Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na DP kikiwakilishwa Mch. Christopher Mtikila, wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakiondoka bungeni kwa madai kwamba wenzao CCM wameuteka nyara mchakato wa kupata katiba mpya.
Na Elias Mhegera
Taasisi ya Kijerumani yenye uwakilishi nchini Tanzania ya
Konrad Adenaeur Stiftung (KAS) imekanusha kwamba inawafadhili wabunge wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ili wasusie vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Katika mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake mtaa wa Upanga
Isimani hivi karibuni, Mwakilishi Mkazi wa KAS nchini Tanzania Bw. Stefan Reith
alisema anasikitishwa na propaganda chafu zinazoelekezwa kwa taasisi yake
kwamba ndiyo inayowafadhili UKAWA kwa lengo la kuharibu mchakato wa kupatikana
kwa katiba mpya.
“Ninasikitika kwamba kuna waandishi wanaoshindwa kuzingatia
maadili ya taaluma yao na kisha wanaandika habari za kutunga mezani ambazo
zinaweza tu kuandikwa na waandishi wasio ifahamu vizuri taaluma yao na pia
kuchapishwa na vyombo visivyoheshimika.” anasema.
Kujiondoa kwa wabunge wa vyama vya upinzani vya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na National
Convention for Construction nand Reform (NCCR-Mageuzi) kumeleta sintofahamu
iwapo kweli katiba mpya itapatikana katika mazingira ya sasa.
Kujitoa huko kulikofanyika mwezi Aprili kumesababisha pia mgawanyiko
mkubwa kwa wananchi kwa ujumla huku wale wanaounga mkono muundo wa serikali
tatu wakiwaunga mkono UKAWA na wale wanaopenda muundo wa serikali mbli uendelee
wakiwashambulia wabunge hao wa upinzani.
“Si taasisi yangu wala ubalozi wa Ujerumani tunaowafadhili
UKAWA, bali kinachoendelea ni matunda ya mabadiliko ya kisiasa ndani ya
Tanzania. Gazeti hilo limeaindika uongo mtupu kwa kudai eti tunatoa kiasi cha
shilingi 450,000 kwa siku na ndiyo maana wabunge wa UKAWA wameamua kujitoa kwa
sababu posho yao ni shilingi 300, 000/= huu ni uzushi mkubwa” anasema Reith.
Pia anashangaa kuona kwamba mashambulizi yanaelekezwa kwenye
taasisi yake sasa bila kukumbuka kwamba taasisi hii imekuwapo nchini Tanzania
kuanzia mwaka 1964 walipoanza ujenzi wa chuo cha itikadi cha TANU Kivukoni, kwa
wakati huo, kwa sasa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Anakumbusha kwamba taasisi yake ambayo kwa sasa inashambuliwa
pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kutibu majeraha yaliyosababishwa na
kampeni chafu za udini ambazo zilisababisha kuanza kwa mitafaruku ya udini
ambayo tayari ilikwisha sahaulika nchini kwa muda mrefu.
Anashangaa kuona kwamba taasisi yake ndiyo inashambuliwa kwa
taarifa mbaya wakati zipo taasisi nyingine kutoka nchini mwake na hata nje ya
Ujerumani zikiwa na mahusiano na vyama vya siasa vingine kama ilivyokuwa kwa
CHADEMA na KAS.
“Kuna shirika la Friederich Ebert Stiftung (FES) ambalo
linaushirikiano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini halishambuliwi, kuna
shirika la Friederich Naumann Stiftung lenye ushirikiano na (CUF) lakini yote
hayo hayashambuliwi, mitazamo ya kuishambulia KAS ni hafifu” anasema.
Bwana Reith anasema kwa upande mwingine mashambulizi hayo
yanampatia faraja kwamba shirika lake linafanya kazi nzuri. Lakini anaonya
tabia ya kulihusisha shirika lake na masuala ya dini kwa sababu hilo siyo lengo
lao hata kidogo.
Kinyume chake anakumbusha kwamba shirika lake limeitisha
mikutano mingi kulikoni taasisi yoyote hapa nchini Tanzania na hata kuchapisha
taarifa za mikutano hiyo na kuwakaribisha wanaoyahitaji waende ofisini kwake.
Anasema machapisho hayo yamewahusisha watu wa dini zote kama vile Wakristu,
Waislamu, Baahai , Wahindu n.k katika kutafuta amani ya kudumu nchini Tanzania.
Anasema Baraza la Viongozi wa Dini la Kutafuta Amani Tanzania
(IRCPT) ni mshirika wake mkubwa na watu wote makini wanalifahamu hilo hivyo
anasikitishwa na tabia ya kuingiza udini katika shughuli za KAS-Tanzania.
“Nakemea sana kampeni za udini kwani ndizo zimesababisha
majeraha makubwa katika jamii ya Watanzania, viongozi kadhaa wa kiroho
wameshambuliwa, makanisa yamechomwa moto, haya yote ni makovu ya siasa chafu za
uchochezi,” anasisitiza.
Ni dhahiri malalamiko hayo ya Bw. Reith yatarejesha kumbukumbu
kwamba kampeni za udini ziliwahi pia kufanywa na chama hicho hicho bingwa wa
kuwagawa Watanzania kwa manufaa ya muda mfupi kama ilivyofanyika mwaka 2000
dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba akigombea kwa tiketi ya CUF.
Bw Reith anasema njia pekee ya hao wanaoeneza kampeni chafu
dhidi ya shirika lake ni kujibu hoja za wananchi katika masuala kadhaa
yanayoendelea nchini kama vile kwa nini Watanzania wanataka maoni ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba (Tume ya Jaji Warioba),
yazingatiwe, na vile vile mambo mengine kadhaa.
Anawashauri wanahabari kufanya uchunguzi wa kina ili
kuwabaini wanaohusika na uharamia dhidi ya tembo na faru katika mbuga za
wanyama, na hata dhidi ya ufisadi katika maeneo mbali mbali yaliyotajwa katika
sekta za madini, nishati na Benki Kuu ya Tanzania.
Anawasihi wanahabari kutoa msaada wa mawazo kwa serikali ni
jinsi gani inaweza kushughulikia suala la deni kubwa la taifa, tatizo la ajira,
kuanguka kwa sekta ya elimu na hata ubadhirifu katika sekta ya usafirishaji.
Hususani ukwepaji wa kodi bandarini n.k.
Malalamiko ya Bw. Reith yanakuja wakati ambapo makundi mengi
ya wanajamii wakiwamo wasomi, asasi za kiraia na hata viongozi wa kiroho Waislamu
kwa Wakristu, wakidai kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph
Warioba ilizingatia maoni ya wananchi kwa hiyo ni bora yakazingatiwa badala ya
kutanguliza itikadi za vyama.
Ni wakati muafaka sasa kwa watawala na mawakala wao
wakafahamu kwamba katika jamii yoyote iliyostaarabika ni lazima kutakuwapo ni
mijadala yenye kuleta afya na manufaa kwa jamii hata kama mijadala hiyo
haiwafurahishi watawala hao.
Suala la katiba mpya si mali ya CCM, CHADEMA, CUF wala
NCCR-Mageuzi bali ni mchakato wa Watanzania na hivyo hakuna mwenye haki ya kumuita
mwenzake kwamba ni mchochezi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni