pichani ni miongoni mwa nyumba ambayo ziliteketezwa na inaosadikiwa kuwa ni wafugaji wa Kimasai katika mgogoro wa kugombea ardhi katika bonde la mto Mgongola wilayani Mvomero
Na Elias
Mhegera
Oktoba 28 /2013
Miongoni mwa majukumu magumu kabisa ambayo
mtu anaweza kuachanganyikiwa na kukosa ufumbuzi iwapo atakabidhiwa ni jukumu la
kusuluhisha migogoro inayoendelea nchini Tanzania kati ya wakulima na wafugaji.
Na kwa msingi huo naamini kwamba nitaitendea
haki mada ninayotaka kuijadili kwa sasa iwapo nitavaa joho la msuluhishi asiye
na upande katika migogoro yenyewe. Na pili ni lazima niwe na busara ya kukumbuka
kwamba wanaouana ni Watanzania wenzangu tena kutoka tabaka moja la ‘walalahoi’
lililosahaulika.
Kwa bahati mbaya wakati hali hiyo ikiendelea
kuna mabadiliko kadha wa kadha yanaotokea nchini ambayo ni ya kisiasa,
kiuchumi, kiitikadi na hata kimaadili ambayo yamesababisha umiliki wa ardhi
ulete migogoro mikubwa isiyo na kifani.
Katikati ya maendeleo hayo hasi kuna jambo
limejitokeza nalo ni kusambaratika au kudhoofika kwa nguvu ya dola inayolenga
katika kuwaunganisha Watanzania, na badala yake kuibuka kwa matumizi makubwa ya
nguvu za dola na hivyo kuzidisha uchonganishi badala ya upatanishi mfano hai
ukiwa ni Kiteto.
Mchango wa
viongozi
Ni dhahiri ukitaka kuijadili migogoro mikubwa
inayoendelea nchini ni lazima uanze kwa muktadha mpana wa kuangalia tulikotoka
na kule tunakoelekea. Kwa mfano miaka ya utawala wa Mwl. Julius Nyerere
alilenga kuupenda ujamaa, kilimo, na Uafrika.
Leo hii taarifa nyingi kuanzia katika asasi
za kiraia (NGOs) na hata za waandishi wa habari mikoni zinaonesha kwamba NGO
zinazojihusisha na masuala ya ardhi na mazingira zipo katika hali ngumu kiusalama
na pia wanahabari wanakuwa na hali ngumu pale wanapogusia masuala ya ardhi.
Katika ujumla wao watetezi wa haki za
binadamu wanakuwa na changamoto zaidi pale wanapogusa maslahi ya ardhi ambayo
kimsingi ni ya kisiasa. Kwa mfano Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Jukwaa la Katiba (JUKTA) na hata Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT)
hawawezi kuwekwa katika kundi moja na NGO zinazotetea wanawake na watoto kama vile
WLAC au TAWLA.
Katika muktadha huo huo waandishi wa habari
wanaguswa na vyombo vya dola pale wanapoandika juu ya ufisadi katika
halmashauri za miji kwa sababu huko kuna miungu watu waliojitangazia ufalme na
pale wanapogusa maslahi ya wakubwa kama vile ardhi zinazoporwa kutoka mikononi
mwa wanyonge.
Binafsi nimebahatika kutembelea mikoa
taribani 18 ya Tanzania Bara na pia Unguja na Pemba. Nimehuhudia jinsi ambavyo
viongozi wetu waliopo madarakani na wale waliostaafu wanavyojimilikisha maeneo
makubwa ya ardhi hali ambayo sasa imesababisha uhaba mkubwa wa raslimali hiyo
kwa wakulima na wafugaji ambao kwa upande wao wameshindwa kumtambua adui yao halisi
ni nani.
Tembelea Morogoro, Manyara, Bahi n.k. utakuta wakuu wa wilaya wamehusika kwa kiwango
kikubwa katika kupora ardhi kwa niaba ya wakubwa zao waliowatuma. Na kwa maana
hiyo basi wakati mwingine ndiyo maana wanashindwa kuitatua kwa sababu kimantiki
ni vigumu kwa mtu yeyote kuutatua mgogoro kwa weledi yakinifu iwapo yeye
mwenyewe anamaslahi ndani ya mgogoro huo.
Mgogoro wa
Mvomero
Ingawaje mwandishi wa makala hii hajafanya
tafiti za kina juu ya migogoro ya ardhi lakini kwa kiwango fulani anaweza
kujigamba kwamba ana uelewa wa kutosha wa kuizungumzia. Kwani amewahi kuhudhuria
warsha kadhaa za HakiArdhi, taasisi inayojihusisha na tafiti na ufuatiliaji wa
masuala mbali katika ardhi na hata kufanya mahojiano na afisa mwandamizi wa
taasisi hiyo Wakili Joseph Chiombola kwa ajili ya uandaaji wa makala kama hii.
Pia amepata kuwapokea wakulima kutoka mkoani Morogoro
kwa nyakati tofauti tofauti na kuwasaidia kutoa taarifa zao kwenye vyombo vya
habari. Kilichodhahiri kutokana na tafiti zake ni kwamba Mkoa wa Morogoro ni
miongoni mwa mikoa iliyoathirika sana kutokana na uvamizi wa matajiri wengi
wakiwamo viongozi wa serikali kutoka Dar es Salaam.
Kwa lugha nyingine ukaribu wa mkoa huo na
jiji la Dar es Salaam ndiyo umechagiza zaidi ulafi wa wenye pesa katika
kijitafutia maeneo makubwa ya ardhi mkoani humo. Katika siku za hivi karibuni
lugha kuu zinazotumika ni kama tatu hivi. Kwanza ni Kilimo Kwanza, pili ni
Hafidhi za Taifa na tatu ni Utunzanji wa ardhi oevu chini ya Mkataba wa Ramsar
nchini Iran wa mwaka 1971.
Mazoezi yote hayo yamekuwa yakiendeshwa bila
ushirkishwaji wa kutosha wa wakulima ambao wengi wao uelewa wao ni mdogo. Kwa mfano katika mkutano mmoja ambao
mwandishi wa makala hii alihusika kwa kumsaidia kiongozi wa wakulima kutoka
Morogoro, kiongozi wa msafara alidai kwamba ardhi yao imeporwa na akakabidhiwa
muarabu mmoja anayeitwa Ramsar.
Msafara huo ulikuwa na watu wasiopungua kumi,
ikabidi kuwauliza wakulima wale suali la kizushi kama wote wamewahi kumuona
huyo muarabu anayeitwa Ramsar wakasema ni kweli wamekuwa wakimuona na kisha wakaanza
kuelezea jinsi alivyo. Mkanganyiko huo
ulitosha kuonesha kwamba hapakuwa na ushirikishwaji wa kutosha kwa wakulima hao
kabla ya kuanza kuwanyakua mashamba yao.
Kwa hiyo taswira nzima ya mkoa wa Morogoro
haipishani sana isipokuwa namna masuala hayo yanavyoshughulikiwa. Mgogoro wa Mvomero
ulimpatia nafasi mwandishi wa makala hii kushuhudia kinachoendelea mikoani
ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe katika jina la wakulima na wafugaji
ili labda kuondoa dhana ya kwamba wanaopigana ni Watanzania wenzetu.
Mgogoro wa Mvomero una taswira nyingi na
labda unaweza kufananishwa kwa kiwango fulani na ule wa Kiteto. Mwandishi wa
makala hii alifika wilayani Mvomero akiwa ni mmoja wa wajumbe wa asasi za
kiraia nne, yaani ya wafugaji PINGOs kutoka Arusha, HakiArdhi kutoka Dar es
Salaam, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kutoka Dar es Salaam
ambao mwandishi wa makala hii uliuwakilisha.
Baada ya kufika Morogoro timu hii iliunganika
na taasisi mbili zenye makazi yao mkoani humo, yaani Mtandao wa Vikundi vya
Wakulima Tanzania (MVIWATA) na Parakuiyo Pastoralist Indegenous Community Development
Organisations (PACODEO) na pia ikaunganika na wanahabari Michel Msilo (ITV) na
Juma Mtanda (Mwananchi) ambao walikuwa wameuripoti mgogoro huo kwa kina.
Muhtasari wa
visa na mikasa
Ili msuluhishi apate busara katika mgogoro
huu ni vyema awaangalie wafugaji na wakulima kwamba wote ni sawa na watoto wake
waliokosa maridhiano lakini yeye anawapenda wote kwa kiwango sawa.
Mtazamo wa nani ni mkorofi, nani siyo, nani
ana nyaraka, nani hana, nani ni mwenyeji nani ni mgeni na labda nani anatumiwa
na anatumiwa na yupi n.k. ndicho chanzo kikubwa cha kushindikana kwa muafaka wa
mgogoro huo kwa njia ya majadiliano.
Kuna mengi yametokea wilayani Mvomero licha
ya vifo vya zaidi ya watu 30, bado mpaka sasa kuna makovu ya watu kuchomewa
nyumba na akina mama toka pande zote mbili za wakulima na wafugaji wakidai
wamekuwa wakitishiwa kubakwa. Wawakilishi wa NGOs walikuwa na wakati mgumu
kidogo wa kuchambua nani anasema ukweli kati ya wafugaji na wakulima chini ya
umoja wao wa Umoja wa Wakulima Mgongola (UWAMGO)
Eneo lililosababisha mauji ya watu sita mmoja
akiwa ni mfugaji na wakulima watano ni bonde la mto Mgongola, Kambala, Hembeti,
Mkindo na Msufini ambako kuna baadhi ya wakulima wanaishi na wengine kutoka
kijiji kimoja kwenda kingine kwa ajili ya kilimo.
Hebu jaribu kudodosa kauli hizi za viongozi
kama ifuatavyo;
Msimamo wa
MVIWATA
Mkurugenzi wa MVIWATA Bw. Stephen Luvuga anaonesha
uelewa na ushirikiano wa hali ya juu katika kutafuta utatuzi wa mgogoro huo.
Hata hivyo katika maelezo yake anaonesha dhahiri kuwa na huruma kwa wakulima
ambao chombo chake kimuundo ndiyo hasa jukumu lake kuhakiksha kwamba maslahi ya
wakulima yanakumbukwa katika undeshaji wa nchi.
Hata hivyo Bw. Luvuga hafichi hisia zake anapoeleza
kwamba mgogoro huu unamaslahi mengi yaliyofichika ingawaje hata baadhi ya
wahusika wenyewe (wagomvi) hawayafahamu maslahi hayo na badala yake wamezingwa
katika mitazamo ya kikabila na kutawaliwa na hasira kali zenye madhara makubwa.
Msimamo wa
Askofu Jacob Maneo wa KKKT
Kiongozi huyo wa kiroho na Askofu wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ni mtumishi wa Mungu mwenye viapo vya
kuutetea ukweli bila woga. Anaeleza kwa kina anavyoufahamu mgogoro wenyewe tena
akiwa na uchungu mkubwa kwa sababu baba yake mzazi Marehemu Paul Sendeu Moreto
aliuawa mwaka 1991 wakati akitafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi.
Askofu huyo anaeleza kwamba anasikitishwa na
jinsi baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vinaripoti matukio ya mgogoro huo
na kuwafanya wanajamii ya Kimasai ambao yeye ni miongoni mwao waonekane kwamba
ni watu katili. Anaeleza pia jinsi ambavyo jamii hiyo ya wafugaji wanavyoteseka
na kwamba sasa wanatakiwa kuondolewa kwa kuonekana kwamba ni wavamizi.
Msimamo wa wafugaji
Kwa upande wao wanajitetea kwamba wanauhalali
wa kuishi katika maeneo yaliyopo bila kubughudhiwa kwa sababu wanazo nyaraka halali
za makazi na shughuli za ufugaji ambayo kwa sasa yanagombewa. Wanatoa nyaraka
zao kwa timu ya NGOs na kwa waandishi walioambatana na timu hiyo. Inadhhirika
kwamba nyaraka hizo ni za muda mrefu na pia kuna ramani iliyochorwa kitaalamu.
Wakiongozwa na diwani wa zamani wa Kata ya Hembeti,
Majuka Koira wanasema wamekuwapo kwa miaka mingi katika maeneo hayo na
wanashangaa leo kuitwa kwamba ni wavamizi. Bw. Koira anasema alisoma katika
Shule ya Msingi Hembeti mwanzoni mwa miaka ya 70. Anakosoa kwamba wakulima
wamekodi kikundi cha Umwano ambacho hakitokani na wanavijiji hao bali ni watu
wa kukodiwa kwa lengo la kuwadhuru wafugaji.
Msimamo wa
wakulima
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Bi. Zawadi Juma
Chande wanaonekana kuwa na uchungu na hasira dhidi ya wafugaji na kuwaita
majina ya kuwakana kama vile Wamasai au Wakenya. Lengo mahsusi la lugha hizo ni
kuwakana ili waonekane kwamba ni wageni wavamizi. Wanaikanusha historia ya Askofu Maneo na ile
ya Bw. Koira ambaye wanasema hasemi ukweli.
Wanahitimisha kwa kusema kwamba ongezeko la ghafla
la mifugo limetokana na kufukuzwa kwa wafugaji wa Kimasai kutoka maeneo mbali
mbali nchini na mwisho wa siku kuzamia Mvomero ambako wamepata unafuu. Kwa
mujibu wa wakulima wafugaji hao ni watu wakorofi na wapenda vita.
Msimamo wa
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Anthony Mtaka
Kwa bahati mbaya DC huyu kijana anaanza kwa kuwatazama
wawakilishi wa NGO kwa mtazamo hasi kama ilivyokawaida kwa viongozi wengi
serikalini ambao huona kwamba asasi za
kiraia zina tabia ya kukosoa hata pale zisipostahili kufanya hivyo. Kwa hiyo
badala ya kujibu maswali yeye ndiye akawa muulizaji mkubwa kwa maswali kama
“kwani nyie mlitakaje?” au wewe ungefanyeje? Hatimaye timu ya NGO inamuomba
asilete malumbano yasiyo na tija.
Hapo DC anateremsha munkari na kuanza kujibu
kwamba yeye amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kutatua mgogoro huo lakini
kilichomkera ni pale magari kadhaa ya watendaji wake yaliporushiwa (kupopolewa)
kwa mawe na wakulima wenye “hasira kali” kiasi kwamba licha ya kufunga bara
walidhamiria hata kuwaduru viongozi wa wilaya.
Msimamo wa
Afande OCD Idd Abdallah Ibrahim
Anakiri kwamba kutokana na ugeni wake katika
eneo hilo bado hajauelewa mgogoro huo kwa undani lakini hata hivyo anaamini
mbinu sahihi za usuluhishi hazitumika. Anashauri kwamba watendaji wangejipatia
muda wa kutosha ili kuizisikiliza pande kuu zinazokinzana kwa nyakati tofauti
na kisha kuwaweka pamoja wote wakulima na wafugaji.
Maoni ya
Mkuu wa Mkoa Joel Bendera
Labda miongoni mwa mambo yaliyowashangaza
wawakilishi wa timu ya NGO ni ile hali ya woga aliyokuwa nayo mkuu wa mkoa.
Pamoja na kwamba RC huyo alitoa ushirikiano wa dhati kwa timu ya NGO lakini anaonekana
kama vile anayejaribu kuukwepa mgogoro wenyewe.
Katika utetezi wake anadai kwamba mgogoro
wenyewe upo katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi hivyo yeye hawezi kuuingilia
mhimili huo ingawaje anakiri kwamba tayari alimuomba Jaji Mkuu Othman Chande
ili kesi hiyo iharakishwe. Na pia anasisitiza kwamba mgogoro huo umo katika
eneo la kiutendaji la DC wa Mvomero.
Mapendekezo
ya asasi za kiraia
Miongoni mwa mapendekezo muhimu kutoka katika
NGOs ni kwamba viongozi wa mkoa hawastahili kutoa utetezi wa aina yoyote na
kwamba katika mazingira hayo DC hawezi kuachiwa kutatua mgogoro ambao umesababisha
mauaji ya watu mara kadhaa. Hali kadhalika si jambo jema kwa kiongozi kujitenga
na mgogoro unaendelea katika eneo lake kwa kisingizio cha kuogopa kuingilia
uhuru wa mahakama, hadi mwaka jana mgogoro ulikuwa mahakamani kwa zaidi ya miaka
minane.
Asasi za kirai zinashauri kwamba wabunge wa
majimbo mawili la Morogoro Mjini Aziz Aboud na wa Mvomero Bw Amos Makala kwa
kushirikiana na Mkuuwa Wilaya ya Mvomero, Mtaka, na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Morogoro,
Bendera, wakutane mara kwa mara ili kupeana maendeleo ya usalama katika wilaya
hiyo mpya na changa.
Na vivyo hivyo viongozi mbali mbali likiwamo
Jeshi la Polisi na wanajamii wengine wajitahidi kuingilia katika kutatua
migogoro badala ya kusubiri mauaji yatokee ndipo waanze kuhesabu miili ya
marehemu na kulaani mauaji kama ilivyogeuka kuwa mchezo wa kawaida sasa.
Pia kuwepo na muingiliano wa kijamii kama
vile michezo ya ujirani mwema kati ya wakulima na wafugaji, kupata chakula na
vinywaji kwa pamoja, ngoma za kimila na hata kuoleana kwa makabila ya pande
hizo mbili kama ilivyo jadi nchini Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni