Mwenyekiti wa Umoja wa Asasi za Kiraia (AZAKI) Katika Mchakato wa Kupata Katiba Mpya Bw. Irenei Kiria akisoma tamko la AZAKI tarehe 24/4/2014 katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Na Elias Mhegera
KUPINGWA kwa mchakato wa katiba mpya
unaoendelea mjini Dodoma na makundi mbalimbali ya wanajamii, ni ishara tosha
kwamba mtindo wa uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK) unaotumika hauwezi
kutoa katiba ya wananchi.
Hofu ya kuvurugwa kwa mchakato huo ilianzishwa
na Rais Jakaya Kikwete mwenyewe, pale alipolihutubia Bunge hilo mjini Dodoma
mnamo tarehe 21 Machi, ambapo kiongozi huyo wa kitaifa alidiriki kuikejeli Tume
ya Mabadiliko ya Katiba (TMK) ya Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Kejeli ya kazi hiyo na matumizi ya takwimu
vikachochea wanachama wa chama chake, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuata
mkumbo na kuanza kurusha makombora dhidi ya Mzee Warioba na timu yake.
Ni kutokana na muendelezo huo unaotaka
kuuteka mjadala huo kwa manufaa ya CCM, ndipo makundi mengine ikiwa ni pamoja
na wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na wanajamii wengine
ikiwamo asasi za kiraia, wamepinga kwa namna mbalimbali kutekwa kwa mchakato
huo.
Wanafunzi wa vyuo vikuu
Siku chache zilizopita, mtandao wa umoja wa
wanafunzi wa vyuo vikuu chini ya mwamvuli wa Tanzanian Students Networking
Programme (TSNP) kwa kushirikiana na Shirika la Kijerumani la Konrad
Adenauer-Stiftung (KAS) waliandaa mjadala kuhusu nafasi ya vijana katika katiba
mpya.
Katika mjadala huo uliofanyika katika hoteli
ya Landmark, Ubungo Riverside, sauti nyingi zilionekana kuitetea Tume ya
Mabadiliko ya Katiba maarufu kama Tume ya Jaji Warioba pamoja na rasimu yake ya
katiba ambayo sasa inaelekea kuwekwa pembeni kutokana na ubabe unaofanywa na
CCM dhidi ya wananchi waliotoa maoni yao kupitia tume hiyo.
Akiwakaribisha vijana wenzake zaidi ya 60
katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa TSNP, Alphonce Lusako, alisema kwamba
vijana wametengwa sana na utawala uliopo madarakani ikiwa ni pamoja na
kutokushirikishwa katika mambo mengi ya kitaifa.
Alisema kwamba vijana wengi wanaohitimu
kutoka katika vyuo vikuu hujikuta hawana ajira na hivyo wengine kushawishika
kujiunga katika makundi mbalimbali mazuri na mabaya katika kuhaha wakitafuta
maisha na mkate wao wa kila siku.
Alisema hali ni mbaya zaidi kwa wale ambao
hawajafika katika ngazi ya vyuo vikuu na hao ndio wanaouawa na polisi katika
maandamano ya vyama vya upinzani wakiwa katika kutafuta watetezi wa hatima zao.
“Vijana tumeonewa sana, wamachinga
wanafukuzwa hapa na pale kila kukicha, vyuo vikuu vinafungwa kila uchao,
ufisadi umetamalaki kila mahali nchini, ni lazima tupiganie katiba mpya
itakayolinda maslahi yetu,” aliwahamasisha wenzake.
Naye Mkuu wa Utawala wa KAS, Richard Shaba,
alisema kwamba taasisi yake ililetwa na Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa la
Tanzania ili kuanzisha Chuo cha Itikadi Kivukoni, ambacho kiliwaandaa viongozi
bora wa nchi hii ambao alidai kwa sasa wamebakia wachache sana.
Humphrey Polepole afichua siri nzito
Aliyekuwa mmoja wa makamishna wa TMK,
Humphrey Polepole, alisema kwamba kuna siri nzito zinazofanya watawala na
vibaraka wao waichukie rasimu ya katiba inayoendelea kujadiliwa Dodoma.
Alisema miongoni mwa mambo hayo ni kupunguzwa
kwa madaraka ya rais, kuwekewa msisitizo wa maadili ya viongozi, kupunguzwa kwa
idadi ya wabunge na kuwekwa kipengele cha kuweza kumng’oa mbunge aliyepo
madarakani.
“Sasa hivi mimi naongea kama kijana, kama
mwana-asasi za kiraia na vile vile kama Mtanzania mwenye uchungu na nchi yake,
mimi simuogopi mwanadamu yeyote na nipo tayari kuyasimamia yote yaliyotajwa na
tume yetu (TMK),” alisema na kuasababisha hamasa kubwa ukumbini.
Akiendelea kufafanua kwa kujiamini, alidai
kwamba tume yake ilifanya utafiti wa kina na kuyajadili, na kuchuja yote
yaliyotokana na tafiti hizo ndipo wakaja na rasimu ambayo inaelekea kuwa mwiba
mkali kwa watawala.
“Huwezi ukang’ang’ania muungano katika muundo
uliopo sasa ambapo Zanzibar imeunda katiba yake inayosema Zanzibar ni nchi na
kisha inakataa kuitambua Mahakama Kuu ya Tanzania, Taasisi ya Viwango (TBS),
hawachangii kodi za mapato na wala hawamtambui Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, huu ni unafiki mkubwa,” alimaka Polepole.
Alifichua pia kwamba katika kipindi cha
kuunganishwa kwa mataifa haya, Wazanzibari chini ya hayati Abeid Amani Karume
walikuwa wanauhitaji muungano kwa udi na uvumba ili kuzuia uwekezano wa kurejea
kwa utawala wa Sultani, na hivyo labda leo hawana hofu hiyo tena na ndiyo maana
wameamua kuja na katiba yao inayotanguliza utengano badala ya kuongeza
ushirikiano.
Alisema kelele za wanasiasa wa Tanzania Bara
(Tanganyika) kuililia Zanzibar hazitokani na kuwapenda Wazanzibari, bali kwamba
muundo wa muungano uliopo unawabeba wao ili kuendelea kujikita madarakani kwa
manufaa yao na kwa hasara kubwa kwa Watanzania waliosalia.
Polepole alishangazwa na kitendo cha Rais
Kikwete kushindwa kuilinda katiba aliyoapa kwamba atailinda na kuitetea wakati
aliposhuhudia ikivunjwa, lakini akapata ujasiri wa kumshambulia Jaji Warioba na
timu nzima na hata Watanzania waliotoa maoni kupitia kwenye timu hiyo.
Wanavyuo wahamasika, waja juu
Baada ya mijadala yao, wanafunzi wa vyuo
vikuu walihamasika na kutoa maazimio kama wakisema kwamba wananchi wachukue
hatua ya kulivunja Bunge hilo iwapo halileti tija iliyotarajiwa.
Vijana waliipongeza TMK ya Warioba na kudai
kwamba jaji huyo huyo aliwahi kuheshimiwa sana alipotafiti mianya ya rushwa,
lakini leo anashambuliwa na watawala kwa sababu amegusa maslahi yao.
Walionya mara moja kutumika kwa vitisho
kwamba jeshi litaipindua nchi iwapo muundo wa serikali tatu utapitishwa,
vijembe na matusi yanayoendelea ndani ya BMK. Na pia walisema watahamasishana
ili vijana wote waliofikia umri wa kupiga kura wafanye hivyo na kuleta
mabadiliko ya dhati nchini Tanzania.
Walitoa onyo kwa vyombo vya dola kutumika kwa
manufaa ya watawala katika kile kinachoitwa “kulinda amani ya nchi” na hivyo
kuwageuza vijana kuwa asusa wa kupigwa risasi na kuuawa mara kwa mara pale
wanapoonyesha kuwa na misimamo tofauti na watawala wa nchi hii.
Waliahidi kuendelea kuwahamisha vijana wenzao
kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembeleana vijiweni na katika mitandao
ya kijamii kama vile facebook, twitter na blog na kushiriki katika mijadala
mitandaoni kama vile Jamii Forum, Wanabidii, Wanamabadiliko.
Viongozi wa kiroho nao wachachamaa
Wakati hayo yakiendelea kwa vijana, viongozi
wa kiroho nao walionyesha kukerwa na mchakato unavyoendelea na wakapeleka
maazimio yao Dodoma kwa ajili ya kumkabidhi Mwenyekiti wa BMK, Samuel Sitta.
Mwamvuli uliotumika unaitwa Baraza la
Mahusiano ya Dini mbalimbali kwa Amani Tanzania (IRCPT) watumishi hao wa Mungu
kutoka madhehebu ya Kihindu, Baahai, Kikristu, Kiislamu na Wabudha, walitoa
maoni na mapendekezo yao kufuatana na mjadala wa katiba mpya.
Walidai kwamba katiba mpya iache kuendekeza
mambo ya kufichaficha masuala yanayowahusu wananchi na wakataka katiba mpya
ilete uwazi, umoja, ilinde hadhi ya taifa na uwajibikaji. Pia walitaka taifa
lizilinde kwa dhati tunu zake kupitia katika katiba yake.
Wakati viongozi hao wakijiandaa kupeleka
madai hayo, ndipo hati za muungano zikatolewa hadharani kwa mara ya kwanza
jambo ambalo linaacha maswali mengi kuliko majibu, kwamba kulikoni nyaraka hizo
za taifa zinafichwafichwa? Je, kuna siri gani inafichwa hapo?
Miongoni mwa mambo muhimu waliyodai katika
mkataba mpya ni pamoja na rais mstaafu kufikishwa mahakamani kwa makosa ya
kijinai aliyoyatenda wakati akiwa madarakani.
Asasi za kiraia nazo zakerwa
Labda katika kuonyesha ni kwa kiwango gani
Watanzania wengi hawaridhishwi na jinsi mchakato mzima wa kupata katiba mpya
unavyoendeshwa, asasi za kiraia nazo hazikubakia nyuma.
Akisoma tamko kwa niaba ya asasi zaidi ya
500, mwenyekiti wa jumuiko la mitandao na asasi za kiraia (NGOs) na Networks,
Irenei Kiria, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Asasi ya Sikika, alisema wana-azaki
wanalaani jaribio la kuuteka nyara mchakato wa katiba kwa manufaa ya watu
wachache na kupuuzwa kwa maoni ya wananchi kama yalivyokusanywa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Warioba.
mhegera@gmail.com Simu: 0754-826272

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni