Jumatatu, 14 Julai 2014

MZEE BENJAMIN MKAPA ALILEGEZA UZI WA UONGOZI

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin Mkapa 


NB: Makala hii ilitumika katika gazeti la Majira Jumapili May 02, 2008

Na Elias Mhegera

Ufisadi ni tunda la kukengeuka kimaadili, hali hiyo inajitokeza mara kwa mara kwa viongozi wetu, kwa hiyo ni lazima tujiulize mara mbili mbili ni wapi tumepotoka.

Pia tutafakari ni kwa jinsi gani tunaweza kuondokana na hali hiyo. Ufisadi ndiyo unaochangia katika kuongezeka kwa udikteka katika nchi za Kiafrika kwani viongozi waliopo madarakani huogopa kwamba wanaweza kufunguliwa mashitaka mara waondokapo madarakani.

Ni katika mazingira hayo tulishuhudia nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiitwa Zaire chini ya Mobutu Seseko ikigeuzwa kuwa kisima cha wendawazimu  kuchota utajiri wa nchi hiyo bila huruma huku wakiiacha nchi na mashimo matupu baada ya kuchota hazina kubwa ya madini iliyomo nchini humo.

Leo hii DRC ni nchi maskini kama zilivyo nchi nyingi za kiafrika bila kujali ina hazina kiasi gani ya utajiri.Ufisadi ni maradhi mabaya ambayo Watanzania hatuna haja ya kukumbushwa kwa sababu tayari madhara yake tumeyaona.

Mikataba mibovu katika upatikanaji wa tenda mbalimbali kama vile zile za umeme za IPTL, Richmond, Songas, ni mifano michache ya jinsi ambavyo hazina ya taifa inaweza kuchotwa na waroho wachache kwa manufaa yao, na kuwaacha wananchi walio wengi wakiwa wanaumia kwa kukosa huduma muhimu.

Tunapozungumzia tuhuma za ufisadi hatuna maana kwamba watuhumiwa au hata wahusika wanyongwe, wakatwe mikono au wafanyiwe mambo kama hayo bali tunawashawishi tu wapendwa wetu hao warudi kundini ili tuishi tena maisha ya amani na utulivu kama ilivyo utamaduni wetu Watanzania.

Ni imani yangu kwamba hakuna mtu mwenye busara atakayechukia hizi kelele zinazopigwa dhidi ya ufisadi.Ni ukweli usiopingika kwamba hata kama ufisadi unamnufaisha kwa namna gani mtu mmoja na familia yake lakini bado kuna ndugu zake wengi wanaathirika kutokana na ufisadi huo huo.

Leo kuna tuhuma kadhaa ambazo nyingine zipo mahakamani. Kimsingi ni kwamba bado watuhumiwa wanaweza kushinda katika kesi hizo, lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba watu hao wamehujumu mali ya umma.

Ni dhahiri katika nchi ambayo viongozi wake wakuu wengi wamekengeuka kimaadili basi hata mifumo mingine inayotakiwa kuunga mkono mifumo hiyo nayo itaathirika kwa kiwango kikubwa.

Uoza katika jamii huanza kwa kiwango kidogo lakini baadaye husambaa katika maeneo makubwa kama vile ugonjwa.

Kwa vile Mzee Mkapa amestaafu kwa heshima zote, nadhani ni vizuri tukamuacha apumzike, lakini na yeye pia atutendee uungwana kwa haya yafuatayo; akiri kwamba ametenda ndivyo sivyo.

Watanzania walimuamini na kumpatia dhamana ya uongozi kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, hivyo awatambue wakosoaji wake kwamba si maadui zake bali ni watu wenye mapenzi mema na nchi yao. Kuna mazuri mengi lakini kuna mapungufu kadhaa pia aliyoyacha.

Alirudisha heshima ya watumishi wa umma ambao kwa miaka kadhaa walikuwa wanadharaulika kama watu wa chini wasio na kipato baada ya walanguzi kujimilikisha uchumi hasa katika awamu ya pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Katika hilo alipandisha mishahara ya watumishi wa umma na akaanzisha utaratibu wa kujenga majengo mapya kwa ajili ya makazi na ofisi kadhaa za watumishi hali ambayo hakuwapo katika awamu zote zilizomtangulia.

Ni Mkapa huyo huyo aliyehjitahidi kuongeza udahili wa wanafunzzi katika vyuo vikuu, ikiwa ni pamoja na kutoa majengo kadhaa ya serikali kwa baadhi ya vyuo kama vile Chuo Kikuu cha Tumaini, Chuo Kikuu cha Mt. Agostino, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, n.k.

Itoshe tu hapa kuonyesha kwamba wakati tunapotafakari juu ya hatma ya Mkapa tukumbuke pia kwamba yapo mazuri aliyoyafanya.

Lakini kwa upande mwingine ipo historia kivuli ambayo kwa miaka kadhaa haitashahauliuka kwa Watanzania na hasa kwa kuzingatia imani waliyokuwa nayo katika uongozi wake.

Ndiyo maana nimesema lengo la makala hii ni kutaka viongozi wengine wajifunze na kutanabahisha ni kwa nini mtu huyo aliyeanza kwa kupewa sifa zote za usafi ameondoka madarakani na kugubikwa na tuhuma nyingi za ufisadi.

Katika mambo mawili ambayo hata mimi binafsi sikuyategemea kutoka kwa mwanadiplomasia mahili kama yeye ni ‘ukatili’ dhidi ya wapinzani, na hili la kula bila kunawa mikono, yaani ufisadi wa kupindukia.

Ni hapo ndipo ninaona maanguko makuu ambayo yameizika historia nzuri ya utumishi uliotukuka kwa miaka kadhaa. Nitaeleza kwa kifupi juu ya hoja zangu hizo.

Ni imani yangu kwamba si matajiri wote wanaoipenda CCM kwa mapenzi ya dhati bali wamejifunza kutoka kwa wenzao ambao walijiunga na kambi ya upinzania na mambo yao kibiashara yakaharibika kwa  kiwango kikubwa.

Mifano ipo mingi lakini nataka tujikumbushe yale yaliyompata mwandishi mwandamizi Jenerali Ulimwengu ambaye alivuliwa uraia katika misingi ambayo ilijionyesha dhahiri kwamba ni ya kisiasa kutokana na kuikosoa vilivyo serikali ya Mkapa.

Katika mantiki hiyo hiyo tunawaangalia watu kama vile Dkt. Masumbuko Lamwai ambao walijiunga na upinzani.

Dkt. Masumbuko Lamwai alikuwa mwiba mkali pale alipojiunga na NCCR-Mageuzi na kuunda ngome imara ya upinzani akishirikiana na Mabere Marando, Mzee Ndimara Tegambwage, Mch. Kamara Kusupa na wengine kadhaa.
Upinzani wake ulisababisha apoteze wadhifa wake wa uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akafungiwa uwakili Bara , akapoteza udiwani Manzese na hatimaye akabakia mtu wa kuwawaya.

Wapo wengi waliodhurika kutokana na mfumo mbaya wa kisiasa ambao aliujenga Mkapa miongoni mwao ni pamoja na Mwenyekiti wa sasa wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John John Guninita ambaye alikihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.

Mazingira magumu aliyokumbana nayo katika kambi ya upinzani yalimrejesha ‘kikondoo’ katika chama tawala na leo amekumbukwa na kupata wadhifu huo.

Ni Mkapa  huyo huyo aliyeshinikiza Karume awe mgombea wa urais Zanzibar mwaka 2000 wakati alikuwa wa tano katika mchujo wa kura za maoni akitanguliwa na wenzake Dkt. Gharibu Bilali, Marehemu Hassan Diria, Amina Salum Ali na Abdisalam Issa Khatib.

Kwa hali yoyote Mkapa alitakiwa awaachie Wazanzibari waamue nani anayewafaa badala ya kumpitisha kimabavu mtu ambaye labda wao walimuona kwamba hana uwezo wa kuwaongoza.

Mifano mingine michache ni ubabe uliofanywa kwa kupigwa virungu kwa Dkt. Fortunatus Masha katika uchaguzi mkuu wa 2000 huko Sengerema, Mwanza. Tusisahau pia vipigo vya polisi dhidi ya wafuasi wa TLP, dhidi ya mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, n.k.

Tukirejea nyuma kidogo, mara Mzee Ruksa alipoyumba na ikabidi Mwalimu Nyerere aingilie kati, hakusita kusema kwamba Mwinyi binafsi hakuwa mtu mbaya isipokuwa alikuwa na kundi la watu wabaya lilokuwa limemzunguka, je leo mwalimu angewasema akina nani hao?

Tuwasiliane: mhegera@gmail.com,  Na: 0754-826272

             


      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni