Marehemu Nkwabi Ng'wanakilala, mwanazuonii aliyetangulia mbele ya haki
Na Elias Mhegera
Miongoni mwa habari zilizoshtua Watanzania wengi kwa kiwango
kikubwa hivi karibuni ni kifo cha mwanahabari mahiri Nkwabi Ng’wanakilala,
kilichotokea jijini Mwanza na baadaye mwili wake ukaletwa Dar es Salaam kwa
ajili ya maziko.
Kwa kawaida wanapofariki watu wa aina ya mwandishi huyo
mahiri huwa hawajadiliwi wao bali yale waliyoyasimamia. Sitaki kusema hapa
kwamba yeye alikuwa mtakatifu na nikifanya hivyo nitakuwa mnafiki mkubwa.
Lakini kwa upande mwingine ninajiona kwamba nina wajibu wa
kushiriki katika zoezi la kumuaga hapa duniani kwa njia ya kalamu walau hata
kwa sababu moja tu, kwamba alikuwa mwalimu wangu katika Chuo cha Mt. Agostino
jijini Mwanza.
Nasema kwa sababu hiyo moja tu nilitakiwa kuwa sehemu ya
kumuaga walau katika kuuweka mwili wake kaburini, lakini kwa bahati mbaya
sikupata nafasi hiyo kwa sababu zisizozuilika. Lakini labda mimi nina sababu
mbili za ziada za kumuenzi mzee huyo.
Kwa wale waliofundishwa na marehemu Ng’wanakilala masomo
mawili ‘media and democracy’ au ‘media and politics’ hapo ndipo haswa lilikuwa
eneo lake.
Alishangazwa na tabia ya wasomi kuzungumzia somo la maadili
kwa kunukuu mambo ya Ulaya tu kama vile hapa Afrika hapajawahi kuwa na maadili.
Hivyo akaunga mkono watetezi wengine wa maadili ya Kiafrika (Afriethics).
Marehemu huyu gwiji wa habari alipata kuniambia kwamba
niachane na mtindo wa kuandika makala pekee na badala yake nielekeze nguvu
katika uandishi wa vitabu kwa sababu ya utunzaji wa kumbu kumbu za siasa.
Alipendelea kuniita mwalimu kwa sababu nimesoma mara tatu
Chuo cha Mt. Agustino taaluma za uandishi na muda huo huo nikiendelea na ualimu
katika seminari ndogo ya Mt. Maria Nyegezi mahali ambapo pia nilisoma kwa miaka
sita kidato cha kwanza hadi cha sita na kurejea kama mwalimu miaka 19 baadaye
nikafundisha kwa miaka minne.
Akizoea kuniambia; “mwalimu mimi nitabakia mwana CCM daima
lakini hii iliyopo sasa siyo ile ya Mwalimu Julius Nyerere, hii ni ya wachumia
tumbo” kisha aliangua kicheko mara kadhaa alipozungumza mada za aina hiyo.
Sifa moja aliyokuwa nayo ni kwamba yeye alikuwa ni mtu wa
marika yote akiwa na vijana hujiona kana kwamba ni kijana mwenzao na mara
akairejea kwa watu wa makamu yake huongea kwa namna inayostahiki kwa rika hilo.
Mwaka 2005 katika sherehe za kuazimisha uhuru wa habari
ambapo yeye alishirikiana nasi kulikuwa na mchezo wa kuvutana kwa kamba. Kwa
bahati nzuri mzee huyu alikuwa upande wangu na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni
mkuu wa wilaya ya Nyamagana akawa upande wa pili.
Niliwekwa mbele na upande wa pili akawekwa Bw. Emmanuel
Chacha mwandishi wa The Guardian nakumbuka nilipata nguvu za ziada
tukawaangusha wenzetu nguvu zangu kama mtangulizi zilitokana na heshimwa kwa
mzee huyo na wavuta kamba wote wanafahamu mtu wa mbele ni muhimu sana katika
zoezi hilo.
Kwetu sisi tuliobahatika kufundishwa na watu ambao licha ya
kuwa wahadhiri pia wamewahi kushika nyadhifa serikalini basi somo halikuwa
nadharia peke yake bali kubadilishana uzoefu au labda niseme kupokea uzoefu wa
wakongwe hao.
Licha ya Ng’wanakilala alikuwapo Profesa Fortunatus
Lwanyantika Masha ambaye muda mwingine alituchekesha kwamba Mwalimu Nyerere
hakuwaamini watu kama yeye waliosomea Marekani. “nilikuwa na bahati mbaya
Mwalimu aliponiona siku ya kwanza akauliza huyo kijana anatoka wapi? ni
Mtanzania huyo?
Profesa Masha alisema Mwalimu Nyerere aliuliza hivyo kwa
sababu alimuona akitanga tanga kutafuta picha akiwa na kamera mkononi akiwa
amevaa suti za kimagharibi. Kwa hiyo kwa Mwalimu Nyerere maadili ya Kitanzanaia
na hasa kwa viongozi hakuyaangalia katika umiliki wa mali bali hata mavazi yao.
Walimu aina ya Ng’wanakilala na Masha walikuwa wanakumbusha
mara kwa mara kwamba wanahabari wanaweza kuirudisha Tanzania mahali pake,
sielewi ni kwa kiwango gani wanahabari wanatamiza azma hiyo, wasomaji ndiyo wanaweza kutuhukumu.
Marehemu Ng’wanakilala alizoea kusema kwamba misingi ya
mwalimu ilianza kuporomoka pale nchi iliporuhusu mfumo wa vyama vingi mwaka
1992. Anasema kipindi cha mfumo wa chama kimoja viongozi walichunguzwa sana
maadili yao.
Anasema kinyume chake baada ya kuruhusu siasa za ushindani
mafisadi walianza kukifadhili Chama Cha Mapinduzi na kisha watu hao hao
wakatokea kuwa wakwepa kodi wakubwa na wengine wakijihusisha na ufisadi mkubwa
wa aina mbali mbali.
Pia akasema urafiki mkubwa kati ya viongozi wa CCM na baadhi
wafanyabiashara wakubwa ulikuwa unafifisha vita dhidi ya ufisadi. Siku moja
akaja na rundo kubwa la magazeti na kutuambia tusome jinsi mgogoro kati ya
wafanya biashara Yusufu Manji na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Mzee Reginald Mengi
ulivyokuwa unaripotiwa.
Akauliza “nyie wachambuzi mnaona hapo serikali ipo upande wa
nani katika mgogoro huu? je ni kwa nini hali hii inajitokeza? haya ndiyo mambo
mnayotakiwa kujiuliza kama wanataaluma” akasema.
Kipindi kile mara kadhaa vyombo vinavyomilikiwa na IPP Media
viliandika kwamba kulikuwapo na ubia wa kutia mashaka kati ya Mfuko wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF) , CCM na Serikali yake.
Naamini njia mojawapo ya kumuenzi mwanahabari huyo mahiri
itakuwa ni kupambana na ufisadi na pia kuyapitia machapisho pamoja na vitabu
vyake ili kuusambaza ujumbe wake kwa kizazi cha sasa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni