Jumapili, 6 Julai 2014

TATIZO LIPO NDANI WALA SI KAS AU UJERUMANI


26/09/2013 | Elias Mhegera |
KUKATALIWA kwa Balozi mpya wa Ujerumani, Hellwig-Boette, si jambo geni katika ulimwengu wa kidiplomasia, lakini jambo hilo limeacha maswali mengi kuliko majibu.
Maswali hayo yanatokana na ukweli kwamba mwanadiplomasia huyo ameacha rekodi nzuri ya kupinga vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu nchini Kenya.
Inasemekena ni mmoja wa washinikizaji wa kupelekwa The Hague, Uholanzi watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 2007baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya.
Lakini kukataliwa huko kunaacha maswali iwapo kuna uhusiano wa jambo hilo na madai ya kwamba Ujerumani kupitia taasisi yake ya kupigania demokrasia duniani ya Konrad Adaneur Stiftung (KAS), imekuwa nyuma ya mafanikio ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Labda jambo la kushangaza ni kwamba uhusiano kama huo upo pia kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na taasisi nyingine kutoka huko huko Ujerumani ya FES, uhusiano ambao ulianza mwaka 1965.

Pia Chama cha Wananchi (CUF) kina uhusiano na taasisi nyingine kutoka Ujerumani ya FNS tangu mwaka 1997.
Ingawa dhana ya kuamini kwamba mafanikio ya CHADEMA yanatokana na ufadhili kutoka nje ni kiashiria cha uvivu wa kufikiri, lakini pia tukio la kukataliwa kwa balozi huyo kunaonesha kwamba serikali yetu imejikita katika kutafuta mchawi wa nje badala ya kuangalia wapi panapoleta ufa wa kiuongozi ndani ya nchi ili kuuziba ufa huo.
Busara ndogo inatosha kuonesha kwamba kukubalika kwa CHADEMA si zao la misaada ya ‘Wazungu’ au udini na ukabila kama ambavyo watu waliofilisika kimawazo wanavyopotosha umma wa Watanzania.
Kinyume chake ni kwamba ahadi hewa na kushindwa kujibu maswali ya wananchi kwa ufasaha ndicho chanzo cha kuporomoka kwa kasi kwa chama tawala.
Kwa haraka haraka inaonesha kwamba miji yote yenye mikusanyiko mikubwa ya vijana hususan wamachinga ndiyo ngome kuu ya CHADEMA, kwa hiyo hasira ya vijana inatokana na kurubuniwa kama mtoto anavyonyamazishwa kwa ahadi ya pipi kunakofanywa na watawala wetu wakati wa chaguzi kuu.
Ni dhahiri kukataliwa kwa balozi huyo hakutakuwa mwisho wa uhusiano mzuri na wa kihistoria kati ya Tanzania na Ujerumani, kwani yapo mambo mengi yanayoashiria kwamba uhusiano huu una mizizi kuliko upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya wanasiasa wazembe.
Ripoti iliyochapishwa na Mkurugenzi Mkazi wa KAS, Stefan Reith, akishirikiana na mtafiti Danja Bergmann ilileta taharuki ilipochapishwa na magazeti mbalimbali likiwamo Tanzania Daima.
Ndipo wakaibuka waandishi kuijibu ripoti hiyo wakidai kwamba ushirikano kati ya CHADEMA na KAS umejikita katika misingi ya udini, hususan dini ya Kikiristu, ambayo inatuhumiwa kuwa nguvu ya chama hicho kupitia kwa madhehebu mbalimbali ya dini hiyo.
Ni ujinga kuuaminisha umma wa Watanzania kwamba eti uhusiano wa Christian Democratic Union (CDU), KAS na CHADEMA ni wa kidini, sasa ule wa CCM na FES au CUF na FNS ni wa ufisadi, rangi au nini?

Ingawa tunaamini kwamba Watanzania walio wengi kwa sasa wamekwisha kufunguka na hawawezi kudanganywa na propaganada za kijinga kama hizo, lakini pia ipo hofu kwamba zisipokemewa zinaweza kuaminika na kujenga matabaka na chuki katika jamii yetu.
Wakosoaji marafiki wanafanya hivyo kwa sababu nchi wanayoipenda ya Tanzania imeingia katika majanga ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika miaka 50 na zaidi ya uhuru wake.
Matukio ya hivi karibuni yanaogofya, si kwa watalii tu bali hata kwa Watanzania wenyewe. Kwa mfano mtu anaweza kushambuliwa na kuumizwa mwili wake na bado vyombo vya dola vikashindwa kumpata au kuwapata wahusika.
Majanga yaliyotokea na kukosekana kwa wahusika wa uhakika ni pamoja na utekwaji wa Dk. Stephen Ulimboka, kiongozi wa Jumuia ya Madaktari Tanzania, kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na mauaji ya Padri Evarist Mushi huko Zanzibar.

Yapo matukio mengine ya kutisha kama vile mashambulio ya mabomu mara mbili mjini Arusha, moja likiwalenga waamini wa Kanisa Katoliki na jingine kwa wafuasi wa CHADEMA. Lakini pia uchomaji wa makanisa Mbagala na Zanzibar.
Mambo ya uchochezi wa udini kwa malengo ya kisiasa ndiyo yalisababisha mauaji ya Mchungaji Mathayo Kachila wa Kanisa la Pentekoste Buseresere, Geita.
Matukio ya aina hii yanaonesha kwamba dola imeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda raia na mali zao. Kwa hiyo serikali yetu ikikumbushwa na marafiki wa muda mrefu wa nchi yetu kama ilivyokuwa kwa KAS, wasikimbilie kurusha lawama bali wajizatiti pale walipoanguka.
Wale wanaozusha uongo kwamba taasisi kama KAS imedhamiria kuiangusha CCM waangalie upande wa pili kwamba kuna taasisi gani nyingine ambayo imewahi kugharimia mikutano ya maridhiano ya dini mbalimbali hapa Tanzania ikiwa ni Wakristu, Waislamu, Wahindu, Mabudha, Baahai na wengineo kupitia ushirika wa IRCPT.

Itoshe kwa ujumbe huu kusema kwamba kabla watu wasioitakia mema nchi hii hawajaanza kurusha makombora kwa taasisi za wageni wajiangalie na kujitathmini wao kwanza, wabaini chanzo na ndipo wapate ufumbuzi.
Tuwasiliane: mhegera@gmail.com Simu: 0754-826272


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni