayoendelea chini kwa chini kutoka vyama vya siasa
na makundi mengine ya kijamii.
Kwa sasa mada zinazoelekea kugusa
mijadala zaidi ni muundo wa Serikali ya Muungano, rasilimali za taifa na
madaraka ya rais. Wachambuzi wa masuala ya Katiba wametaja kwa nini mada hizo
zimepewa umuhimu kuliko nyingine.
Katika warsha ya Februari 13
chini ya maandalizi ya Chama cha Walimu wa Uraia (CETA) na ile iliyofanyika
Januari 31, kwa maandalizi ya pamoja ya taasisi tatu za Konrad Adenauer
Stiftung (KAS), Jukwaa la Katiba (JUKATA) na Friedrich Ebert Stiftung (FES)
ilidhihirisha kwamba muundo wa Serikali ya Muungano ni hoja nzito kupita zote
katika mtazamo wa washiriki wengi.
Akifafanua hofu na manufaa ya
kuundwa kwa serikali tatu, Profesa Josephat Kanywanyi, ambaye ni mhadhiri wa
sheria mstaafu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema ni wazi muundo wa
serikali tatu utauvunja muungano iwapo Watanzania hawatakuwa makini.
“Ni dhahiri iwapo serikali ya
Tanganyika itazaliwa na kupata rais mwenye nguvu kuliko wa serikali ya muungano
basi hilo linaweza kusababisha kuzaliwa kwa Serikali ya Zanzibar kwa kuzingatia
katiba yao ya mwaka 2010,” anaonya msomi huyo.
Profesa Kanywanyi anasema
kimsingi ingawa muundo wa serikali tatu ambao umepitishwa na Tume ya Jaji
Warioba kwa ajili ya mjadala wa kitaifa bado ni jambo jema lakini upo uwezekano
wa kuibuka kwa rais wa serikali ya Tanzania (Bara) mwenye nguvu kuliko hata wa
serikali ya Muungano.
Kimsingi msomi huyo hapingani na
hoja ya walio wengi kwa sasa ya kutaka serikali ya Tanganyika. Awali wakati wa
ufunguzi wa semina hiyo wakurugenzi wa KAS, Stefan Reith na Rolf Paasch wa FES
walisema mjadala wa Katiba mpya ni wa Watanzania, kwa manufaa yao.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la
Katiba, Deus Kibamba, anakiri kwamba kwa hali yoyote ile mwelekeo wa kuwapo kwa
serikali tatu kutadhoofisha Muungano lakini haoni tatizo kwa hilo iwapo ndiyo
chaguo la Watanzania.
Hata hivyo mwenyekiti huyo
anaipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kufanya kazi nzuri ingawa awali kulikuwa
na kusigana kwa hapa na pale kati ya tume hiyo na asasi za kiraia hususan
JUKATA.
Anasema maeneo yatakayoathiriwa
na muundo mpya wa Katiba ni umiliki wa maliasili, ardhi, mafuta na serikali za
mitaa. Anatetea hoja yake kwamba baadhi ya mambo yemeachwa kwa sababu hayahusu
muungano lakini yanaweza kuibuka katika sura mpya.
Naye mshauri mwelekezi wa masuala
ya habari, Lawrence Kilimwiko, anasema hajaridhika iwapo Katiba mpya imejikita
vya kutosha katika kuzingatia maadili ya viongozi. Pia anauliza sababu za vyama
vya siasa kuendelea kuwa suala la muungano.
“Iwapo sasa tunaruhusu mgombea
binafsi ni kwa nini suala la vyama linaendelea kuwa la muungano? Je, tunataka
kuendelea na tume ya uchaguzi kama ilivyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa?”
anauliza.
Lakini katika warsha nyingine
iliyoandaliwa na taasisi ya KAS kwa ushirikiano na ile ya Tanzania Development
Initiative Programme (TADIP) suala la Tanganyika linaonekana kuwa kinara kuliko
masuala yote yaliyopata wachangiaji wengi.
Mmoja wa Makamishina wa Tume ya
Jaji Warioba, Profesa Mwesiga Baregu, anaainisha kipengele kwa kipengele sababu
za yeye na wenzake kufikia muafaka huo.
Lakini Profesa Chris Maina
anasema bado kuna mambo yaliyoachwa juu juu. Kwa mfano lugha zinazotumika
katika viapo bado hazijaachana moja kwa moja na ile dhana ya utii kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya sheria
na siasa wanasema lilisababisha kuwapo kwa matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo anaawacha wasikilizaji
na kauli ya matumaini: “Naomba niweke wazi msimamo wangu kwamba napendelea
muundo wa serikali tatu, nina matumaini kwamba kwa mara ya kwanza sasa Watanzania
wataachana na katiba za kupandikizwa na kuwa na katiba yao,” anasema Profesa
Maina.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Jaji Mstaafu Amir Manento, anaibua furaha
kwa wanaharakati na waandishi ukumbini kwa kusema: “Nipo tayari kunukuliwa
popote pale msimamo wangu ni wa serikali tatu!” anasema.
Mjadala mkubwa hapo unajikita
katika masuala ya muungano. Muwezeshaji kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) William Kahale,
anatoa mada kwa staili yake ya kupiga kura.
Kura zinapigwa kabla ya mijadala
na inaonekana kwamba watu 29 katika ya 57 wanataka serikali tatu lakini baada
ya mijadala inaonekana asilimia 95 wanataka serikali tatu, hali inayothibitisha
kwamba mijadala ina umuhimu katika kuwajengea wananchi uelewa juu ya masuala ya
katiba.
Humphrey Polepole, Kamishina wa
Tume ya Jaji Warioba, anasema walichokifanya wao ni kupata maridhiano ya
makundi yote badala ya kuangalia masilahi ya vyama na itikadi za makundi
yaliyowatuma.
Tuwasiliane: mhegera@gmail.com simu: 0754-826272
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni